Waziri Mkuu, Mizengo Pinda
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, ameziagiza wizara zote kuwawezesha wanawake na wasichana kwa usalama wa kesho katika kuchangia kuleta maendeleo endelevu ili kupunguza athari za maafa.
Alisema hayo jana katika taarifa yake kwa vyombo vya habari kuelezea maadhimishi ya siku ya Kimataifa ya Upunguzaji wa Athari za Maafa (International Day for Disaster Reduction) inayoadhimishwa Oktoba 13, mwaka huu.
Alisema kuna umuhimu wa kuwawezesha wanawake na wasichana hususani katika suala la utunzaji wa mazingira na usimamizi wa mali asili, utawala na mipango ya matumizi ya ardhi na miji pamoja mipango ya kiuchumi na kijamii ambayo ndiyo mihimili ya kinga ya maafa.
Pinda alisema wanawake na wasichana Tanzania ni asilimia 51 ambao ni miongoni mwa waathirika wa maafa ambapo asilimia 60 wanasaidia katika uzalishaji wa chakula vijijini hivyo uzoefu, ujuzi na uelewa wao ni muhimu sana katika mikakati na shughuli za upunguzaji wa athari za maafa na kuhimili mabadiliko ya tabia nchi.
Pinda alisema mchango ya wanawake na wasichana utakuwa na matokeo mazuri iwapo watashirikishwa katika hatua zote za menejimenti ya maafa.
Aliongeza kuwa itambulike kuwa uwiano sawa wa jinsia unaanzishwa na elimu wanawake na watoto hivyo ni lazima washiriki katika kufahamu jinsi ya kujiandaa, kukabili na kupunguza athari za maafa katika jamii.
Pinda alisema Serikali imekuwa ikichukua hatua kadhaa kuwezesha ushiriki wa wanawake katika masuala mbalimbali ya kimaendeleo ikiwa ni pamoja na shughuli za upunguzaji athari za maafa katika ngazi za kisiasa na kutoa maamuzi kwa kuwapa fursa ya moja kwa moja katika kusimamia Ofisi za Umma zikiwamo Wizara, Taasisi na Idara za serikali.
No comments:
Post a Comment