Banner

Banner

FOLLOW US FACEBOOK

propertyfinder.co.tz

Saturday, August 18, 2012

RUFAA YA GODBLESS LEMA (CHADEMA) YAPIGWA TAREHE...!

Godbless Lema
RUFAA ya kupinga kuvuliwa ubunge ya aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Arusha Mjini, Godbless Lema (CHADEMA), imepangwa kusikilizwa Septemba 20, mwaka huu, mbele ya majaji watatu wa Mahakama ya Rufaa; Natalia Kimaro, Mbarouk Salim Mbarouk na Salumu Massati.
Kwa mujibu taarifa za kikao cha Mahakama ya Rufaa cha Arusha, rufaa hiyo iliyofunguliwa na Lema akipinga uamuzi uliotengua ubunge wake kufuatia shauri lililofunguliwa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, inatarajiwa kusikilizwa kwa siku moja ambapo baada ya hapo itapangwa tarehe kwa ajili ya kutoa uamuzi.
Awali, Lema kupitia wakili wake, Method Kimomogoro, aliwasilisha kwenye mahakama hiyo hoja 18 za madai akipinga kutenguliwa kwa ubunge wake na Mahakama Kuu Kanda ya Arusha Aprili 5, mwaka huu.
Kwenye baadhi ya madai hayo, Lema aliiomba Mahakama ya Rufaa kutengua uamuzi wa Mahakama Kuu, uliotengua ubunge wake, huku akiitaka imtangaze kuwa mbunge halali wa Jimbo la Arusha Mjini.
Aidha, aliitaka mahakama hiyo ya juu, iwaamuru walalamikiwa katika shauri hilo walipe gharama za rufaa hiyo pamoja na zile za kesi iliyomalizika kwenye Mahakama Kuu Kanda ya Arusha.
Katika madai mengine, Lema anamlalamikia, Jaji Gabriel Rwakibarila, aliyesikiliza kesi hiyo kuwa, alitoa uamuzi wake kwa kuzingatia maneno ya uvumi, huku akipuuza ushahidi uliotolewa mahakamani hapo.
Lema anadai kuwa, Jaji alikosea wakati alipoamua kuwa mpiga kura yeyote anaruhusiwa kupinga matokeo ya uchaguzi hata kama haki zake za msingi hazijaguswa.
Kesi hiyo iliyotengua ubunge wa Lema, ilifunguliwa na wanachama watatu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM); Mussa Mkanga, Agness Mollel na Happy Kivuyo, wakidai kuwa wakati wa kampeni mbunge huyo alimdhalilisha mgombea mwezake, Dk. Batilda Burian kwa kutumia lugha za matusi.

ANGALIZO
Jaji Mbarouk Salim Mbarouk ni yule aliyeonekana kutajwa kwa namna isiyo nzuri kwenye utetezi wa Tundu Lisu au ni mwingine? na kama ni yeye hiyo haitaleta tena kutoridhika iwapo maamuzi hayatakuwa upande wa Lema na Chadema? nini mawazo yenu katika hili?

No comments:

Post a Comment