ASEMA CCM YA SASA HAIWATISHI
SIKU moja baada ya Mwenyekiti wa Taifa wa CCM, Rais Jakaya Kikwete,
kuwataka makada wa chama hicho kujibu mapigo ya wapinzani, akidai
wanafanya kazi ya kueneza uongo na kupotosha wananchi, CHADEMA imesema
inamvutia pumzi kabla ya kumjibu.

Akihitimisha mkutano mkuu wa CCM mjini Dodoma juzi usiku, Rais Kikwete
aliwataka mawaziri na makada wa chama hicho kufanya mikutano ya hadhara
na kutumia vyombo vya habari kujibu hoja za wapinzani badala ya
kutegemea nguvu za Jeshi la Polisi.
Huku akionekana kukasirishwa na kasi ya CHADEMA, Rais Kikwete alimtaja
wazi wazi Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk. Willibrod Slaa, kuwa aliwahi
kumzulia uongo pamoja na mwanaye Ridhiwani.
“Slaa aliita mkutano akasema mimi, mwanangu Ridhiwani na Rostam Aziz
tulikutana kwenye hoteli moja jijini Mwanza, huku akijua siku aliyoitaja
mi nilikuwa kusini nikiendelea na shughuli zangu,” alisema.
Rais Kikwete alisisitiza kuwa hiyo ndiyo kazi ya upinzani, watu wazima
hovyo, wanasema uongo mbele wananchi na hata wakati mwingine kwenye
vyombo vya habari wakinukuu takwimu za uzushi.
Alipoulizwa jana na gazeti hili kuhusu madai hayo ya kueneza uongo kwa
wananchi, Dk. Slaa alicheka kisha akasema: “Tunawatafakari na
tutawajibu, ila siyo leo, wala hatuna haraka.
“Mimi kwa kweli sikusikiliza hotuba yake, na hata mkutano wa CCM
sijaufuatilia, ila kama Kikwete kasema hayo unayoniuliza, basi tutamjibu
kwa utaratibu rasmi wa chama, leo sisemi kitu.
“Sisi ni watu makini, tunaamini katika kile tunachokisema wala
wasipaniki, tutawajibu. Maana wanadhani tunapoteza muda kufuatilia
mkutano wao, nilimsikia hata Nape Nnauye akisema juzi kuwa anajua
tumeacha kazi tunawakodolea macho,” alisema.
Dk. Slaa alisema kauli ya Nape ambaye pia ni Katibu wa Halmashauri Kuu
(NEC), Itikadi na Uenezi wa CCM, inachekesha, kwani CCM ya wao kuacha
kazi zao na kuikodolea macho ilikuwa ya zamani si hii ya leo.
Katika kile kinachoonekana kama CHADEMA kuinyima usingizi serikali na
CCM, Kikwete aliagiza mawaziri wote kujiwekea utaratibu wa kila mmoja
kutoa taarifa za utekelezaji wa majukumu ya serikali katika vyombo vyote
vya habari.
Alisema kwa vile viongozi wa chama na serikali hawajibu taarifa za
upotoshaji zinazotolewa na wapinzani, wananchi wanapozisikia zikirudiwa
rudiwa bila kukanushwa wanaziamini.
Chanzo Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment