Banner

Banner

FOLLOW US FACEBOOK

propertyfinder.co.tz

Wednesday, June 27, 2012

CHAMA cha Wanunuzi wa Kahawa Tanzania, kimewajia juu Wabunge

 

CHAMA cha Wanunuzi wa Kahawa Tanzania (TCBA), kimewajia juu Wabunge wanaomshinikiza Waziri mkuu, Mizengo Pinda atangaze kupiga marufuku ununuzi wa kahawa mbivu nchini.
Katibu mkuu wa TCBA,Eric Ng’maryo aliwaambia wanahabari mjini Moshi jana, Waziri mkuu anapaswa kushauriwa vizuri na wasaidizi wake kwa vile kutoa tamko kama hilo ni kinyume cha sheria.
“nimefuatilia kwa karibu hoja zilizoibuliwa Bungeni na waheshimiwa Wabunge wawili wa mkoa wa Mbeya lakini namsihi Waziri mkuu kuwa suala hilo liangaliwe kisheria na si kisiasa”alisema Ng’maryo.
Kwa mujibu wa Ng’maro, biashara ya kahawa nchini inatawaliwa na sheria ya tasnia ya kahawa ya mwaka 2001 na kanuni zake na kama ni kuzitengua, ni lazima utaratibu uliozitunga ufuatwe.
Alisema kuwa uamuzi huo wa wadau wote ambao ni pamoja na wanunuzi binafsi, wakulima wadogo na wakubwa, wasafirishaji nje ya nchi ndio unaompa nguvu ya kisheria Waziri kutunga kanuni.
Katibu mkuu huyo alisema maamuzi ya wadau ya kutaka kuendelea kwa biashara ya kahawa mbivu, yalitungiwa kanuni na Waziri wa Kilimo na kanuni hizo zilipata nguvu ya kisheria Mei 25 mwaka huu.



Ng’maryo alisema kanuni hizo zilitangazwa kwenye gazeti la serikali kwa G.N namba 187 la Mei 25 na kuhoji”Waziri anahusikaje na kanuni hizi…haya ni makubaliano ya wadau tusipotoshe umma”.
Kuhusu suala la ununuzi wa kahawa mbivu kuwa linamnyonya mkulima, Ng’maryo alisema hiyo ni dhana potofu na propaganda chafu ili kuua ushindani wa kibiashara mkoani Mbeya.
Ng’maryo aliwataka wanaopotosha suala hilo kutokana na maslahi binafsi waache kuwayumbisha wakulima na wakulima waachwe wenyewe kuamua wauze kahawa yao katika hatua gani.
Wakati wakichangia mjadala wa hotuba ya bajeti ya waziri mkuu unaoendelea Bungeni, Mbunge wa Mbozi Mashariki, Godfrey Zambi na Rungwe Magharibi, David Mwakyusa walipinga biashara hiyo.
Zambi alienda mbali na kusema hataunga mkono bajeti hiyo kama hatapata majibu stahiki huku Mwakyusa akitaka Waziri mkuu kupiga marufuku biashara hiyo wakati akihitimisha hotuba yake.
Wakati hayo yakijiri, taarifa zilizopatikana baadae jana zilisema wakulima wilayani Mbozi wametuma ujumbe wa watu 15 kwenda kumuona waziri mkuu wakipinga mapendekezo ya Zambi na Mwakyusa.

No comments:

Post a Comment