Pages

Sunday, September 2, 2012

CRDB YAJIUNGA NA SACCOS...!


VYAMA vya Akiba na Mikopo (Saccos) mkoani Mbeya  vilivyo chini ya vyama vya ushirika, vinatarajia kuanza kunufaika na mfumo mpya wa upatikanaji wa fedha kwa kutumia simu za mkononi (SIM Bank) unaotolewa na benki ya CRDB.

Mfumo huo hutolewa kupitia akaunti za wateja ili kuwarahisishia upatikanaji wa fedha kwa wakati katika matawi yao hasa vijijini na kujikita katika shuguli mbalimbali za ukuaji wa uchumi.

Ofisa Mahusiano wa CRDB tawi la Mbeya, Msafiri Masanula alisema kuwa lengo la kutoa huduma hizo kwa wananchi ni kuwawezeha kupata huduma za kifedha kwa wakati kutokana na wananchi wengi kujihusisha katika shughuli za kilimo na biashara hasa mijini na vijijini .
“Tumeona mfumo huu utawasaidia wananchi wengi zaidi kuachana na dhana ya kupanga foleni, na msongamano wa watu katika benki na kwamba mfumo huu pia watatumia hata kuhamisha fedha kutoka katika akaunti zao kupeleka katika huduma za kifedha za simu za mkononi M-Pesa na Tigo-Pesa popote walipo,” alisema.

Alisema kuwa kabla ya kuanza mfumo huu walitoa elimu kwa wananchi vijijini na mijini kujiunga katika vikundi vya vyama vya akiba na mikopo ili kuweza kukopeshwa fedha na kila mmoja kujianzishia miradi endelevu na kuweka akiba zao katika vyama hivyo ili kujikiwamua kiuchumi miongoni mwao na kuachana na utegemezi.

“Tuna imani huduma hii itawasaidia sana wakulima na wafanyabiashara kwani hata akiwa maeneo yoyote anapata fedha na si kusubiri kufika katika matawi yetu ya kibenki. Bado tutapanua wigo zaidi ili kufika hata maeneo yasiyofikika na kutoa elimu kwa wananchi juu ya umuhimu wa kujiunga katika mfumo huu wa SIM Bank kwa mteja aliye na akaunti na asiye na akaunti CRDB,” alisema Masanula.

Aidha alitoa wito kwa wananchi na wakulima kujiunga katika vyama vya akiba na mikopo ili kuweza kupatiwa mikopo kupitia CRDB ili kujiongezea mitaji na wigo wa kupanua miradi yao kuwa endelevu hususan kurejesha mikopo  hiyo kwa wakati katika vyama vyao ili kuviwezesha kupiga hatua zaidi








No comments:

Post a Comment