Banner

Banner

FOLLOW US FACEBOOK

propertyfinder.co.tz

Tuesday, April 23, 2013

NIMEMWAMBUKIZA MWANANGU UKIMWI KUTOKANA NA UMASIKINI WANGU...!

Ukimsikiliza Zaituni Ally (35) anayeishi na virusi vya ukimwi (VVU) kwa miaka saba sasa, machozi yanaweza kukutiririka mashavuni.

“Nakula mlo mmoja kwa siku siku nyingine nalala na njaa,”alisema Zaituni.


Siyo hivyo tu. Zaituni ana watoto watatu wenye umri wa miaka 9, 5 na miezi mitatu. Alimzaa mtoto wake wa kwanza, ambaye hivi sasa yuko Mtwara kwa dada yake, akiwa hana maambukizi lakini alijifungua mtoto wa pili na watatu akiwa ameshagunduliwa kuwa na VVU.


Hivi sasa mtoto wake wa pili naye anatumia dawa za ARV. Amegunduliwa kwamba ana VVU, japokuwa alipozaliwa alikuwa hana.


Zaituni anasema alipewa maelekezo ya namna ya kumtunza mtoto wake kila alipokwenda kliniki.


“Nilifurahi sana kuambiwa mtoto wangu hana maambukizi alipozaliwa. Niliambiwa nimlee vyema ila cha msingi nilitakiwa kumtengea vifaa vyake vya kutumia kama wembe na sindano,” alisema Zaituni

Ni vigumu kujua lini mtoto huyu alipata maambukizi lakini hali yake iligundulika baada ya kufikisha miaka minne.

Na japokuwa ni vigumu kujua namna alivyoambukizwa, maisha ya Zaituni yanatoa ushahidi wa aina Fulani. Hana mume kwa sababu baba ya watoto wake wapili wa kwanza alimuacha baada ya kugundua mama na mtoto wana VVU.


“Umasikini wa kipato ndio umechangia kumuambukiza mtoto wangu virusi vya ukimwi,” alisema Zaituni, huku akibubujikwa na machozi shavuni.


Afisa habari kutoka tume ya kudhibiti ukimwi nchini (TACAIDS) Glory Mziray anasema kuwa, tatizo la Zaituni kukosa chakula na watu wengine wenye tatizo kama lake, wanatoapesa katika kila halmashauri zote nchini ili, kuwawezesha kufanya muitikio wa kudhibiti ukimwi kwa kuwashirikisha watu wanaoishi na virusi vya ukimwi.

Mziray alisema kuwa wilaya inatakiwa kupanga na kujua kuna waathirika kiasi gani na kuwapatia mahitaji mbalimbali wanayowahitaji, kwa mfano chakula, mavazi,elimu kwa jamii juu ya kujikinga na virusi vya ukimwi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto.

“Haki za watu wanaoishi na virusi vya ukimwi na ukimwi vinajumuishwa na kulindwa katika kila sekta, pia kuna mkakati na sera kwa watu wanaoishi na virusi vya ukimwi wa mwaka 2008 hadi 2012, ili kuweza kuratibu watu hao katika kila sekta, maana watu wanaoishi na virusi vya ukimwi wako katika kila sekta hapa nchini, pamoja na kuunda baraza la watu wanaishi na virusi vya ukimwi ili waweze kujadili haki zao na kuzitatua,” alisema Mziray

Mziray alisema kuwa kila mwaka wanatumia Bilioni 15.5 pesa za kuthibiti ukimwei, pia pesa hizo zinapelekewa katika kila halmashauri kulingana na mahitaji hali ya halmashauri husika, lengo kubwa ni kuhakikisha kuwa wanapambana na maambukizi mapya na kuwapatia mahitaji ya muhimu kwa watu wenye virusi vya ukimwi, hata nchi nyingine kama Kenya, Uganda,Rwanda nao wanawapatia pesa halmashauri husika kudhibiti ukimwi kama tunavyofanya hapa nchini.

Katika Kitabu cha pili cha mkakati wa taifa wa kudhibiti ukimwi cha mwaka 2008 hadi 2012 kinaeleza kuwa, kuhakikisha uwianishaji kwa ukamilif wa changamoto zinazohusu janga la ukimwi katika sera na mipango mikuu ya maendeleo ya muda mrefu, kwa kuzingatia athari mahususi kwa watu wanaishi na virusi vya ukimwi na ukimwi, familia zao zilizoathirika pamoja na masuala yanayohusu jinsia na umasikini.

“Ningekuwa na pesa ya kununua wembe, sindano, chanuo na sabuni mtoto wangu asingepata maambukizi. Lakini hata pesa ya kununua unga na mboga ni tatizo kwangu; nitawezaje kupata pesa ya kununua vifaa mmbalimbali vya kutumia mtoto pekee yake? Kikubwa ninachoangalia ni watoto kupata chakula.”

Akikosa kabisa chakula, Zaituni analazimika kutumia dawa zake za ARVs hivyo hivyo na kumuombea mtoto wake chakula kwa majirani ili asiregee na dawa anazotumia.

Mtoto wa pili wa Zaituni hajui kwa nini anapewa dawa kila siku. Anasema mama yake anampatia dawa asubuhi na jioni; muda mwengine akisahau, inabidi amkumbushe

Mtoto huyo alisema kuwa mama yake alimwambia akinywa dawa hiyo ndio anakua haraka. Pia, aliongeza kwa kusema kuwa anaamini akifikia umri wa kuanza shule akuwa na akili nyingi shuleni kutokana na dawa hizo.

Maamuzi ya kumpeleka wake wa kwanza kwa dada yake yalimsaidia mtoto huyo kutopata maambukizi ya virusi vya ukimwi, mwaka 2006 alianza kliniki na kupimwa akakutwa na maambukizi ya virusi vya ukimwi. Kwa wakati huu, Zaituni bado hajui kama mtoto wake watatu ana maambukizi ya VVU; amemleta katika hospitali ya wilaya ya Nachingwea kupima.

“Sina hakika kama naye atakuwa vema bila ya kupata maambukizi, maana huyu kaka yake amezaliwa mpaka anamaliza kunyonya hakupata maambukizi, alipofika miaka minne aligundulika na maambukizi ya virusi vya ukimwi,” alisema Zaituni.


Kwa mujibu wa Kaimu Mratibu wa ukimwi wilaya ya Nachingwea Dokta Khadija Komba zaidi ya watoto 458 wameambukizwa virusi vya ukimwi, pengine katika mazingira ya kuchangia nyembe, chanuo na sindano za kutolea funza na mzazi au na mzazi mwenye virusi kwa kugusuna kama ana mchubuko mwilini.

Watoto 458 waliozaliwa na mama wenye VVU, mpaka wanafikisha miezi 18 walikuwa hawana maambukizi ya virusi vya ukimwi, inawezekana wamepata maambukizi ya virusi vya ukimwi kwa kutumia vitu vya ncha kali pamoja na mama zao kwa kipindi cha miaka mitatu.

Jumla ya watoto 200 wanatumia dawa za ARVs, kati ya hao watoto wa kiume 90 na watoto wa kike 110, pia watoto 258 bado hawajaanza kutumia dawa za ARVs, kati ya hao watoto wa kiume 118 na watoto wa kike 140, kwa sababu kinga za mwili kuwa juu. Kama mtoto kinga yake ya mwili iko chini anapatiwa dawa kuanzia umri wa mwezi mmoja hadi miaka 14.

Dokta Komba alisema kuwa watoto kuanzia mwezi mmoja hadi miaka 14 wanapewa dawa aina ya AZT 390, niverapin na seprin mpaka wanapoacha kunyonya, dawa hii wanayopewa inasaidia kudumaza wadudu wa virusi vya ukimwi wasizaliene kwa wingi kwa mtoto.

Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii Dokta Hussein Mwinyi, alisema kuwa mwaka 2011 jumla ya vituo 1,660 vinavyotoa huduma za (PMTCT) vilianza kutoa huduma za utambuzi kwa kutumia sampuli kwenye hospitali za rufaa.

Idadi ya watoto waliopatiwa huduma hiyo imefikia 18,231 kwa mwaka 2009 na watoto 22,033 kwa mwaka 2010 na 27, 245 kwa mwaka 2011. Kwa sasa tumefikia asilimia 26 ya kupunguza maambukizi ya virusi vya ukimwi lengo ifikapo 2015 ifikie asilia 4 ya maambukizi.

Kwa upande wake Muuguzi Mkunga anayewapima watoto wakiwa chini ya miezi 18 Evarist Chingwuile, alisema kuwa mtoto anapozaliwa na mama mwenye maambukizi ya virusi vya ukimwi anapewa dawa za AZT390 na niverapin kwa muda wa miezi 18.

Chingwuile alisema kuwa akiwa na miezi miwili anapimwa antijen katika sehemu ya unyayo kujua kama anamaambukizi au hana maambukizi, wakishamtoa damu inapelekwa katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili.

Majibu yanarudi baada ya wiki mbili, wakati wote huo mtoto anaendelea na dawa, mtoto akiachishwa kunyonya, anapimwa kumuangalia kama anamaambikizi, kama anamaambukizi anapimwa na kinga ya mwili kama iko chini anaendelea kupewa dawa ya niverpin na seprin na kumuamishi katika kituo cha ctc.

Dokta Debora Kayoka meneja wa mradi wa kumkinga mtoto asipate maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto nchini, alisema mashine za kumpima damu ya mtoto ili kujua kama ana maambikizi au hana kwa hapa nchini, mashine hizo zipo katika hospitali za rufaa tu, kama hospitali ya Mbeya, hospitali ya Bugando, hospitali ya Kcmc na hospital ya Muhimbili.

Mashine ya (DNA-PCR) ambazo zinatumika kujua kama damu ya mtoto inamaambukizi mashine hizi zinauzwa kwa gharama ya dola ya Kimarekani 35,000 hadi dola 45,000, serikali ya Tanzania imepewa ufadhili na mfuko wa Bill Cliton Fundation.

Kwa sasa nchini Tanzania tunawataalamu wa kupima damu ya mtoto wa umri wa miezi miwili kwa kutumia mashine hii ya DNA-PCR wako wangapi 22 na wamesomea kozi za maabara Kwa muda wa miaka miaka 3, kwa kiwango cha degree,mashine hizo kwa hapa nchini zipo 10.

Chingwuile alisema kuwa kwa mwaka 2012 wanawake wajawazito waliofika kliniki kupima waliku 1,614 kati hao wasiona maambukizi ni 1565, wenye (VVU) 49, wanaume walipima na wake zao wakati wa ujauzito ni 26.

Wanaendelea na dawa ambao wana watoto wa changa ni 14. Pia mimba za utotoni 86 na wajawazito 14 wanatumia dawa hizo za kumkinga mtoto asipate na maambukizi.

Watoto wote waliozaliwa na wamama wenye virusi vya ukimwi hawana maambukizi ila mama anapojifungua salama tunamuuelekeza jinsi ya kumtunza mtoto asimuambikize virusi.

“Tunamuelimisha mama kutotumia nyembe, sabuni, sindano na chanuo pamoja na mtoto wake, anatakiwa kutunze vizuri mtoto wake kwa kumuandalia vifaa mbalimbali vya kwake kama wembe, sindano, sabuni na chanuo ili asimuambukize (VVU),” alisema Chingwuile.

Alisema kuwa baada ya miaka miwili au mitatu mama anapokuja kliniki mtoto anaanza kuumwa homa za mara kwa mara, ukimpima unamkuta mtoto amemuambukiza virusi vya ukimwi wakati alipojifungua unamuelimisha jinsi ya kumtunza mtoto ana anapokuja kliniki kila mwezi.

“Wengi husema hali ngumu ya maisha wanashindwa kununua wembe wa peke yake na mtoto akinunua wembe anatumia na mtoto wake kama kumkata kucha kumtoa funza na kumyoa nywele na kumpa vyakula akiwa chini ya miezi sita pia kunasababisha kumuambukiza virusi vya ukimwi,” alisema Mkunga Chingwuile.

Kwa upande wake mkurugenzi wa wilaya ya Nachingwea Mwanamvua Mrindoko alisema kuwa, kila mwaka wa fedha Tume ya kuthibiti ukimwi nchini wanawapatia shilingi milioni 80 kwa ajili ya mapambano ya virusi vya ukimwi laki kwa mwaka huu wa fedha mpaka sasa wamepokea shilingi milioni 20 tu bado shilingi milioni 60.

Mrindoko alisema kuwa pesa hizo wakizipata wanazitumia kwa, Kuwajengea uwezo kamati mbalimbali za ukimwi za kata. Kwa sasa wilaya ina kamati 32, pia wanawalipia ada ya shule wanafunzi waliotoka katika familia zilizoathika na ukimwi na wanafunzi wanaishi na virusi vya ukimwi na ukimwi ambao wako 438 wa shule za sekondari.

Aidha alisema kuwa zaidi ya milioni 20 inatumika kuwalipia ada wanafunzi hao wenye maambukizi ya ukimwi na ukimwi katika shule mbalimbali kuanzia kidato cha kwanza mpaka chuo kikuu.

Pia wanatoa lishe kwa wanafunzi wapata 15 wa shule ya sekondari na wanafunzi 20 wa shule ya msingi, vile vile wanatoa lishe kwa wagonjwa wenye ukimwi ambao hawajiwezi majumbani, kuwezeshwa katika miradi mbalimbali kama kutunza mazingira, kutengeneza lishe na vikoba.

Mrindoko alisema kuwa idadi kubwa ya watoto wanafunzi wanaishi na virusi vya ukimwi na wenye ukimwi katika wilaya hiyo, imetokea mwaka 1990 hadi 1998 kwa sababu kulikuwa bado hakuna dawa ya kumkinga mtoto asipate maambukizi ya virusi vya ukimwi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto. Kwa sasa zaidi ya watu wenye 4,625 kati ya wakazi 17,00,000.

“Changamoto kubwa sana wanayoipata ni pesa kuwa finyu ukilinganisha na idadi kubwa ya maambukizi mpya ya ukimwi siku hadi siku katika msimu wa korosho na ufuta, pia uwepo wa machimbo ya madini Kiegei pamoja na makambi makubwa matatu ya kijeshi kuwepo katika wilaya hiyo na inasemekana wanajeshi hao wanafanya ngono zembe katika wilaya hiyo,”alisema Mrindoko

Kufuatia ufinyu wa bajeti na kuchelewa kufika muda muafaka, waathirika wengi hasa vijiji ambako kuna kata 26 za wilaya hiyo wanakosa huduma muhimu kama lishe na kujiunga katika vikundi vya uzalishaji mali ili waweze kujitegemea wenyewe katika kupata chakula, wanaiomba tume ya kuthibiti ukimwi nchi kuwaongea bajeti ya wilaya ya Nachingwea kutoka shilingi milioni 80 hadi ifike shilingi milioni 100.

Kwa mujibu wa kitabu kilichochapishwa kwa hisani ya Amref na Watu wa Marekani mwezi Julai mwaka 2007 na kusainiwa na Katibu Mkuu Mukama, ambacho kinaelezea muongozo kwa mama mwenye maambukizi ya virusi vya ukimwi kulimsha mtoto asiye na maambukizi , kunaweza kumuambukiza virusi hivyo.

Kitabu hicho kinaeleza kuwa mwanamke anayeishi na (VVU), anaweza kumuambukiza mtoto wake akiwa na ujauzito,uchungu na wakati wa kujifungua na wakati wa kunyonyesha.

Kama mama mjamzito hajapima (VVU), hawezi kufahamu kama anaishi na VVU. Hivyo ni muhimu wanamke mjamzito na wanaonyonyesha kupima ili kutambua hali yao ya maambukizi ya (VVU) na kupata ushauri wa jinsi ya kuwakinga watoto wao na maambukizi ya (VVU).

Mama anaishi na(VVU), damu na maziwa yake huwa na (VVU). VVU kutoka kwa mama vinaweza kwenda kwa mtoto wakati wa mimba, hususan wakati wa uchungu na kujifungua, wakati mtoto anapogusana na damu au majimaji ya mwili wa mama yeke. Ikiwa mama ananyonyesha (VVU) kwenye maziwa yake vinaweza kupita kwa mtoto.

Dokta Hussein Mwinyi alitoa ufafanuzi katika siku ya ukimwi duniani iliyofanyika katika Mkoa wa Lindi, hali halisi ya maambukizi kwa wanawake wajawazito hapa nchini kwa waka 2011, 86,875 walipatiwa dawa za ARVs kuzuiya maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto.

Sawa na asilimia 71 ya wajawazito 122,146 waliokadiriwa kuwa na maambukizi ya virusi vya ukimwi, asilimia ya wajawazito kuwa na maambukizi ya virusi vya ukimwi imeongezeka mpaka kufikia asilimia 62 ukilinganisha na mwaka 2005 kulikuwa na asilimia 9 ya wajawazito wapatao 11,435 waliopatiwa huduma hii.

Kaimu Mganga mkuu wa Wilaya dokta John Sijaona alisema kuwa, tatizo la watoto wa chini ya miaka 15 kupata maambukizi linatokana na elimu duni kwa wanawake wanaoishi na virusi vya ukimwi pamoja na ugumu wa maisha mama anashindwa kutenga vifaa mbalimbali vya kutumia mtoto wake na kusababisha kumuambukiza virusi vya ukimwi.

“Mama akipewa elimu ya kutosha jinsi ya kumtunza mtoto aliyemzaa asimuambukize virusi vya ukimwi itasaidia kupunguza maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto, lakini ugumu wa maisha nao unachangia mama kushindwa kumudu kununua nyembe, chanuo na sindano kwa mtoto pekee,” alisema Dokta Sijaona

Makala ya kisayansi iliyofanywa na dokta Kahabi Isangura mwaka 2007-2008 ambaye pia ni mtaalamu wa afya ya jamii inasema kuwa, kiwango cha maambukizi kwa wanawake ni asilimia 21.5 na wanaume kiwango cha maambukizi ni asilimia 11.4.

Makala hiyo ya kisayansi inaeleza kuwa kati ya watoto 70,000 hadi 80,000 wanaozaliwa kila mwaka wapo hatarini kuambukizwa virusi vya ukimwi (VVU) kipindi cha kuzaliwa na wakati wa kunyonya.

Kipindi cha mwaka 2007-2008 zaidi ya watu milioni 1,400,000 wanaishi na virusi vya ukimwi, kati hao wanawake ni asilimia 52 na asilimia 11. 4 ni watoto wa chini ya umri wa miaka 15.

Aidha makala hiyo inaeleza kuwa kwa sasa Tanzania inakadiliwa kuwa na watu milioni 2, 113,158 wanaishi na virusi vya ukimwi lakini kati ya hao asilimia 21. 5 ndio wanaopatiwa dawa za kupunguza makali ya ugonjwa huo.


Chanzo: kalulunga

No comments:

Post a Comment