THE
UNITED REPUBLIC OF TANZANIA
DIRECTORATE
OF PRESIDENTIAL COMMUNICATIONS
TAARIFA
KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais Jakaya Mrisho Kikwete ameishukuru kampuni ya simu za mkononi
ya Vodacom kwa kuchangia katika mradi wa kuhifadhi mbwa mwitu katika hifadhi ya
Taifa ya Serengeti, mradi unaojulikana kama Vodacom Foundation Serengeti
Wild Dogs Conservation Project, kwa dola za Marekani 450,000 kwa kipindi
cha miaka mitatu.
Rais ametoa shukrani hizo Kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Vodacom hapa
nchini Bw. Rene Meza, Ikulu Dar-Es-Salaam, walipokutana jana jioni,
Ijumaa Agosti 31,2012
"Napenda
kutoa shukrani zangu kwa Vodacom kwa msaada huu mkubwa, tunashukuru kwa
jitihada zenu kubwa katika hili" Rais amesema.
Naye
Mtendaji Mkuu wa Vodacom amemhakikishia Rais kuwa kampuni yake itaendelea
kushirikiana na serikali katika miradi mbalimbali ya maendeleo, elimu na Afya.
“Tunajisikia
faraja sana kuwa miongoni mwa washirika wa mradi huu. Ni heshima kwetu na tuko
makini nao, tunataka kuendelea na mradi huu" Bw, Rene Meza amemhakikishia Rais.
Tayari mbwa mwitu kumi na Moja, wamerudishwa mbugani siku ya
Alhamisi Agosti 30, 2012 baada ya kuhifadhiwa kwenye boma maalumu la
mradi huo, katika eneo la Nyamuma, Magharibi mwa Hifadhi ya Taifa ya
Serengeti, mkoani Mara.
Wadau wengine walioshiriki na kufanikisha zoezi hilo ni pamoja na
Idara ya Wanyamapori, Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (TANAPA), Mamlaka ya Hifadhi
ya Ngorongoro (NCCA), Frankfurt Zoological Society , Grumeti Fund
na Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro.
Kuachiwa kwa Mbwa Mwitu hao 11 walioondolewa katika msitu wa
Samunge wilayani Loliondo ni mojawapo ya juhudi za kurudisha tena makundi ya
wanyama hao katika mbuga hiyo maarufu duniani. Hivi sasa kuna makundi 11
yanayofuatiliwa, manane yakiwa Loliondo na matatu katika Hifadhi ya Ngorongoro,
yakifanya jumla ya Mbwa Mwitu 200.
Mtafiti wa Magonjwa ya Wanyama kutoka Taasisi ya Utafiti wa
Wanyama (TAWIRI) Dkt. Ernest Mjingo, alimwambia Rais Kikwete kwamba katika
Hifadhi ya Serengeti makundi ya Mbwa Mwitu yalikuwa yakionekana kwa wingi,
lakini sasa yametoweka na mara ya mwisho Mbwa Mwitu wawili walionekana mwaka
1998.
Mtafiti huyo alisema Mbwa Mwitu wamekuwa wakitoweka
kutokana na kuuawa kwa sumu na wananchi baada ya kula mifugo yao na
kuugua magonjwa mbalimbali kama kichaa cha mbwa.
Dkt. Mjingo alisema baada ya kuachiwa Mbwa Mwitu hao, waliovishwa collar maalumu zenye redio, juhudi
zitaendelea ili kupata makundi sita yenye Mbwa Mwitu takriban kumi kila moja,
ikiwa ni hatua endelevu ya muda mrefu ya kuhakikisha uwepo wa wanyama hao
mbugani humo.
Mbwa Mwitu ni miongoni mwa wanyamapori ambao wapo hatarini
kutoweka duniani. Takwimu zinaonyesha kuwa katika Bara la Afrika kuna
Mbwa Mwitu wanaofikia 8,000 na Tanzania pekee inakadiriwa kuwa wanyama
hao 3,500 katika mbuga mbalimbali nchini. Katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti
walitoweka kabisa kabla ya juhudi hizi za kuwarejesha kuanza.
Imetolewa na:
Kurugenzi
ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.
No comments:
Post a Comment