Banner

Banner

Imetosha Mdimu

Imetosha Mdimu

FOLLOW US FACEBOOK

propertyfinder.co.tz

Tuesday, September 11, 2012

VILIO VYATANDA KWENYE MAANDAMANO YA WANAHARAKATI IRINGA...! 


           Mmoja wa wanahabari akilia kwa uchungu 

Jeshi la Polisi sasa lipewe mwelekeo mpya ...!

IMEKUWA kawaida sasa kuona habari nyingi zinazochapishwa au kutangazwa na vyombo vya habari kuhusu Jeshi la Polisi nchini, kwa kiasi kikubwa zimekuwa hazionyeshi taswira nzuri kuhusu jeshi hilo. Hali hiyo siyo tu imethibitishwa  na matukio ya kila siku hapa nchini, bali pia na tafiti na tathmini mbalimbali ambazo zimekuwa zikifanywa kila mwaka na taasisi kadhaa zinazoheshimika za hapa nchini na nchi za nje. Tafiti na tathmini hizo zimeonyesha, kwa mfano kwamba jeshi hilo, mbali na Mahakama linaongoza kwa vitendo vya rushwa.
 
Nyingi ya taasisi hizo za kitafiti, ikiwamo Transparency International ya Marekani zimesema, tofauti na taasisi nyingine zilizokubuhu katika vitendo vya rushwa kama ilivyo Mahakama, jeshi hilo pia hutumia mabavu, mateso na vitisho katika kudai rushwa. Na kama hiyo haitoshi, pia taasisi kadhaa za haki za binadamu, ikiwamo Amnesty International ya Uingereza zimefanya tafiti na kutoa ripoti za kila mwaka zinazoonyesha  kwamba jeshi hilo ni mkiukaji mkubwa wa haki za binadamu.
 
Hiyo ndiyo taswira halisi ya jeshi hilo katika nchi yetu. Hivyo, vyombo vya habari vinaporipoti  habari zenye kuonyesha taswira hasi ya jeshi hilo, havifanyi hivyo kwa lengo la kulipaka matope, isipokuwa kuwajulisha wananchi kuhusu mwenendo wake usiofuata maadili na weledi, ili wazishinikize mamlaka husika zifanye mabadiliko stahiki kwa kulisafisha jeshi hilo katika ngazi zote za uongozi. Ni jambo la ajabu kuona Jeshi lililokuwa la mfano barani Afrika baada ya Uhuru wa nchi yetu, kwa maana ya kuwalinda wananchi na mali zao na kuwa kimbilio la wanyonge, linageuka kuwa adui mkubwa wa wananchi kwa kuwatisha, kuwatesa, kuwaua, kuuza haki zao na kuwadai rushwa.
 
Hata vyombo vya habari vingejitahidi kiasi gani kuisafisha, kuiremba na kuipodoa sura ya jeshi hilo katika hali lililomo sasa hakika isingewezekana, kwani sura hiyo imechafuka kiasi cha kutosafishika na kutorembeka tena. Habari za askari polisi kufanya mauaji ya raia wasiokuwa na hatia, au kushiriki katika mitandao ya wizi, uporaji na ujambazi, au kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya, usafirishaji wa binadamu, utapeli na uhalifu mwingine wa kutisha ndizo habari zinazotoka katika jeshi hilo kwa wingi.
  
Hatuoni jinsi jeshi hilo la polisi linavyoweza kuendelea kufanya kazi katika hali na mazingira hasi lililomo hivi sasa kutokana na kupoteza sifa ya kuwa Jeshi la Polisi. Kama wananchi wamefikia hatua ya kupaza sauti zao kwa pamoja na kusema jeshi hilo ni adui yao namba moja, inawezekana kweli askari wake wakavaa sare za jeshi hilo na kutembea kifua mbele kama walinzi wa raia na mali zao? Hivi wanajisikiaje sasa wanapopita  mitaani na kusikia raia wakiguna na kuwabeza tofauti na zamani walipokuwa kimbilio lao?
 
Hoja tunayoijenga hapa ni kwamba jeshi hilo limeacha njia lililotumwa na waasisi wake kuifuata. Jeshi hilo limechafuka na linanuka, hivyo tunadhani njia pekee iliyobaki ni kulibomoa na kulisuka upya kwa kuwafukuza na kuwastaafisha wale wote waliolifikisha hapa lilipo. Kwa kuzingatia ukweli kwamba siyo askari wote waliomo katika jeshi hilo ni wala rushwa, wezi, majambazi au wauaji, ingefaa ufanyike mchakato wa kura za maoni na za siri jeshi humo ili askari waovu watambuliwe kwa majina.
 
Zoezi hilo linaweza kuendeshwa na tume huru itakayoteuliwa na Rais au Bunge. Hata hivyo, yafaa tutambue kwamba kupitisha fagio la chuma pekee hakutoshi kama Serikali haitawaengua askari vihiyo, ili vijana wasomi na wenye uadilifu, ambao wamejaa mitaani bila ajira  wachukue nafasi zao. Tunahitaji jeshi jipya la polisi lenye uadilifu na lililo rafiki wa raia, linalotambua na kuheshimu haki za msingi za kiraia na ambalo mikono ya askari wake haina harufu ya damu ya wananchi waliouawa bila hatia.

Chanzo: Mwananchi

Genge la wahalifu lateka nyara Polisi...!

  • Ni yule aliyeshiriki operesheni Bandarini
  •  Latoa masharti ya kuachiwa huru wenzaoKatika tukio linalofanishwa na vita ya vigogo wa dawa za kulevya dhidi ya mamlaka za serikali nchini Mexico, limetokea nchini kwa askari wa Bandarini jijini Dar es Salaam, Cornel Kufaizalu, ambaye alishiriki katika operesheni ya kukamata watu waliovamia bandari kwa lengo la kuiba madini ya shaba na petroli, kutekwa nyara na watu wasiojulikana ambao pia inadaiwa wametishia kumuua kama masharti yao hayatatimizwa na polisi haraka.

Askari huyo ambaye anaonekana kama shujaa kwa kujitoa muhanga kupambana dhidi ya askari wenzake walioamua kuasi na kujiunga na magenge ya wizi na uhalifu bandarini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki, sasa ametekwa nyara na hajulikani aliko.

Askari huyo alikuwa mwiba dhidi ya watuhumiwa wa wizi wa mali bandarini Dar es Salaam akipambana na watu hao miongoni mwao wakiwamo askari waliokuwa doria na taarifa kuhusiana na sakata hilo zilitolewa na Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe,wakati akizungumza na waandishi wa habari Jumamosi iliyopita.

Taarifa ambazo NIPASHE imezipata ambazo zilithibitishwa na viongozi wa bandari hiyo pamoja na Wizara ya Uchukuzi zinasema kwamba askari huyo alitekwa Septemba 8, mwaka majira ya jioni na watu wasiojulikana ambao wamempeleka kusikojulikana.

Waziri Mwakyembe alipoulizwa kuhusiana na tukio hilo, alisema amepewa taarifa za kutekwa kwa askari huyo ikiwa ni siku moja tu baada ya kukamatwa kwa watu 14 waliovamia bandari usiku wa kuamkia Jumamosi iliyopita.

Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na viongozi na wafanyakazi wa bandari, watu waliomteka askari huyo wametoa masharti kwamba watamuachia huru iwapo tu wenzao watuhumiwa waliokamatwa wakati wa mapambano kati yao na polisi wa bandarini katika tukio hilo wataachiwa huru.

Walisema watekaji hao ambao wametuma ujumbe mfupi wa maneno katika simu ya askari huyo aliyetekwa, wametoa muda wa saa 24 kuachiliwa kwa watu hao waliokamatwa katika tukio hilo na kama hawataachiwa, watachukua uamuzi mwingine dhidi yake.

Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, alisema taarifa walizopata ni kwamba askari huyo amepatikana Mafinga mkoani Iringa.

Wakati Kova akieleza hivyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Michael Kamuhanda, alipoulizwa alisema hana taarifa za askari huyo wa bandari aliyetekwa kupatikana mkoani kwake.
 
Dk. Mwakyembe akizungumza na waandishi wa habari Jumamosi iliyopita baada ya kutokea tukio hilo, aliagiza watu wote waliohusika na wizi huo wakamatwe na kufunguliwa mashitaka, wakiwemo askari waliokuwa doria ambao baada ya kufika eneo la tukio walianza kuiba mafuta badala ya kusaidia askari wa bandarini kupambana na wezi.

Alisema ofisa wa bandarini aliyehusika kufunga kontena namba MSKU 268357(6) ameshafahamika na yeye atakamatwa ili afunguliwe mashitaka.

Akielezea zaidi kuhusiana na tukio hilo, Dk. Mwakyembe alisema Jumamosi usiku kulitokea matukio mawili ya wizi. La kwanza lilitokea saa 9:00 ambalo injini ya treni yenye kichwa namba CK620006 ilikuwa inakwenda bandarini kwa ajili ya kubeba mabehewa manane.

Waziri Mwakyembe alisema kati ya hayo, matano yalibeba mbolea na matatu yalikuwa tupu.
Alisema katika treni hiyo kulikuwa na wafanyakazi wanne ambao ni dereva Abdallaham Shebe (dereva), Bakili Kitanda (muongoza treni), Polisi PC Abubakar mwenye namba F 8784 na msimamizi wa treni Gideon Anyona.

Dk. Mwakyembe alisema wakiwa bandarini, walivunja kontena ambayo ilikuwa na shaba na kuanza kupakua na kuihamishia kwenye makontena ya treni ya Tazara na kufanikiwa kuhamisha vipande 19.

Wakati wakiendelea na harakati hizo, kulizuka mapambano kati ya polisi wa bandarini  na wafanyakazi hao ambayo dereva pamoja na muongozaji walifanikiwa kukimbia na kwenda eneo la Yombo na wengine wawili walikamatwa.

Tukio la pili lililotokea saa 10 alfajiri katika depo ya Oryx ambako kulikuwa na kundi kubwa la watu waliokuwa wanaiba madumu ya mafuta na kuyatupia upande wa pili wa bandarini. Madumu yalikuwa tisa ya lita 20 kila moja lilikuwa na petroli.

Alisema wakati wanaendelea na harakati hizo, polisi waliokuwa doria walifika eneo la tukio na kukuta polisi wa bandarini wakipambana na kundi la wezi, lakini polisi wa doria badala ya kuwasaidia polisi wa bandarini kupambana na wezi hao, walianza kuiba madumu hayo ya mafuta na kuchukua manne na kuondoka nayo.

Aidha, alisema bosi aliyewatuma wafanyakazi kuiba shaba kwenye kontena anaonekana kuwa ni mzoefu hivyo watamkamata kwa sababu wameshamfahamu.

WATU 14 WATIWA MBARONI

Kamanda Kova jana alizungumza na waandishi wa habari na kusema kuwa Septemba 8, mwaka huu majira ya saa 8:00 usiku katika eneo la Shedi No. 7, polisi waliwakamata watu 14 kwa kosa la kuvunja kontena na kuiba vipande 19 vya madini ya shaba, mafuta ya petroli lita 360 na dizeli lita 60.

Aliwataja waliokamatwa kwa kuiba madini ya shaba kuwa ni Askari Polisi kikosi cha Tazara mwenye namba F. 8774  PC Abubakar; Charles Rejino (49), mkazi wa Tandika Azimio;  Range Boaz (40),  mkazi wa Kichemchem Mbagala na Willy Mwamlima (20), mkazi wa Kiwalani.

Wengine ni Ally Rwanda (28), mkazi wa Tandika Azimio; Said Salum (39), mkazi wa Tandika Azimio; Shabani Matimbwa (33), mkazi wa Tandika; Salum Kinyama (34) mkazi wa Tandika Azimio na Gideon Anyina (35) mkazi wa Mbezi Louis.

Kuhusu tukio la wizi wa mafuta ya petroli lita 360 na dizeli lita 60 yaliyoibwa katika yadi ya Oryx, aliwataja waliokamatwa kuwa ni Mohamed Said (18), mkazi wa Mtoni Mtongani na Fadhili Said (18), mkazi wa Mtoni kwa Azizi Ally.

Wengine ni Ailaji Bakari (19), mkazi wa Kurasini na Erasto Adam (18), mkazi wa Kurasini Shimo la Udongo.

Kamanda Kova alisema kimeundwa kikosi kazi cha watu 10 kinachojumuisha askari polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Polisi  bandari na Polisi Tazara kwa ajili ya kuhakikisha kuwa matukio ya wizi  bandarini yanakomeshwa.
 
Chanzo: Nipashe

Mkuu wa Wilaya ya Ruangwa aongoza Mazishi ya Wahanga wa mgodi wa Nandagala...!

Mkuu wa Wilaya ya Ruangwa Mh.Agness Hokororo(kushoto) akiwa karibu na mama mzazi wa Nyang'ana Mkelecha  wakati wa ibada ya mazishi katika Makaburi ya mji Ruangwa.
Nyang'ana ni ni mmoja kati ya wachimbaji walifukiwa na kifusi na kupoteza maisha yao  katika machimbo ya Nandagala Ruangwa Lindi. 

Mh.Agness Hokororo akikabidhi  rambirambi ya Tshs 100,000 kwa wafiwa

Marehemu Nyang'ana Mkelecha  ni mzaliwa wa Bunda - Musoma
Alizaliwa mwaka 1968 katika kijiji cha Isenye Bunda na kupata elimu ya msingi kijijini hapo, ameacha wake wawili na watoto watatu 

Wachimbaji  na Wananchi wakichangisha pesa kwa ajili ya  majeruhi mmoja aliyenusurika kifo (Oswald) aliyelazwa Ndanda Hospital baada ya kuvunjika miguu.

WANAHABARI WAMTIMUA WAZIRI NCHIMBI KATIKA MAANDAMANO YAO...!

Katibu wa Jukwaa la Wahariri Bw. Nevil Meena akiongea kwa uchungu mbele ya wanahabari wenzake ambapo pamoja na maazimio mengine wametangaza kutoandika habari zinazohusiana na jeshi la polisi kwa siku 40. 
Na Datus Boniface.
Wakiwa katika nyuso za huzuni kubwa ya kuondokewa na mwenzao ambaye aliuawa kwa kupigwa na bomu, kundi la Wanahabari wao wamemtimua Waziri wa Mambo ya Ndani Mh. Emmanuel Nchimbi kutokana na kuwaingilia kwenye maandamano yao.
Wanahabari kote nchini leo wamefanya maandamano ya amani kwa lengo la Kulaani mauaji ya mwenzao wa kituo cha Televisheni cha Channel Ten, Daudi Mwangosi.
Kufukuzwa na kuzomewa kwa Waziri Nchimbi kumekuja baada ya kugundulika kuwa ameingilia maandamano kwa lengo la kuyapokea bila kupewa mwaliko.
Kutokana na zomea zomea hiyo ya wanahabari hao dhidi ya Waziri Nchimbi hali ilionekana kuwa si shwari na kupelekea waziri huyo kuondolewa na rais wa UTPC Keneth Simbaya na viongozi wengine wakiwemo askari polisi.
Akizungumza na kundi la waandishi Katibu wa Jukwaa la Jukwaa la wahariri (TEF) Neville Meena amesema “Hatuna ugomvi na Waziri Nchimbi kwani ni mwenzetu, rafiki yetu, ila leo hana vazi la msiba”
Mara baada ya kuondoka bila kupenda Waziri Nchimbi, hali ya utulivu ilikuwa kama kawaida na shughuli zingine ziliendelea kama ilivyopangwa.

Monday, September 10, 2012

Waandishi wa habari kuandamana kesho

Aliyekuwa mwandishi wa Kituo cha Televisheni cha Channel Ten, mkoani Iringa, Daudi Mwangosi

Kufuatia mauaji ya aliyekuwa mwandishi wa Kituo cha Televisheni cha Channel Ten, mkoani Iringa, Daudi Mwangosi, waandishi wa habari nchini wamepanga kufanya maandamano ya amani kesho.
Kauli hiyo ilitolewa jana jijini Dar es Salaam, katika kikao kilichoandaliwa na TEF, chini ya Kaimu Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Nchini (TEF), Theophil Makunga.

Aidha, madhumuni makubwa ya kufanya maandamano hayo ya amani ni kueleza huzuni iliyowapata wadau na tasnia ya habari hapa nchini kufuatia mauaji ya Mwangosi, kwani tangu kupatikana kwa uhuru wa taifa hakuwajawahi kutokea kwa tukio la kusitikisha kama hilo katika tasnia hiyo.

Kwa mujibu wa TEF, jijini Dar es Salaam maandamano hayo yatafanyika kesho kuanzia saa 2:00 asubuhi, ambapo yataanzia ofisi za Channel Ten, kupitia mitaa ya Azikiwe hadi Barabara ya Bibi Titi, na kuhitimishwa katika viwanja vya Mnazi Mmoja ambako mkutano utafanyika.

Maandamano hayo yameratibiwa na vyama vya habari (press clubs) kote nchini na kuhusisha wadau wote wa tasnia ya habiri ikiwa ni pamoja na waandishi wa habari.

Mwangosi alifariki dunia Jumapili wiki iliyopita katika Kijiji cha Nyololo Mufindi, mkoani Iringa na kuzikwa jijini Mbeya, wiki hiyo hiyo, baada ya kuuawa kwa kupigwa na kitu mithili ya bomu lililopelekea mwili wake kusambaa vipande vipande.