Banner

Banner

FOLLOW US FACEBOOK

propertyfinder.co.tz

Wednesday, December 12, 2012

AJALI MBAYA YASABABISHA VIFO VYA WAALIMU WATANO NA WANNE KUJERUHIWA ...!

Robert Boaz

WALIMU watano wa Shule ya Sekondari Scolastika katika mji mdogo wa Himo wilayani Moshi Vijijini, Mkoa wa Kilimanjaro, wamekufa na wengine wanne kujeruhiwa vibaya baada ya gari walilokuwa wakisafiria kupata ajali.

Ajali hiyo ilitokea juzi wakati walimu hao wakiwa katika gari walilokodi aina ya Toyota Hiace lenye namba za usajili T771 AQD. Gari hilo liligongana na lori aina ya Scania, mali ya Kampuni ya Vinywaji Baridi ya Bonite Bottlers yenye namba za usajili T212 AHH na tela namba T653. Akielezea ajali hiyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Robert Boaz alisema ilitokea juzi saa 8:30 usiku katika daraja la Mto Kikavu Kata ya Machame wilayani Hai mkoani Kilimanjaro. Boaz alisema walimu hao wakiwa katika gari hilo, likiendeshwa na Alexander Mocha mali ya shule hiyo, walikuwa wakitokea mkoani Arusha kwenye maziko kurejea mjini Moshi. Aliwataja waliopoteza maisha katika ajali hiyo, kuwa ni walimu Julius Kimaro, mkazi wa Rombo mkoani Kilimanjaro, Bernard Omukunyu, Ernest Ambani ambaye pia ni mwangalizi wa wanafunzi wa kiume na Nelly Sasaka, ambaye ni mwangalizi wa wanafunzi wa kike, wote ni raia wa Kenya, na Joseph Opolochi ambaye ni raia wa Uganda. Kamanda Boaz alisema walimu watatu walikufa papo hapo. Wengine walipoteza maisha wakati wakipatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya KMC mara baada ya kufikishwa. Kwa mujibu wa Kamanda Boaz, majeruhi wanne wa ajali hiyo, ambao pia ni walimu wa shule hiyo, wamelazwa katika hospitali hiyo na hali zao si nzuri. Kwa mujibu wa taarifa kutoka eneo la tukio, chanzo cha ajali hiyo kimedaiwa ni dereva wa lori kuendesha gari lake katikati ya barabara na walipokaribiana na Hiace iliyowabeba walimu hao, alirudi upande wake, lakini tela lilibaki katikati na kusababisha ajali hiyo. Mkuu wa Shule ya Sekondari Scolastica, Scolastika Shayo, alisema walimu hao walitoka kwenye maziko ya mwanafunzi wa kidato cha tatu katika shule hiyo, Jackson Kelvin, aliyekufa baada ya kugongwa na gari akiwa likizo. Alisema waliojeruhiwa wengine ni Msaidizi wa Mkuu wa Shule, Peter Mlay. Aliwataja wengine kwa jina moja kuwa ni, Mwalimu Dismas, Mwalimu Nelson na Mocha, ambaye ni dereva wa gari la shule hiyo.

No comments:

Post a Comment