Banner

Banner

FOLLOW US FACEBOOK

propertyfinder.co.tz

Thursday, October 11, 2012

Mramba: serikali haikupata hasara kuingia mkataba na Kampuni ya Alex Stewart

Aliyekuwa Waziri wa Fedha, Basil Mramba
Aliyekuwa Waziri wa Fedha, Basil Mramba, ameiambia Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa, hakuna hasara yoyote iliyopatikana kutokana na mkataba ulioingiwa kati ya serikali na Kampuni ya Alex Stewart Government Business Assayers na badala yake mkataba huo ulikuwa na faida kubwa kwa serikali.

Mramba ambaye alikuwa  waziri katika kipindi cha awamu ya tatu, aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam wakati akijitetea mbele ya Jopo la Majaji wawili na Hakimu linaloongozwa na Jaji John Utamwa linalosikiliza kesi inayomkabili na wenzake wawili ya matumizi mabaya ya madaraka wakiwa watumishi wa umma na kuisababishia hasara serikali ya Sh. bilioni 11.52.

Akiongozwa na wakili wake Peter Swai, Mramba aliiambia mahakama hiyo kuwa pamoja na faida zingine, kampuni hiyo iliweza kufundisha na kuwapatia utaalamu Watanzania 30 wa jinsi ya kukagua migodi kifedha na kitaalamu.

Sehemu ya mahojiano kati ya Mramba na wakili wake yalikuwa kama ifuatavyo:

Swali: Umesema Government Notice (GN) zilitoka kwa utaratibu na mkataba ukaanza kufanya kazi inavyotakiwa, lakini hapa una shitaka la kuisababishia serikali hasara ya Sh.bilioni  11.52 unasemaje kuhusiana na hilo?

Jibu: Si kweli kuwa kulikuwepo na hasara wala fedha iliyopotea, kama ushahidi wa mashahidi wawili wa upande wa mashtaka ulivyoeleza kwamba hakukuwa na hasara kwa sababu mkataba ulifuata sheria, taratibu na kanuni zilizokuwepo ambapo.

Walisema fedha hizo ni ‘tax forgone’ yaani kodi ambayo haikuwepo. Unaposamehe kodi huwezi ukasema tena kuna hasara kutokana na kodi uliyoisamehe.

Swali: Hakukuwa na hasara, je kulikuwa na faida?

Jibu: Faida iliyopatikana siyo faida ya kifedha (profit and loss) bali faida kwenye uchumi na siasa za nchi.

Swali: Unaweza ukatupatia mojawapo ya faida ya wazi iliyopatikana kwenye uchumi wa nchi.

Jibu: Waheshimiwa, mbali na mshauri huyo kufundisha Watanzania hao 30 kwa mara ya kwanza katika historia ya Tanzania, serikali imewatumia watanzania hao  kuanzisha Wakala wa Ukaguzi wa Migodi nchini. Na kwa ukaguzi wao serikali imeweza kujibu hoja za wabunge na wananchi wengi kwamba migodi ilikuwa inailalamikia serikali.

Faida nyingine aliyoitaja Mramba ya mkataba huo, ni ile ya serikali kupata mtambo mkubwa wa kisasa kuliko yote nchini wa kupima dhahabu iliyoachwa na mshauri huyo, baada ya kuondoka nchini.

Kesi hiyo iliahirishwa hadi leo ambapo Mramba ataendelea kujitetetea.

 Mbali na Mramba wengine wanaoshitakiwa katia kesi hiyo ni pamja na waziri wa zamani wa Nishati na Madini, Daniel Yona na aliyekuwa Katibu Mkuu wa wizara ya fedha, Grey Mgonja.

Katika hatua nyingine Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jana iliahirisha kesi inayomkabili Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Usafiri Dar es salaam (UDA), Iddi Simba, na wenzake wanaoshitakiwa kwa kula njama, kughushi, kuchepusha fedha na kusababisha hasara ya Sh. bilioni 2.4.

Hakimu Mfawidhi wa mahakama hiyo, Ilvin Mgeta,  aliahirishwa kesi hiyo hadi Novemba 9 mwaka huu, kufuatia ombi la upande wa mashtaka lililosababishwa na kutokamilika kwa taratibu za kuendelea na kesi hiyo.

Wakati huo huo  Mbunge wa Jimbo la Bahi (CCM), Omary Badwel anayekabiriwa na makosa ya rushwa ya shilingi milioni moja toka kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga imeahirishwa hadi Oktoba 29 mwaka huu.

Kesi hiyo imeahirishwa kufuatia hakimu, Faisal Kahamba aliyekuwa akiisikiliza kuhamishiwa katika mkoa wa Mara.

No comments:

Post a Comment