Banner

Banner

FOLLOW US FACEBOOK

propertyfinder.co.tz

Tuesday, September 11, 2012

Jeshi la Polisi sasa lipewe mwelekeo mpya ...!

IMEKUWA kawaida sasa kuona habari nyingi zinazochapishwa au kutangazwa na vyombo vya habari kuhusu Jeshi la Polisi nchini, kwa kiasi kikubwa zimekuwa hazionyeshi taswira nzuri kuhusu jeshi hilo. Hali hiyo siyo tu imethibitishwa  na matukio ya kila siku hapa nchini, bali pia na tafiti na tathmini mbalimbali ambazo zimekuwa zikifanywa kila mwaka na taasisi kadhaa zinazoheshimika za hapa nchini na nchi za nje. Tafiti na tathmini hizo zimeonyesha, kwa mfano kwamba jeshi hilo, mbali na Mahakama linaongoza kwa vitendo vya rushwa.
 
Nyingi ya taasisi hizo za kitafiti, ikiwamo Transparency International ya Marekani zimesema, tofauti na taasisi nyingine zilizokubuhu katika vitendo vya rushwa kama ilivyo Mahakama, jeshi hilo pia hutumia mabavu, mateso na vitisho katika kudai rushwa. Na kama hiyo haitoshi, pia taasisi kadhaa za haki za binadamu, ikiwamo Amnesty International ya Uingereza zimefanya tafiti na kutoa ripoti za kila mwaka zinazoonyesha  kwamba jeshi hilo ni mkiukaji mkubwa wa haki za binadamu.
 
Hiyo ndiyo taswira halisi ya jeshi hilo katika nchi yetu. Hivyo, vyombo vya habari vinaporipoti  habari zenye kuonyesha taswira hasi ya jeshi hilo, havifanyi hivyo kwa lengo la kulipaka matope, isipokuwa kuwajulisha wananchi kuhusu mwenendo wake usiofuata maadili na weledi, ili wazishinikize mamlaka husika zifanye mabadiliko stahiki kwa kulisafisha jeshi hilo katika ngazi zote za uongozi. Ni jambo la ajabu kuona Jeshi lililokuwa la mfano barani Afrika baada ya Uhuru wa nchi yetu, kwa maana ya kuwalinda wananchi na mali zao na kuwa kimbilio la wanyonge, linageuka kuwa adui mkubwa wa wananchi kwa kuwatisha, kuwatesa, kuwaua, kuuza haki zao na kuwadai rushwa.
 
Hata vyombo vya habari vingejitahidi kiasi gani kuisafisha, kuiremba na kuipodoa sura ya jeshi hilo katika hali lililomo sasa hakika isingewezekana, kwani sura hiyo imechafuka kiasi cha kutosafishika na kutorembeka tena. Habari za askari polisi kufanya mauaji ya raia wasiokuwa na hatia, au kushiriki katika mitandao ya wizi, uporaji na ujambazi, au kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya, usafirishaji wa binadamu, utapeli na uhalifu mwingine wa kutisha ndizo habari zinazotoka katika jeshi hilo kwa wingi.
  
Hatuoni jinsi jeshi hilo la polisi linavyoweza kuendelea kufanya kazi katika hali na mazingira hasi lililomo hivi sasa kutokana na kupoteza sifa ya kuwa Jeshi la Polisi. Kama wananchi wamefikia hatua ya kupaza sauti zao kwa pamoja na kusema jeshi hilo ni adui yao namba moja, inawezekana kweli askari wake wakavaa sare za jeshi hilo na kutembea kifua mbele kama walinzi wa raia na mali zao? Hivi wanajisikiaje sasa wanapopita  mitaani na kusikia raia wakiguna na kuwabeza tofauti na zamani walipokuwa kimbilio lao?
 
Hoja tunayoijenga hapa ni kwamba jeshi hilo limeacha njia lililotumwa na waasisi wake kuifuata. Jeshi hilo limechafuka na linanuka, hivyo tunadhani njia pekee iliyobaki ni kulibomoa na kulisuka upya kwa kuwafukuza na kuwastaafisha wale wote waliolifikisha hapa lilipo. Kwa kuzingatia ukweli kwamba siyo askari wote waliomo katika jeshi hilo ni wala rushwa, wezi, majambazi au wauaji, ingefaa ufanyike mchakato wa kura za maoni na za siri jeshi humo ili askari waovu watambuliwe kwa majina.
 
Zoezi hilo linaweza kuendeshwa na tume huru itakayoteuliwa na Rais au Bunge. Hata hivyo, yafaa tutambue kwamba kupitisha fagio la chuma pekee hakutoshi kama Serikali haitawaengua askari vihiyo, ili vijana wasomi na wenye uadilifu, ambao wamejaa mitaani bila ajira  wachukue nafasi zao. Tunahitaji jeshi jipya la polisi lenye uadilifu na lililo rafiki wa raia, linalotambua na kuheshimu haki za msingi za kiraia na ambalo mikono ya askari wake haina harufu ya damu ya wananchi waliouawa bila hatia.

Chanzo: Mwananchi

No comments:

Post a Comment