Banner

Banner

FOLLOW US FACEBOOK

propertyfinder.co.tz

Monday, October 15, 2012

NAIBU WAZIRI AMCHOMA KIONGOZI KWA TAKUKURU...!

Naibu Waziri wa Uchukuzi, Charles Tizeba amemkabidhi mikononi mwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Mthamini wa makazi ya wahanga wa ujenzi wa bandari mpya ya Mwambani ya jijini Tanga kwa kuisababishia serikali hasara ya sh. milioni 800.
Tizeba alitoa amri hiyo mbele ya ofisa wa Taasisi hiyo aliyeambatana na msafara wake wa  kukagua eneo lililoandaliwa kwa ajili ya ujenzi wa bandari ya kisasa.
Hali ya hewa ilianza kubadilika pale mthamini wa makazi, Gregory Mwapule kueleza kuwa kuna nyongeza ya sh. milioni 800 za fidia kwa wakazi hao tofauti na sh. bilioni 1.7 zilizolipwa awali na serikali.
Katika hali ya kubabaika mthamini huyo alimueleza Naibu Waziri kuwa majengo ambayo hayakufanyiwa uthamini awali hayakufahamika wamiliki wake na mengine yalijengwa baada ya zoezi hilo kukamilika na kwamba alilazimika kufanya marudio ya uthamini kwa mara nyingine.
Baada ya taarifa hiyo, Naibu Waziri alipata hofu na kutaka maelezo kamili kuhusiana na ongezeko hilo na kudai kuwa haimuingii akilini kwamba mthamini huyo aliacha majengo ambayo wamiliki wake hawakutambulika kwa bahati mbaya ama kwa mujibu wa muongozo wa kazi yake.
Akipingana na taarifa hiyo, Tizeba alitaka kuonyeshwa majengo hayo mapya hata hivyo hayakuwepo na badala yake yalionekana maboma ya zamani tofauti na maelezo ya mthamini huyo.
“Hili si boma jipya ni la zamani iweje liwe ni ongezeko…unajua mimi sitaki mambo ya ubabaishaji, nieleze hizi milioni 800 umezipata wapi...kwani hili jengo halikufanyiwa uthamini awali!? Alihoji Tizeba alipoonyeshwa moja ya boma linalodaiwa kuwa ni ongezeko la uthamini wa awali.
“Wewe bwana acha wizi…huu ni ufisadi, sitaki kuamini kuwa wewe hujui wajibu wako,  lakini hainiingii akilini madai yako ya kutothaminisha  jengo eti mmiliki hajulikani!…hivi wewe unathaminisha mali au watu?…kwanini usingethaminisha majengo yote na baadae kutambua wamiliki?” alihoji Tizeba.
Kutokana na mkanganyiko huo, Tizeba aliitaka taasisi ya Takukuru kuondoka naye kwa ajili ya kumchunguza yeye pamoja na mtandao wake aliyoshirikiana nao katika kutenda hujuma hizo za kuitia serikali hasara ya sh. milioni 800.
“Takukuru hebu ondokeni na huyu mtu,…fanyeni uchunguzi kwa kuibia serikali, na taarifa yake naitaka kabla ya kuanza Bunge, sawa!? alisema Tizeba huku akimkabidhi Mwapule mikononi mwa Takukuru.
Aidha Mwapule alipoulizwa kuhusiana na tuhuma hizo alidai kuwa yeye ni safi na wala hana hofu na hilo kwa kuwa kilichofanyika ni kwa mujibu wa taratibu za utekelezaji wa majukumu yake.
“Aaa!, unajua mimi sibabaiki, kama ni kusimamishwa ama kuchunguzwa si mageni kwangu  yalishanifika kwa Waziri Magufuri” alisema huku akionyesha kukerwa na kauli ya Naibu Waziri.

CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment