Utangulizi
Ndugu
Wananchi;
Kila
mwisho wa mwezi nimekuwa nazungumza na taifa kuhusu masuala mbalimbali muhimu
kwa taifa letu na watu wake. Leo nina
mambo mawili ya kuzungumza nanyi.
Lakini, kama ilivyo mazoea yetu hatuna budi kwanza tumshukuru Mwenyezi
Mungu, muumba wetu, kwa kutujaalia baraka zake, za uhai na uzima na kutuwezesha
kuwasiliana leo tarehe 31 Agosti, 2012.
Ndugu
Wananchi;
Jambo
la kwanza ninalotaka kuzungumzia leo ni zoezi la Sensa ya Watu na Makazi
lililoanza tarehe 26 Agosti, 2012 ambalo linatarajiwa kumalizika tarehe 01
Septemba, 2012. Mtakumbuka kuwa tarehe
25 Agosti, 2012 nilizungumza nanyi na kuwaomba mjitokeze kwa wingi na muwape
ushirikiano unaostahili Makarani wa Sensa watakapopita majumbani mwenu
kutekekeza wajibu wao. Tumebakisha siku
moja kufikia kilele cha sehemu ya kwanza ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka
2012.
Napenda
kuwashukuru kwa dhati Watanzania wenzangu wote kwa kujitokeza kwa wingi
kuhesabiwa. Mpaka sasa mwelekeo ni mzuri
na ugumu ulioonekana kuwepo pale mwanzoni uliendelea kupungua siku hadi siku
kadri utekelezaji wa zoezi ulivyokuwa unaendelea. Kwa mwenendo huu nina matumaini makubwa kuwa
Sensa ya mwaka huu itakuwa na mafanikio mazuri.
Ndugu Wananchi;
Napenda
kutumia nafasi hii kutoa wito kwa wale wote ambao hawajahesabiwa wafanye hivyo.
Naomba waitumie siku moja iliyosalia yaani tarehe 1 Septemba, 2012 kufanya
hivyo. Aidha, namuomba Mkurugenzi Mkuu
wa Ofisi Kuu ya Takwimu ya Serikali ya Muungano na Mtakwimu Mkuu wa Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar kuhakikisha kuwa kasoro zo zote zilizopo mahali po pote
zinatafutiwa ufumbuzi ili mambo yakamilike bila upungufu wowote.
Ndugu
Wananchi;
Baada
ya kazi ya Makarani wa Sensa kuhesabu watu kufikia kilele chake, tarehe 2
Septemba, 2012, linaanza zoezi la kuwashughulikia wale ndugu zetu ambao
watakuwa bado hawajahesabiwa. Itakuwepo
fursa ya siku saba kwa watu hao kuhesabiwa.
Watatakiwa wao wenyewe kupeleka taarifa zao kwa Wenyeviti wao wa
Serikali za Mitaa au Vijiji. Taarifa
hizo zitafikishwa kwa Kamishna wa Sensa kwa ajili ya kujumuishwa. Baada ya muda huo kwisha, zoezi la kuhesabu
watu litakuwa limefika mwisho. Yule
ambaye atakuwa hakutumia fursa hizo mbili atakuwa amekosa kuingizwa katika
hesabu ya Watanzania ya mwaka 2012.
Napenda kuwasihi ndugu zangu, Watanzania wenzangu kutumia siku ya tarehe
1 Septemba, 2012 kuhesabiwa na kama
hapana budi basi tumia fursa ya kupeleka taarifa zako kwa Mwenyekiti wako wa
Mtaa au Kijiji katika siku saba zinazofuatia siku hiyo ili nawe ujumuishwe.
Ndugu
Wananchi;
Baada
ya kazi ya kuhesabu watu kwa namna zote mbili kufikia mwisho, itaanza kazi ya
uchambuzi na kuunganisha takwimu na taarifa zilizokusanywa. Kazi hiyo ni muhimu na ni kubwa hivyo inahitaji
umakini na uangalifu wa hali ya juu sana, kwani ikikosewa zoezi zima la Sensa
litaingia dosari. Nafarijika
kuhakikishiwa na Viongozi wa Sensa na Wakuu wa Idara za Takwimu za Serikali
zetu mbili, kwamba wanatambua ukweli huo na wajibu wao. Wameniarifu kwamba kama mambo yatakwenda kama
ilivyopangwa, matokeo ya awali ya Sensa ya Watu na Makazi kuhusu idadi ya watu
na jinsia zao yatatolewa mwishoni mwa mwaka huu. Taarifa nyingine zitafuata
baadaye. Narejea kuwasihi Watanzania
wenzangu kuwapa nafasi wataalamu wetu wafanye kazi yao kwa ufanisi ili tupate
matokeo yaliyo sahihi.
Mpaka
na Malawi
Ndugu
Wananchi;
Jambo
la pili ninalotaka kuzungumza nanyi leo ni kuhusu mpaka baina ya Tanzania na
Malawi katika Ziwa Nyasa. Kama mjuavyo, kwa
miaka mingi nchi zetu mbili zinatofautiana kuhusu wapi hasa mpaka uwe. Sisi, Tanzania, tunasema mpaka upo katikati
ya ziwa wakati wenzetu wa Malawi wanasema upo kwenye ufukwe wa ziwa upande wa
Tanzania. Kwa maneno mengine wanasema ziwa
lote ni mali ya nchi yao.
Utata kuhusu mpaka wetu katika Ziwa
Nyasa haujaanza leo. Ulikuwepo tangu
wakati nchi zetu mbili zikiwa bado zinatawaliwa na wakoloni na kuendelea baada
ya Uhuru wa nchi zetu mpaka sasa. Jambo
kubwa lililo tofauti na jipya ni kwamba hivi sasa, nchi zetu mbili zimeamua
kukaa mezani na tunalizungumza suala hilo.
Chimbuko
la Mzozo
Ndugu
Wananchi;
Chimbuko la mzozo wa mpaka uliopo
sasa, baina ya nchi zetu mbili jirani, rafiki na ambazo watu wake ni ndugu, ni
makubaliano baina ya Waingereza na Wajerumani kuhusu mpaka baina ya nchi zetu
yaliyofanywa tarehe 1 Julai, 1890. Makubaliano
hayo yajulikanayo kama Mkataba wa Heligoland, (The Anglo-Germany Heligoland
Treaty) yalitiwa saini kule Berlin, nchini Ujerumani baina ya Waingereza na
Wajerumani. Wakoloni hao walikubaliana
kuhusu mipaka baina ya makoloni yao na baina yao na wakoloni wengine
waliopakana nao. Kwetu sisi hayo ndiyo
makubaliano yaliyoweka mipaka ya Tanganyika na ile ya Zanzibar na majirani zake. Kwa upande wa Ziwa Nyasa, Waingereza na
Wajerumani walikubaliana kuwa mpaka uwe kwenye ufukwe wa nchi yetu. Kwa maana hiyo ziwa lote likapewa nchi ya
Malawi. Kwa upande wa Mto Songwe mpaka
ulikuwa ufukweni upande wa Malawi kwa maana hiyo mto wote ukawa upande wa
Tanzania.
Ndugu Wananchi;
Katika kipengele cha Sita
(Article VI) cha Mkataba huo, wakoloni hao walikubaliana kufanya marekebisho ya
mpaka mahali po pote kama itakuwa ni lazima kufanya hivyo, kulingana na
mazingira na hali halisi ya mahali hapo.
Kwa mujibu wa kutekeleza matakwa ya kipengele hicho mwaka 1898 Tume ya
Mipaka iliundwa. Ilianzia kazi katika Mto
Songwe kuhakiki mpaka baina ya nchi yetu na Malawi. Tume ilikubaliana kuhamisha
mpaka kutoka ufukweni mwa Mto Songwe upande wa Malawi na kuwa katikati ya
mto. Baada ya uhakiki katika eneo hilo
kukamilika, mwaka 1901 mkataba mpya ulisainiwa kuhusu mpaka huo.
Tume iliendelea na kazi yake katika Ziwa
Tanganyika na kuhamisha mpaka kutoka ufukweni hadi katikati ya ziwa na mkataba
mpya kusainiwa mwaka 1910. Tume iliendelea
katika ziwa Jipe ambapo mpaka ulihamishwa pia hadi katikati ya ziwa.
Ndugu Wananchi;
Bahati mbaya Tume hiyo
haikufanikiwa kufanya uhakiki wa mpaka katika Ziwa Nyasa kutokana na kutokea
kwa Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia kati ya mwaka 1914 - 1918. Kama tunavyokumbuka, Waingereza na Wajerumani
waligeuka kuwa maadui na kupigana hata hapa nchini. Baada ya vita hivyo na Ujerumani kushindwa, Baraza
la Umoja wa Mataifa (The League of Nations) liliikabidhi Uingereza udhamini wa Tanganyika.
Hivyo, Uingereza ikawa inatawala Malawi na Tanganyika.
Ndugu Wananchi;
Wakati Tume ya Uingereza na
Ujerumani ilipokuwa imekufa, Tume ya Mipaka kati ya Uingereza na Ureno
iliendelea na kazi. Matokeo yake, mwaka
1954, Uingereza na Ureno zilitengua mkataba wao wa mwaka 1891 ulioweka mpaka wa
Ziwa Nyasa katika ufukwe wa mashariki ya Ziwa, yaani kwenye ufukwe wa Msumbiji,
na kuuhamishia katikati ya ziwa.
Ndugu Wananchi;
Jambo la kustaajabisha ni kuwa,
Waingereza walioona umuhimu na busara ya kurekebisha mpaka kati ya Malawi na
Msumbiji, hawakuona umuhimu wa kufanya hivyo kati ya nchi yetu na Malawi. Inashangaza, kwa sababu wakati huo Uingereza
ilikuwa mtawala wa nchi zetu mbili hivyo kazi ya marekebisho ingekuwa rahisi,
lakini hawakufanya hivyo. Na, baya zaidi
ni kuwa hata pale watu wa nchi yetu walipotaka
kupatiwa ufafanuzi na kutaka ukweli uwekwe wazi kuhusu mpaka hawakusikilizwa. Watu walitaka ufafanuzi kwa sababu
inasemekana kati ya mwaka 1925 na 1938, taarifa ya Uingereza kwa Umoja wa Mataifa
ziliweka mpaka katikati ya ziwa. Lakini,
kuanzia mwaka 1948 mpaka ukawekwa tena ufukweni.
Ndugu Wananchi;
Mwaka 1959, 1960 na 1962, suala la
mpaka wa Malawi lilijitokeza tena na kujadiliwa na Bunge la Tanganyika, wakati
ule lilijulikana kuwa Baraza la Kutunga Sheria, (Legislative Council – LEGCO). Hoja ya Wabunge wa Tanganyika ilikuwa kwamba mpaka
kuwekwa kwenye ufukwe wetu kunawanyima wananchi wa Tanganyika wanaoishi kando
kando ya ziwa haki yao ya msingi ya kutumia maji kwa kunywa, kuoga, kuvua samaki
na kupata manufaa mengine yatokanayo na ziwa bila ya kuomba ridhaa ya Serikali
ya Koloni la Nyasaland kama Malawi ilivyokuwa inajulikana wakati ule. Hoja iliyotolewa ilikuwa kwamba Serikali ya
Tanganyika ijadiliane na Serikali ya Nyasaland kupitia Serikali ya Malkia wa
Uingereza ili ufumbuzi upatikane. Wakoloni
hawakujali na wala hakuna hatua zilizochukuliwa mpaka Tanganyika ikapata uhuru
wake tarehe 9 Desemba, 1961 na Malawi kupata uhuru wake mwaka 1964.
Juhudi
za Kubadili Mpaka wa Ziwa Nyasa Baada ya Uhuru
Ndugu
Wananchi;
Wakati
tulipopata Uhuru mwaka 1961, mjadala kuhusu mpaka wa Tanganyika na Malawi
uliendelea Bungeni, ambapo ilitolewa hoja kwamba zifanyike juhudi za makusudi
za kuanzisha na kuendeleza mazungumzo ya kurekebisha mpaka huo kwa manufaa ya
wananchi wote wanaoishi pembezoni mwa ziwa.
Iliamuliwa kwamba tusubiri mpaka wenzetu wa Malawi wapate uhuru ili yafanyike
mazungumzo baina ya nchi mbili huru.
Kulijengeka matumaini kuwa mambo yangekuwa rahisi. Bahati mbaya haikuwa hivyo na kwamba mambo
yakageuka na kuwa magumu na ya uhasama. Miaka
mitatu baada ya Malawi kupata Uhuru wake (1964), kunako tarehe 3 Januari 1967,
Serikali ya Tanzania iliandika barua kwa Serikali ya Malawi kuelezea tatizo la mpaka
wa ziwani na kupendekeza nchi zetu mbili zizungumze na kulitafutia
ufumbuzi.
Ndugu Wananchi;
Bahati nzuri tarehe 24 Januari,
1967, Serikali ya Malawi ikajibu kukiri kupokea barua hiyo na kuahidi kuwa itatoa
majibu baada ya muda si mrefu. Hata
hivyo, tarehe 27 Juni, 1967, Rais Kamuzu Banda akilihutubia Bunge la Malawi, alikataa
maombi ya Tanzania. Alisema hayana
msingi na alidai kuwa kihistoria Songea, Mbeya na Njombe ni sehemu ya
Malawi. Hivyo basi, mazungumzo yakafa.
Tanzania haikukata tamaa. Alipochaguliwa Rais wa Pili wa Malawi, Mheshimiwa
Bakili Muluzi, juhudi zilifanyika lakini nazo hazikufika mbali. Bahati nzuri
tarehe 9 Juni, 2005, Rais wa Tatu wa Malawi, Mheshimiwa Bingu Wa Mutharika,
ambaye sasa ni marehemu, alimuandikia barua aliyekuwa Rais wa nchi yetu wakati
ule, Mheshimiwa Benjamin William Mkapa, kushauri nchi zetu zifanye mazungumzo
kuhusu mpaka wa ziwani. Alipendekeza iundwe
Tume ya Pamoja itakayojumuisha Mawaziri na Wataalamu kutoka nchi zetu
mbili. Tume hiyo itatoa mapendekezo kwa
Marais wa nchi zetu mbili ambayo yatakuwa msingi wa majadiliano baina yao. Alisisitiza umuhimu wa kulipatia ufumbuzi
suala hilo.
Ndugu Wananchi;
Kwa kuwa ilikuwa kipindi cha
mpito kuelekea kuchaguliwa Serikali ya Awamu ya Nne, Rais Benjamin Mkapa
hakuwahi kuishughulikia barua hiyo. Nilipoletewa barua hiyo nikaijibu kukubali
ushauri na mapendekezo yake. Aidha, nilipendekeza
Wizara na Idara zipi za Serikali zetu zishirikishwe katika Tume hiyo. Bahati nzuri Rais wa Malawi alikubali
mapendekezo yangu pamoja na lile la kwamba Malawi waitishe mkutano wa kwanza wa
Tume hiyo.
Ndugu Wananchi;
Mpaka sasa mikutano mitatu ya Tume
ya Pamoja imeshafanyika, wa kwanza ulifanyika tarehe 8 – 10 Septemba,
2010. Mkutano wa pili ukafanyika tarehe
27 – 28 Julai, 2012 hapa Dar es Salaam na wa tatu ukafanyika Mzuzu na Lilongwe
tarehe 20 – 27 Agosti, 2012. Hatua kadhaa zimepigwa lakini bado muafaka
haujapatikana kwa maana ya madai yetu ya kutaka mpaka uwe katikati ya ziwa na
madai yao kuwa mpaka ubaki ufukweni kwetu kama ilivyo kwenye Mkataba wa Heligoland wa Julai
1, 1890. Hoja ya wenzetu ni kuwa huo
ndiyo mpaka tuliorithi wakati wa uhuru.
Wanataka tuthibitishe hivyo na kwamba tuzingatie kauli ya OAU ya
kuheshimu mipaka tuliyorithi kwa wakoloni. Wananukuu kauli ya Baba wa Taifa,
Mwalimu Julius Nyerere akisisitiza hoja hiyo katika mkutano wa OAU mwaka
1963.
Hoja
za Msingi za Kutaka Mpaka Uwe Katikati ya Ziwa
Ndugu
Wananchi;
Kwa upande wetu tumekuwa na hoja
kadhaa za kutaka mpaka uwe katikati ya ziwa.
Ya msingi kabisa ni ukweli kwamba Mkataba wa Heligoland umekosewa kwa
kuamua kuwanyima wananchi wa Tanzania wanaoishi ufukweni mwa ziwa haki yao ya
msingi ya kutumia maji na rasilimali zilizomo katika Ziwa Nyasa. Zipo sababu kadhaa kwa upande wetu kudai
hivyo. Mojawapo ni sheria ya kimataifa inayoelekeza
kwamba po pote kwenye maji ya asili kama vile ziwa na mito iliyopo kati ya nchi
mbili mpaka huwa katikati. Ndiyo
utaratibu unaotumika duniani kote, na mifano iko tele. Kwa nini iwe tofauti katika ziwa Nyasa na kwa
upande wa Tanzania tu wakati kwa upande wa Msumbiji mpaka upo katikati ya ziwa?
Ndugu Wananchi;
Kwa upande wa Mto Songwe, mpaka
baina ya nchi zetu mbili upo katikati. Iweje
hapa kanuni hiyo itambulike na kuheshimiwa lakini isiwe hivyo ziwani? Kama nilivyoeleza awali, mwanzoni Mto Songwe wote
ulikuwa umewekwa upande wetu, lakini Tume ya Mipaka iliyoundwa mwaka 1898
ilifanya marekebisho na kuweka mpaka katikati ya mto. Kama nilivyokwishagusia kwenye ziwa hilo hilo
la Nyasa kwa upande wa Msumbiji mwaka 1954 mkataba wa mwaka 1891 ulioipa Malawi
ziwa lote ulirekebishwa na mpaka kuwekwa katikati. Kwa nini isifanyike hivyo hivyo kwa upande wa
Tanzania? Hivi hasa ni kipi ambacho
wenzetu wa Msumbiji walichotuzidi na kustahili kupata haki yao ya msingi ya kumiliki
na kutumia maji ya Ziwa Nyasa ambacho sisi Tanzania tumepungukiwa?
Ndugu Wananchi;
Maji ni zawadi ya Mwenyezi Mungu
kwa wanadamu wake, waitumie kwa uhai na maendeleo yao. Iweje leo, kwa watu wanaoishi pembeni mwa
ziwa hilo hilo wengine wapewe na wengine wanyimwe haki ya kulimiliki na kulitumia?
Kwa nini wanyimwe haki ya kunufaika na zawadi hiyo? Hivi kauli ya wakoloni
waliokaa Berlin ya kusema fulani apate na fulani asipate inatosha? Hivi kweli ni rahisi kiasi hicho?
Mpaka wa kwenye maji ni tofauti
na ule wa nchi kavu. Huu una rasilimali
ambayo huwezi kuamua kumnyima mwanadamu mwingine anayeishi pembeni yake kwa
vile haina badala yake. Unapowaambia
watu wa Mbamba Bay, Liuli, Lituhi, Manda, Ngonga, Matema, Mwaya, Itungi na
wengineo waishio kando ya ziwa kuwa maji hayo si yao bali ni mali ya Malawi
hawakuelewi na watakushangaa sana.
Watadhani umechanganyikiwa kwani tangu waumbwe wamekuwepo hapo
wanamiliki na kutumia maji ya Ziwa. Unataka
wafanyeje? Waende Malawi kuomba kibali
cha kuyatumia? Wao watakuuliza swali
moja tu “hivi hao wenzao wanaoishi ng’ambo ya pili wamewazidi nini katika
ubinadamu wao hata wapewe maji yote na wao wanyimwe?”
Ndugu Wananchi;
Kwa maana halisi ya Mkataba wa
Heligoland tangu tarehe 1 Julai, 1890, wananchi wa upande wa Tanzania wamekuwa
wanakunywa, kuoga, kuvua samaki na kusafiri katika maji ya Ziwa yasiyokuwa yao
bali ya nchi nyingine. Na kwa kuwa wamekuwa
wanafanya hivyo bila ya kupata kibali cha Malawi wamekuwa wanaiba maji na
samaki wa Malawi na kusafiri isivyo halali katika nchi ya watu. Jambo hili haliingii akilini hata kidogo. Ndiyo maana tunadai haki yetu stahili.
Ndugu Wananchi;
Na hiyo pia, ndiyo maana, busara na hekima ya Sheria ya Kimataifa kuhusu
mpaka wa kwenye maji kuwa
katikati. Sheria hii inazingatia hali
halisi ya maisha ya jamii inayozunguka ziwa ambayo imekuwa inalitegemea maisha
yao yote kwa shughuli zao za kuwapatia uhai na maendeleo yao. Haiwezekani kuwatenganisha watu waishio kando
ya Ziwa Nyasa kumiliki na kutumia maji hayo na rasilimali zake. Hawataelewa wala kukubali kuambiwa kuwa wanatumia
maji na rasilimali za ziwani kwa hisani
ya nchi ya Malawi.
Kwa watu waliokuwepo tangu Mungu anawaumba
wao na wenzao wa ng’ambo ya pili, siyo sawa na siyo haki hata kidogo kuwafanyia
hivyo. Kwe kweli ni unyanyasaji wa hali
ya juu. Ndiyo maana wazee wetu walidai
suala hili liwekwe sawa wakati wa ukoloni, kabla na baada ya Uhuru. Na ndiyo maana na sisi tunafuata nyayo zao
katika madai haya ya haki.
Ndugu Wananchi;
Kuna mambo mengine mawili ambayo yanatufanya
tudai haki ya kumiliki na kutumia Ziwa Nyasa.
La kwanza ni ule ukweli kwamba mito mingi ya Tanzania nayo inachangia
kujaza maji katika ziwa. Iweje leo maji yanayojaza
ziwa ni jambo jema, lakini yakishaingia ziwani, ziwa hilo si mali yao wenye
mito hiyo tena na wakiyatumia wanaiba mali ya watu wengine. Hivi kweli
ndivyo wanavyostahili kufanyiwa watu wanaotunza vyanzo vya mito hiyo na kuruhusu
maji yake kutiririka na kuingia ziwani?
Ndugu Wananchi;
Jambo la pili ni kwamba mpaka wa
Tanzania na Malawi kuwa ufukweni kunafanya ukubwa wa nchi zetu kuwa haujulikani
kwa uhakika. Unategemea mabadiliko kutokana
na kujaa na kupungua kwa maji
ziwani. Kunafanya mpaka wa nchi kuwa
hautabiriki na unaweza kuwa tatizo siku moja mbele ya safari. Isitoshe kuwa na nchi isiyojulikana ukubwa
wake nalo ni tatizo la aina yake. Ndiyo
maana mpaka kuwa katikati ya ziwa ni bora zaidi.
Ndugu Wananchi;
Kama nilivyokwishasema, chimbuko
la mzozo huu ni mkataba wa Heligoland ambao umepanda mbegu ya fitina baina ya
nchi zetu. Bahati mbaya sana Tume ya
Mipaka haikumaliza kazi ya kuhakiki mipaka yote ya nchi yetu na majirani zake kufuatia
kuzuka kwa Vita Kuu ya Kwanza mwaka 1914.
Ujerumani ikashindwa vita na koloni lake kuwa sehemu ya himaya ya
Uingereza. Bahati mbaya kwetu Waingereza
waliotawala nchi zetu mbili tangu 1918 hawakuchukua hatua za kurekebisha mpaka
kabla ya uhuru wa nchi zetu. Ni maoni yetu
kuwa nchi zetu sasa zifanye kile ambacho hakikufanywa na Tume ya Mipaka ya wakoloni
– Waingereza na Wajerumani. Tukifanye
sisi wenyewe kama nchi mbili huru kwa njia ya mazungumzo.
Bahati mbaya majaribio ya mwaka
1967 hayakufanikiwa. Bahati nzuri
kufuatia uamuzi wa kijasiri wa marehemu Rais Bingu wa Mutharika nchi zetu sasa zinazungumza. Bado hatujafikia muafaka kuhusu kurekebisha
mpaka na huenda ikatuwia vigumu kufikia muafaka. Jambo linaloleta faraja, hata hivyo, ni kuwa
sote wawili tumekubaliana kuwa tutafute mtu wa kutusuluhisha.
Ndugu Wananchi;
Hayo ndiyo matokeo ya mazungumzo
ya Tume yetu ya pamoja tangu ngazi ya Wataalamu, Makatibu Wakuu mpaka kwa
Mawaziri, katika vikao vya Mzuzu na Lilongwe kati ya tarehe 20 – 27 Agosti,
2012. Katika mkutano wao wa tarehe 27
Agosti, 2012 Mawaziri husika wa nchi zetu chini ya uongozi wa pamoja wa Waziri
wa Mambo ya Nje wa Malawi, Mheshimiwa Ephraim Chiume na mwenzake wa Tanzania,
Mheshimiwa Bernard Membe, wameafiki mapendekezo hayo. Aidha, wamekubaliana kuwa pande zote mbili
wakutane tena Dar es Salaam kati ya tarehe 10 – 15 Septemba, 2012 kukubaliana
juu ya usuluhishi wa aina gani unafaa.
Ndugu Wananchi;
Mtakubaliana nami kuwa tumepiga hatua muhimu
kuelekea kwenye kupata ufumbuzi wa kudumu wa suala hili. Hata hivyo, bado safari ni ndefu na huenda
ikawa na magumu mengi. Maombi yangu kwa viongozi
na wananchi wa Tanzania na Malawi ni kuendelea kuunga mkono jitihada hizi. Tuwaunge mkono wataalamu na Mawaziri wetu ili
wafanikishe vizuri jukumu lao.
Tuzingatie na kuheshimu walichokubaliana Lilongwe kuwa viongozi na
wananchi wa nchi zetu wajiepushe na kutoa kauli au kufanya vitendo vinavyoweza kuchafua
hali ya hewa, kuleta uchochezi na kuathiri majadiliano yanayoendelea.
Nawasihi Watanzania wenzangu kuzingatia
ushauri na rai hiyo ya Mawaziri na wataalamu wetu, ili kuwe na mazingira mazuri
ya mazungumzo na kuwezesha mzozo huu kuisha kwa amani na kirafiki.
Hitimisho
Ndugu Wananchi;
Kabla ya kumaliza hotuba yangu, napenda
kusisitiza kuwa si makusudio yangu wala ya Serikali yetu kutafuta suluhisho la
suala hili kwa nguvu ya kijeshi. Nawahakikishia
Watanzania wenzangu kuwa hatuko vitani na Malawi na wala hakuna maandalizi ya vita
dhidi ya jirani zetu hawa kwa sababu ya mzozo wetu wa mpaka katika Ziwa. Ondoeni hofu na endeleeni na shughuli zenu za
ujenzi wa taifa letu kama kawaida.
Nilimhakikishia hivyo Rais wa
Malawi, Mheshimiwa Joyce Banda nilipokutana naye Maputo, Msumbiji tarehe 18
Agosti, 2012. Tanzania haina mpango wa
kuingia vitani na Malawi. Mimi na
wenzangu Serikalini tunaona kuwa fursa tuliyoitafuta miaka mingi ya kukaa na
ndugu zetu Malawi kuzungumzia suala hili lenye maslahi kwetu sote sasa
tumeipata. Hatuna budi kuitumia
ipasavyo. Naamini, tukifanya hivyo,
inaweza kutufikisha pale tunapopataka. Ni muhimu, kwa ajili hiyo kwa pande zetu
mbili, kuipa fursa ya mazungumzo nafasi ya kuendelea bila ya vikwazo
visivyokuwa vya lazima.
Ndugu Wananchi;
Kwa
sababu hiyo basi , napenda kutumia nafasi hii kuwasihi ndugu zetu wa vyombo vya
habari na wanasiasa wenzangu tuepuke kauli au matendo yatakayovuruga mazungumzo
na kuchochea uhasama kati ya nchi zetu mbili jirani na rafiki. Kuna manufaa makubwa ya kumaliza mzozo wetu
kwa njia ya mazungumzo kuliko kwa njia ya vita.
Kufikiria sasa kutumia njia nyinginezo hasa za nguvu za kujeshi, si
wakati wake muafaka. Aidha, tukitumia
njia ya vita, badala ya kuwa tumepata suluhisho inaweza kuwa ndiyo mwanzo wa
mgogoro mpana zaidi. Tuendelee kuwaunga
mkono wawakilishi wetu katika Tume yetu ya pamoja. Naahidi, Serikali itakuwa inawapa taarifa
kadri mazungumzo yetu na wenzetu wa Malawi yatakavyokuwa yanaendelea. Nina hakika tutamaliza salama.
Mungu
Ibariki Tanzania!
Mungu
Ibariki Afrika!
Asanteni
kwa Kunisikiliza
No comments:
Post a Comment