Banner

Banner

FOLLOW US FACEBOOK

propertyfinder.co.tz

Monday, November 24, 2014

Serikali yatakiwa kuingilia kati tatizo la ulevi wilayani Rombo mkoani Kilimanjaro

KILIMANJARO serikali imetakiwa kuingialia kati tatizo la ulevi wilayani Rombo mkoani Kilimanjaro  kutokana na tatizo hilo kuendela kushamiri na kuathiri nguvu kazi ya taifa ikiwa ni pamoja na kuchangia ongezeko la watoto yatima na wale waishio katika mazingira magumu.

Rai hiyo ilitolewa jana na Mwenyekiti wa Asasi ya jinsia na maendeleo wilayani Rombo mkoani Kilimanjaro (AJIMARO) Athony Massawe, wakati akikabidhi msaada wa chakula kwa watoto yatima na wale wenye maambukizi ya ugonjwa wa UKIMWI katika kituo cha Cornel Ngaleku kilichopo wilayani humo.

Massawe alisema tatizo la ulevi kwa wananchi wilayani Rombo limeendela kukua siku hadi siku na kwamba ni vema serikali ikaingilia kati  na kulidhibiti, kwani limechangia maambukizi ya ugonjwa wa UKIMWI na kusababisha ongezeko la watoto yatima na wale waishio katika mazingira magumu.

Aidha tatizo hilo limechangia kiwango cha umasikini kuongezeka kwa wananchi wa wilaya hiyo kutokana na vijana wengi ambao ndio nguvu kazi kuathiriwa na pombe hizo kali  na kusahau kufanya kazi kwa ajili ya kujileta maendeleo na kuondokana na hali ya umasikini.

Massawe alisema kutokana na tatizo hilo asasi hiyo imejikita katika utoaji wa  elimu kwa wananchi juu ya adhari za ulevi ikiwa ni pamoja na namna ya kujikinga na maambukizi ya ugonjwa wa UKIMWI ili kuinusuru jamii hiyo.

Katika hatua nyingine Massawe aliitaka jamii, taasisi mbalimbali za kiserikali na zisizo za kiserikali kuguswa na kuona umuhimu wa  kuwasaidia watoto yatima na wale waishio katika mazingira magumu kwani wamekuwa wakikabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ukosefu wa chakula.

Awali akizungumza wakati akikabidhiwa msaada wa chakula hicho Sista Ritha Massawe alisema kituo hicho kinakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ukosefu wa chakula kwaajili ya watoto kutokana na wafadhili wengi kuacha kutoa misaada kutokana na hali ya uchumi kuwa mbaya.

Alisema kwa sasa watoto yatima wengi wameongezeka ikiwa ni pamoja na wale wanaoishi katika mazingira magumu hali ambayo inachangiwa na  ukosefu wa malezi  bora kutoka kwa  wazazi wao kutokana na  kuendekeza ulevi  hivyo kusahau wajibu wao muhimu.

Alisema wazazi wengi wameathiriwa na ulevi jambo ambalo limekuwa likiwaathiri  watoto ndani ya familia na kupelekea watoto kutoroka majumbani na kuishi mitaani na kukosa mahitaji muhimu kama chakula, elimu, mavazi na malezi bora.

Kwa upande wao baadhi ya wananchi wilayani Rombo walisema kwasasa wanawake ndio wanaofanyakazi kutokana na vijana na wanaume kushindwa kufanyakazi kwaajili ya kujiingizia kipato na kwamba wengi huishia vijiweni wakivuta dawa za kulevya na kutumia pombe kali.

Serikali imelenga kuhakikisha kuwa kaya zote hapa nchini zinajiunga na bima ya afya

KILIMANJARO waziri wa Afya na Maendeleo ya Jamii, Dkt. Seif Rashid, amesema serikali imelenga kuhakikisha ya kuwa kaya zote hapa nchini zinajiunga na bima ya afya ili kujikinga na majanga yanayotokana na kuugua au ajali.

Dkt. Rashid ameyasema hayo wakati wa hafla ya kuuzindua mfuko wa bima ya afya ya jamii ulioboreshwa, (iCHF), kwa Mkoa wa Kilimanjaro, iliyofanyika wilayani Siha.

Katika hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Mganga mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Dkt. Mtumwa Mwako, Dkt. Rashid amesema serikali iko katika hatua za mwisho kuupeleka mswada bungeni ambao utalazimisha kila kaya ijiunge katika bima ya afya.

Aidha amesema kuwa serikali inafahamu changamoto zilizoko kwenye huduma za afya hapa nchini na kwamba kwa kutambua hilo, imekuwa ikifanya juhudi mbalimbali ili kuhakikisha inakabiliana na changamoto hizo.

Dkt. Rashid ametoa shukrani zake za dhati na zile za serikali kwa shirika lisilo la kiserikali la nchini Uholanzi la PharmAccess kwa mchango wake mkubwa iliyotoa na inayoendelea kuutoa katika kuiboresha sekta ya afya hususan katika kuuboresha mfuko wa afya ya jamii, (iCHF).

Akizungumza katika hafla hiyo kwa niaba ya Mkurugenzi mkuu wa mfuko wa bima wa Taifa, (NHIF), Mkurugenzi wa iCHF,  Athuman Rehani, amesema NHIF imekasimiwa na serikali mamlaka ya kusimamia mfuko wa afya ya jamii ulioboreshwa, lengo likiwa ni kuboresha afya ya jamii nchini.

Amesema mfuko wa Taifa wa bima ya afya umelenga ifikapo mwaka 2015 asilimia 30 ya watanzania wotw watakuwa wamejiunga na bima ya afya.

Ameongeza kuwa katika kipindi cha Septemba mwaka huu asilimia 16.5 ni wanzania pekee ambao wanatumia biha hiyo.

Kwa upande wake  Mkurugenzi wa Utetezi na utafutaji rasilimali wa PharmAccess,  Kwasi Boahene, amesema kutokana na mafanikio yaliyoonekana wilayani Siha, Shirika hilo limelenga kupanua wigo wa huduma zake kwa wilaya zote za Mkoa wa Kilimanjaro na Mikoa ya jirani ya Arusha na Manyara.

Nae afisa masoko wa Shirika la PharmAceess Edga Masatu amesema kuwa bima hiyo itasaidia jamii kuondokana na dhoruba ya gharama kubwa za matibabu ambazo zilikuwa zikitolewa na hivyo kusababisha wananchi wengi kushindwa kumudu gharama za matibabu.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Siha Rashid Kitambulilo, amesema mpango huo umekuwa na mafanikio makubwa ambapo jumla ya familia 431 wamejiunga na iCHF.

Friday, November 21, 2014

Dowload na kusikiliza wimbo mpya wa Jambo Squad - Mama Klaree

Unaweza kuDownload Mixtape Track toka "Machalii Wa Ara VOL 1" ya Jambo Squad kwa jina " Mama Klaree" HAPA https://mkito.com/song/mama-klaree/3493 Na kwa maelezo/Mahojiano zaidi check na Nao kwa Nambari +255 653 610 249 na +255 762 164 241 follow @odjambo @chaliijambo @jambosquad powered by www.vmgafrica.com @vmgafrica
--
 Jambo Squad-Mama Klaree (Mixtape.Noiz) https://mkito.com/song/mama-klaree/3493

Wananchi watakiwa kujitokeza kujiandikisha kwenye daftari la wapiga kura

KILIMANJARO wananchi katika manispaa ya Moshi mkoani Kilimanjaro wametakiwa kujitokeza kwenye zoezi  la uandikishaji wa  wapiga kura kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika Disemba 14 mwaka huu.

Wito huo ulitolewa jana na Msimamizi mkuu wa uchaguzi katika Manispaa ya Moshi, Shaaban Ntarambe, wakati akizungumza na waandishi wa habari jana ofisini kwake mjini Moshi.

Alisema wakazi wote katika manispaa ya Moshi wanawajibu wa kujitokeza kwa wingi kwenye zoezi la kujiandikisha kupiga kura kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa ili kuweza kutimiza haki ya kikatiba ya kupiga kura na kuchagua viongozi wanaofaa.

Aidha alisema zoezi la uandikishaji wapiga kura linatarajiwa kuanza Novemba 23 mwaka huu na kumalizika Novemaba 29 mwaka huu na kwamba vituo vitafunguliwa saa 1:30 na kufungwa saa 10:00 jioni.

Aliongeza kuwa zaidi ya vituo 102 vitatumika katika zoezi hilo kwenye kata zote 21 na mitaa yote katika manispaa ya Moshi na kwamba halmashauri hiyo imejipanga vizuri kuhakikisha zoezi hilo linafanikiwa.

Katika hatua nyingine Ntarambe alisema ulinzi wa wananchi umeimarishwa katika vituo hivyo na kwamba wananchi wasiogope kujitokeza kwa kuhofia hali ya ulinzi na usalama wao.

Wahamiaji haramu ambao ni raia wa Ethiopia wamekamatwa wakiwa wamejificha vichakani

KILIMANJARO raia wa  nne kutoka nchini Ethiopia wanashikiliwa na Jeshi la Polisi Mkoani Kilimanjaro baada ya kukamatwa wakiwa wamejificha vichakani.

Kamanda wa polisi mkoani Kilimanjaro, Geofrey Kamwela, amethibitisha kukamatwa kwa raia hao na kwamba walikamatwa  tarehe 19 Novemba mwaka 2014, majira ya saa moja asubuhi katika kijiji cha Kileo wilayani mwanga.

Kamanda Kamwela alisema raia hao  walikamatwa  wakiwa katika vichaka vya kijiji hicho wakihangaika kutafuta njia ya kupita.

Kamwela alisema katika upekuzi uliofanywa kwa raia hao hawakukutwa na  chochote wala nyaraka za kusafiria walikuwa hawana.

Alisema raia hao wametokea nchini Kenya na kuingia nchini kwa kutumia njia za panya na kwamba walikuwa wakipita  kuelekea nchini Afrika Kusini.

Kamanda aliwataja wahamiaji hao kuwa ni Tamru Haile(20) Adinal Samwel (17) Tekele Gebure (17)  na Solomon Adise (18) ambapo waliingia nchini kinyume cha sheria.

Alisema kukamatwa kwa raia hao kumetokana  na wananchi waliowaona na kuwatilia mashaka na kutoa taarifa kwa askari.

Wednesday, November 19, 2014

Watu 16 wafikishwa mahakamana kwa kosa la kuchoma moto mali za muwekezaji

 
KILIMANJARO watu 16 ambao ni wakazi wa kijiji cha miti mirefu na Sanya  Juu Wilayani Siha Mkoani Kilimanjaro, wamefishikishwa katika mahakama ya wilaya ya Hai kwa makosa matatu ya  kuvamia shamba la Mwekezaji wa kampuni ya Tanganyika Film and Safari Tawi  la Ndarakwai  na kuchoma mali mbalimbali  zenye zaidi ya thamani ya shilingi  bilioni  1.7

Akisoma hati ya mashtaka mahakamani hapo mwendesha mashtaka Roymax Membe,  mbele ya hakimu mfawidhi wa mahakama hiyo Denis Mpelembwa, amesema kuwa watuhumiwa hao wote kwa pamoja walitenda  makosa hayo  kwa kuvamia shamba la Ndarakwai linalomikiwa na mwekezaji Peter Jones  mnamo Novemba  14   mwaka huu.

Alisema kuwa watuhumiwa hao walitenda kosa la kwanza  la kuingia ndani ya shamba la Ndarakwai na kuchoma magari 6 ya kambi ya utalii ya Ndarakwai  yenye thamani ya shilingi  milioni 450  ambapo ni kinyume na makaosa ya jinai  kifungu cha 299 ya makosa ya jinai ya mwaka 2002.

Amesema watu hao pia walitenda kosa la pili  la kuharibu mali kwa makusudi za mwekezaji huyo,  zenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 1   ambapo kosa la tatu watuhumiwa hao walichoma mali za mwekezaji huyo zenye thamani ya shilingi milioni 210  kinyume na kifungu cha 326 (i) ya makosa ya jinai ya mwaka 2002.

Membe aliwataja watuhumiwa hao ambao wamefikishwa katika mahaka hiyo kuwa ni Matey Hilita (42), Julias Daudi (45), Elipokea Sefano (42), Andrea Elias (67), Alex filipo (30),  Victor Joakimu (32), Dicksoni Mallya (38), wote wakazi wa kijiji cha Miti Mirefu.

Wengine waliofikishwa mahamakani ni Dicksoni Kweka (62), Emanueli Isaya (17), wakazi wa Sanya Juu, Erick Wilsoni (27), Rael Paulo (26), Bibiana Charles (36), Hellen stepahano (39), Hellen Daudi (26), na Monika Rongai (42) wote wakazi wa kijiji cha Miti Mirefu.

Hata hivyo mwendesha mashtaka huyo aliieleza mahakama hiyo kuwa upelelezi wa kesi hiyo haujakalika na kuiomba mahakama kutowapa dhamana watuhumiwa hao kutokana  na thamanani halisi ya vitu vilivyoharibu bado haijajulikana.

Hata hivyo  watumuhiwa wote wamekana mashtaka hayo, na  hakimu Mpelembwa alikubali ombi la mwendesha mashtaka huyo na  kutoa siku saba awakilishe thamani halisi ya uharibifu huo na kesi imeairishwa hadi tarehe 2 Desemba mwaka huu itakapotajwa tena.

Afungwa jela maisha kwa kosa la kumlawiti mtoto wa miaka saba

 
KILIMANJARO hakimu  mkazi mfawidhi wa Mahakama ya wilaya ya Rombo mkoani Kilimanjaro, Naomi Mwerinde, amemhukumu  Evarist Arobogast (24) kifungo cha maisha  jela baada ya kukutwa na kosa la kumlawiti mtoto wa miaka saba na kumuumiza vibaya sehamu za siri.

 Hakimu mwerinde alisema mshtakiwa huyo mkazi wa kijiji cha kirongo juu wilayani Rombo atatumikia kifungo cha maisha jela baada ya kupatikana na hatia ya kumlawiti mtoto wa miaka saba.

Mwendesha mashtaka wa Polisi, Raymond Sikukuu aliieleza mahakama kuwa mshtakiwa  alimvamia na kumlawiti mtoto huyo wa miaka saba  na kumuumiza vibaya sehemu za siri.

Sikukuu alidai kuwa mnamo tarehe 24 machi mwaka huu katika kijiji cha kirongo juu Usseri ambapo mtoto huyo alifanyiwa kitendo hicho cha kikatili na kumsababishiwa maumivu makali sehemu zake za siri.

Mwendesha mashtaka huyo alisema mtuhumiwa alitenda kosa hilo kinyume cha sheria ya 154 sura 16 ya kanuni ya sheria ya adhabu iliyofanyiwa marekebisho  mwaka 2002.

Akitoa hukumu hiyo hakimu Mwerinde alisema  kuwa baada ya kusikiliza ushahidi wa pande zote  mbili upande wa mashtaka umeweza kuthibitisha shtaka hilo pasipo kuacha shaka.

Hakimu huyo alisema  pia maelezo ya daktari yaliyowasilishwa mahamani hapa  imeonesha kuwa mtoto huyo alifanyiwa kitendo hicho cha kikatili.

Hakimu Mwerinde alisema  kuwa vitendo vya ubakaji na ulawiti katika wilaya ya Rombo vimeshamiri kwani katika mahakama hiyo zipo kesi nyingi za kulawiti.

Alisema  kuwa kutokana na hali hiyo mshtakiwa atatumikia kifungo cha maisha jela ili iwe fundisho kwake na kwa watu ambao wamekuwa wakifanya vitendo hiyo kwa watoto wadogo.