JESHI la Polisi Zanzibar linawashikilia wafanyakazi sita wa meli
ya MV Skagit akiwemo mmiliki wake Saidi Abdulrahman pamoja na nahodha
wa meli hiyo, Mussa Makame Mussa, wanahojiwa na polisi.
Watuhumiwa hao walikuwa wakihojiwa katika Ofisi za Upelelezi Makao
Makuu ya Jeshi la Polisi mjini Zanzibar
ambapo Naibu Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai Zanzibar, ACP Yusuph
Ilembo, amesema watuhumiwa hao watafikishwa mahakamani kujibu mashtaka
yanayowakabili.
Kamanda Ilembo amesema kuwa makachero wa polisi wanaendelea na
uchunguzi na kutafuta taarifa nyingine zinazohusiana na tukio hilo.
Hata hivyo, nahodha wa zamu siku ya tukio hilo la kupinduka na kuzama
kwa meli hiyo ya MV Skagit, Mussa Makame Mussa, ameelezea kwa ufupi
jinsi ajali hiyo ilivyotokea na namna yeye alivyonusurika.
Alisema ajali hiyo ilitokea baada ya kupigwa na dhoruba na mawimbi
yaliyoambatana na upepo mkali, ambapo yeye alinusurika kufa maji baada
ya kuruka kwa kutumia mlango wa mbele wa meli hiyo na kuanza kuogelea
ambapo alijichanganya pamoja na abiria wengine walionusurika na
kuokolewa na vyombo vya uokozi.
Wakati huohuo, wapiga mbizi wa vikosi vya ulinzi na usalama leo
wamefanikiwa kuzipata maiti nyingine tano akiwemo mwanamke mmoja na
wanaume wanne.
Katika upekuzi wa maiti hizo, makachero wa polisi walibaini
kitambulicho cha kupigia kura kutoka kwa mmoja wa marehemu kilichokuwa
na jina la Philip John Busiya aliyezaliwa mwaka 1977 katika kijiji cha
Mapilinga, kata ya Igokelo, wilaya ya Misungwi, mkoani Mwanza.
Kupatikana kwa miili hiyo, kunaifanya idadi ya maiti kufikia 73. Maiti
nyingine 68 zilipatikana siku za mwanzo baada ya kutokea kwa ajali hiyo
ambapo kati ya hizo, maiti 54 zilitambuliwa na kuchukuliwa na ndugu na
jamaa kwa ajili ya mazishi.
Maiti hiyo iliyopewa namba 72, pamoja na maiti nyingine nne, zimezikwa
katika makaburi ya pamoja ya Kama yaliyoko nje kidogo ya mji wa
Zanzibar.
Eneo hilo la Kama pia lilitumika kwa kuwazika watu wengine waliokosa
ndugu wakati wa ajali ya meli ya Spice Islander iliyotokea Septemba 9,
2011.
Kupatikana kwa miili hiyo kumetokana na juhudi zinazoendelea kwa
kuvishirikisha vikosi vya ulinzi na usalama, wazamiaji wa makampuni
binafsi pamoja na Mamlaka ya Bandari Zanzibar wakati wakiwa katika
harakati za kuitafuta boti hiyo ili kuweza kubaini kama kuna miili
mingine iliyosalia kwenye meli hiyo chini ya bahari.
Aidha, juhudi za kutaka kuiibua meli hiyo zinaendelea ambapo wazamiaji
wa JWTZ, polisi, KMKM, JKU, Bandari na wale wa makampuni binafsi na
wale wa kujitegemea wakiendelea na kazi ya kutafuta mahali ilipo meli
hiyo ili kuona kama wataweza kupata miili mingine iliyonasa kwenye
vyumba vya meli hiyo ambayo imekokotwa na maji kutoka eneo ilipozama.
na Mohammed Mhina, Zanzibar
|
No comments:
Post a Comment