Banner

Banner

FOLLOW US FACEBOOK

propertyfinder.co.tz

Sunday, September 2, 2012

Afisa Uhamiaji Mara atishia kumchoma kisu mfanyakazi wa idara hiyo...!

Afisa Uhamiaji Mkoa wa Mara Jacob Sambai anadaiwa kumtisha kwa kumchoma kisu mfanyakazi wa Idara hiyo kwa madai ya kutoa siri za bosi huyo kuwa na mahusiano ya kimapenzi na binti mmoja wa idara hiyo.

Taarifa zinasema kuwa vitisho hivyo dhidi ya Moses Malekela, vilitokea Agosti 24, mwaka huu saa 8 mchana baada ya bosi huyo kupokea malalamiko kutoka kwa afisa mmoja ndani ya ofisi hiyo aliyekuwa akituhumiwa na binti huyo kuwa anatoa taarifa za kuwa na mahusiano ya kimapenzi na bosi huyo.

Kufuatia kuwepo kwa taarifa hizo, ndipo bosi huyo alipoitisha kikao cha dharura kwa kuwahusisha msaidizi wake DCI Milinga, maafisa waliohusika na tuhuma hizo pamoja na maafisa wengine kama mashahidi.

Katika kikao hicho maafisa hao kila mmoja alijieleza kwa muda wake huku wakisisitiza kuwa taarifa hizo zimeenea ofisini na kila mtumishi anajua kuwa bosi anatembea na mmoja wa wafanyakazi katika idara hiyo.

“Bosi mimi na mwenzangu tunaotuhumiwa kusambaza uvumi huo hatukuwepo ofisini kwa muda mrefu, tulikuwa masomoni tuliporipoti na sisi tukayakuta hayo maneno. Fanya uchunguzi,” alisikika mtumishi mmoja akisema.

Baada ya kusikiliza watumishi wote waliokuwepo katika kikao hicho ndipo bosi huyo akapandisha jazba na kuvuta droo yake na kuchomoa kisu kikali na bisibisi na kutaka kumchoma afisa huyo, hatua iliyofanya msaidizi wake akishirikiana na maafisa wengine waliokuwepo kwenye kikao hicho kumzuia na kuamua kuweka kisu chini na kuvua saa yake ya mkononi tayari kwa kumpiga ngumi afisa huyo huku akisema, “leo kazi na iishe”
Tafrani hiyo ilichukua takribani dakika 10 ambapo bosi huyo akitaka kuonyesha umwamba wake lakini busara za msaidizi wake na maafisa waliokuwepo kumzuia bosi huyo na baada ya kuona amezidiwa nguvu ndio akamtolea kauli ya vitisho huku akisema “haina shida, ntakutafuta mtaani”

Kauli hiyo ilimtisha mtumishi huyo na kuamua kutoa taarifa kituo kikuu cha Polisi Musoma kwa RB NO MUS/RB/5872/2012 na vyombo vingine vya ulinzi na usalama ngazi ya mkoa ili kulinda usalama wa maisha yake.

Akiongea kwa njia ya simu na mwandishi wa habari hii, Kamanda wa jeshi la Polisi mkoa wa Mara Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Jeshi hilo, Abslom Mwakyoma, alisema kuwa tayari suala hilo limefika katika kituo hicho na linafanyiwa uchunguzi kabla ya hatua zaidi za kisheria kuchukuliwa

Naye Afisa Uhamiaji huyo alipoulizwa kwa njia ya simu kuhusu sakata hilo alisema kuwa tayari limefikishwa kwenye vyombo vya sheria hivyo ni vyema likafanyiwa kwanza uchunguzi.

No comments:

Post a Comment