Banner

Banner

FOLLOW US FACEBOOK

propertyfinder.co.tz

Tuesday, April 23, 2013

KESI YA LWAKATARE YAFIKIA PAZURI...!

JESHI la Polisi Nchini limetoa taarifa ya kukamilika kwa uchunguzi dhidi ya tuhuma za kuhusika na vitendo vya kigaidi zinazowakabili Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Wilfred Lwakatare na Ludovick Joseph. Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Kaimu Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Nchini, Issaya Mngulu, alisema upelelezi wa kesi hiyo umekamilika na jalada linaandaliwa kwenda kwa Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) kwa hatua zaidi. Lwakatare anakabiliwa na kosa la kupanga njama za kigaidi, kama kuteka na kutesa watu mbalimbali. Hadi sasa bado anashikiliwa na polisi, huku mahakama ikizuia kupewa dhamana.


Alisema kwa upande wa kesi ya kumwagiwa tindikali Kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Musa Tesha, katika uchaguzi mdogo wa ubunge Jimbo la Igunga, mkoani Tabora Septemba 2011, tayari watuhumiwa wawili wameshafikishwa mahakamani.

Alisema upelelezi dhidi ya tuhuma hizo upo katika hatua za mwisho, endapo watabainika watuhumiwa wengine nao watafikishwa mahakamani.Alieleza kuwa kuhusiana na kesi ya kuvamiwa, kupigwa na kujeruhiwa kwa Mhariri Mtendaji wa New Habari (2006) Ltd, Absalom Kibanda, tukio la kutekwa na kujeruhiwa kwa Dk Steven Ulimboka, matukio yaliyotokea huko Zanzibar pamoja na matukio mengine mengi yaliyoripotiwa katika vituo vya polisi hapa nchini, uchunguzi bado unaendelea.

“Uchunguzi wa matukio kama haya upo katika hatua mbalimbali za kiupelelezi, ambazo kwa sasa si vema kuziweka wazi kuepusha kuharibu upelelezi unaoendelea.

“Aidha, tunawashukuru wananchi kwa ushirikiano wao mkubwa unaosaidia kufanikisha upelelezi wa matukio ya uhalifu na hatimaye kufanikisha kukamatwa kwa wahalifu hapa nchini, hivyo naomba wananchi waendelee na ushirikiano huo ili nchi yetu iendelee kuwa na usalama.

“Vilevile Jeshi la Polisi linaomba kuufahamisha umma na waandishi wa habari kwa ujumla kwamba zipo sheria na taratibu za kutoa habari za matukio yanayoripotiwa katika vituo vya polisi.

“Ieleweke wazi kwamba taarifa zinazoripotiwa vituoni kwa mujibu wa sheria ni za siri kwa faida ya wahanga wa kesi na kwa ajili ya kufanikisha upelelezi wa kesi yenyewe.

“Aidha kannuni za jeshi zinamruhusu Kamanda kutoa taarifa za tukio na siyo kujadili ushahidi wa kesi ili kuepusha kuathiri mwenendo mzima wa kesi ziwapo mahakamani,” alisema DCP Mngulu.

habari na ASIFIWE GEORGE NA RUTH MNKENI, DAR ES SALAAM chanzo - mtanzania

No comments:

Post a Comment