Donald Mathew (Dunga) alipokutwa amening'inia kwenye kitanzi, pembeni ni maaskari waliofika kushuhudia tukio hilo,
Siku chache
kabla ya kifo chake askari polisi mwenye namba F 3276, Donald Mathew (33),
aliyejinyonga juu ya mti katika daraja la Shani, mkoani Morogoro alimwandikia
barua Waziri wa Mambo ya Ndani kueleza kinachodaiwa kuwa ni ufisadi unaofanywa
na vigogo wa polisi nchini, imebainika.
Polisi huyo aliyefahamika sana kwa jina la
Dunga aliwahi kutoa tuhuma nzito dhidi ya maofisa, wakaguzi na polisi wa
kawaida, mkoani Morogoro mwaka jana lakini hakuna hatua zilizochukuliwa dhidi
ya maofisa hao.
Kamanda wa
Polisi Mkoa wa Morogoro, Fustine Shilogile, jana alisema jeshi hilo, lilipokea
taarifa za kujinyonga Mathew jana asubuhi.
Alisema askari huyo, aijinyonga kwa kutumia
vipande vya kamba ya kanga ambavyo viliunganishwa na hakuacha ujumbe wowote
unaoeleza sababu ya kuchukua uwamuzi huo.
Alisema askari huyo kabla ya kufanya tukio
hilo, alionekana mitaani akinywa pombe katika Baa ya Shani.
Alisema baada ya kuonekana amelewa, Mathew
aliamua kuvua nguo zote na kubaki mtupu, kitendo kilichofanya baadhi ya askari
polisi waliokuwa eneo hilo, kumfuata na kumsihi avae nguo.
Alisema marehemu, alihamishiwa mkoani Singida
kikazi, lakini Novemba, mwaka jana aliamua kuacha jeshi.
“Pamoja na kwamba marehemu aliacha kazi mwaka
jana, sisi kama jeshi bado tunamtambua kama askari mwenzetu… kwa msingi huo
tutasafirisha mwili wake Agosti 8, mwaka huu kwenda nyumbani kwake mkoani
Kilimanjaro,” alisema Kamanda Shilogile.
Alipoulizwa kama kifo cha Mathew
kimesababishwa na baadhi ya askari waliohusishwa kwenye tuhuma za kuhusika na
biashara za dawa za kulevya, Kamanda Shilogile alisema uchunguzi unaendelea, na
kwamba ikibainika kama kuna askari aliyehusika atachukuliwa hatua kali.
Hata hivyo, askari huyo mwishoni mwa mwaka
jana, alitoa tuhuma mbalimbali ambazo zilichapishwa katika moja ya magazeti
linalotoka mara mbili kwa wiki, zikiwatuhumu askari 9 wa kikosi cha kupambana
na majambazi wa kutumia silaha kupokea rushwa kutoka kwa wafanyabiashara wa dawa
za kulevya.
Tuhuma nyingine alizotoa ni polisi kukamata
majambazi wenye silaha, lakini huachiwa baada ya kupewa fedha na mali
mbalimbali, hivyo kushindwa kuwafikisha kituoni.
Alisema tuhuma nyingine ni polisi kuwakamata
wafanyabiashara wa pombe haramu aina ya gongo na bangi bila kuwachukulia hatua
zozote baada ya kuhongwa.
Tuhuma nyingine, zinazodaiwa kufanywa na
askari hao ni kushirikiana na matapeli, kutapeli raia wa kigeni na kushirikiana
na majambazi kuvunja maduka na kuiba mali za wafanyabiashara nyakati za usiku.
No comments:
Post a Comment