TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa
Jakaya Mrisho Kikwete amemwambia Mwenyekiti wa Taasisi ya Mapinduzi ya Kijani
katika Afrika (AGRA), Mheshimiwa Kofi Annan kuwa Afrika haiwezi kuzungumza ama
kupata maendeleo ya maana bila kumshirikisha mkulima mdogo.
Aidha, Rais Kikwete amemwambia Mheshimiwa Annan,
Katibu Mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa (UN) kuwa bila mkulima mdogo wa
Afrika kusaidiwa hawezi kutoka kwenye umasikini kwa sababu anakabiliwa na
changamoto nyingi ambazo peke yake hawezi kupambana nazo.
“Huwezi kuzungumzia maendeleo ya aina yoyote katika
Afrika bila kumshirikisha mkulima mdogo. Huwezi kufanikiwa kwa kumtenga mkulima
mdogo. Kwa bahati mbaya sana, mkulima mdogo katika Afrika amebakia anatumia
zana zile zile za jadi, jembe la mkono, pekee yake hawezi kupiga hatua bila
kusaidiwa kwa sababu anakabiliwa na changamoto nyingi mno,” amesema Rais Kikwete.
Rais Kikwete ameyasema hayo usiku wa jana, Jumatano,
Septemba 26, 2012, kwenye Hoteli ya Ngurdoto, Arusha wakati alipokutana na
kufanya mazungumzo na Mheshimiwa Annan.
Viongozi hao wamefikia kwenye Hoteli ya Ngurdoto
ambako wamewasili jana kuhudhuria Mkutano wa Pili wa AGRA ambao umeanza jana
kwenye hoteli hiyo. Rais Kikwete amewasili jioni ya jana tayari kuufungua rasmi
mkutano huo.
Huu ni mkutano wa pili wa AGRA baada ya wa kwanza
uliofanyika Ghana miaka miwili iliyopita. Agenda kuu ya AGRA ni kujaribu kuleta
mageuzi ya kilimo katika Afrika.
Katika mkutano kati ya viongozi hao, Rais Kikwete
amemwambia Mheshimiwa Annan kwamba kwa sababu kilimo kinaajiri watu wengi
nchini na kwa sababu kinakua kwa kasi ndogo sana, kwa asilimia nne tu, bado
kinamvuta chini kila mmoja nchini.
“Uchumi wetu unakua kwa kasi ya kuridhisha sana na
hasa katika sekta za mawasiliano, miundombinu, madini na utalii, lakini bado
mafanikio hayo hayajaanza kuonekana kwa wazi kwa wananchi kwa sababu kilimo
ambacho kinaajiri Watanzania wengi zaidi kinakua kwa kasi ndogo. Kasi hii
inamvuta kila mmoja kurudi chini.”
Mheshimiwa Annan amemsifu Rais Kikwete kwa uongozi
shupavu katika eneo la kilimo kutokana na program mbali mbali ambazo Serikali
imezianzisha. “Nakupongeza sana Mheshimiwa Rais kwa uongozi. Umekuwa mfano wa kuigwa
katika Bara letu kwa uongozi wako katika eneo hili la kilimo”.
Imetolewa
na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.
27 Septemba,
2012
No comments:
Post a Comment