Banner

Banner

FOLLOW US FACEBOOK

propertyfinder.co.tz

Thursday, May 30, 2013

Mishahara Kima cha chini sekta binafsi juu..!

Serikali imetangaza nyongeza mpya ya mishahara ya kima cha chini kwa sekta binafsi nchini, ambayo itaanza kutumika Julai mwaka huu. Vile vile, serikali imetangaza kutengeneza ajira mpya 600, 000 kwa vijana nchini kupitia programu ya ajira kwa vijana katika mwaka ujao wa fedha. Hayo yalitangazwa bungeni jana mjini Dodoma na Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudence Kabaka, wakati akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara yake kwa mwaka wa fedha 2013/2014. Waziri Kabaka alisema nyongeza hiyo mpya pia itakuwa katika sekta binafsi nne mpya zilizoainishwa hivi karibuni ambazo ni Ujenzi, Shule Binafsi, Nishati na Mawasiliano. 

Alisema wizara imekamilisha utafiti wa majadiliano ya kima cha chini cha mshahara katika sekta binafsi 12 na kwamba katika sekta zote 12 kima cha chini kimeongezeka.
Alitaja sekta hizo kuwa ni  Ujenzi, Shule Binafsi, Nishati, Viwanda na Biashara, Hoteli na Huduma Majumbani.
Nyingine ni, Ulinzi Binafsi, Afya, Madini, Uvuvi na Huduma za Majini, Usafirishaji na Mawasiliano na Kilimo.
Waziri Kabaka alisema kima cha chini katika sekta zote 12 kimeongezeka kwa kiwango tofauti tofauti, huku Viwanda na Biashara kikiongezeka kwa asilimia 43.8, Hoteli na Huduma za Majumbani (asilimia 55.2), Ulinzi Binafsi (asilimia 46.4), Madini (asilimia 25), Afya (asilimia 65), Uvuni na Huduma za Majini (asilimia 21.2), Usafirishaji (asilimia 49) na Kilimo (asilimia 42.9).
 Kuhusu ajira 600, 000, Waziri huyo alisema utekelezaji wa programu hiyo utafanyika katika kipindi cha mwaka wa fedha wa 2013/2014-2015/16.
Aidha, alisema serikali katika mwaka wa fedha wa 2013/2014 inatarajia kuwezesha kupatikana kwa fursa za ajira zaidi ya 300,000 na kwamba ajira hizo ni mbali ya ajira 61, 915 za watumishi wa umma watakao ajiriwa na serikali.
Alisema serikali imewabaini waajiiri ambao hawalipi wafanyakazi wao mishahara ya kima cha chini cha serikali, kutowapa mikataba ya kazi na kuwafanyisha kazi kwa saa nyingi bila malipo ya ziada.
Alisema baadhi ya waajiri hawatoi likizo ya uzazi, lakini serikali imeshawachukulia hatua za kisheria ikiwamo wizara kutoa amri elekezi kwa waajiri 118 na kuwafikisha mahakamani waajiri 33.
Alisema wizara imehakiki mikataba ya ajira ipatayo 56,000, kati ya hiyo mikataba 19,247 ni madereva wa malori yanayosafirisha bidhaa nje ya nchi.
Waziri Kabaka alisema mpango huo utaanza kutekelezwa baada ya kukamilika kwa taratibu na maandalizi ya utekelezaji wake kwa lengo la kuufanya kuwa bora na endelevu.
Alisema wizara yake kwa kushirikiana na taasisi za hifadhi ya jamii nchini zimefanya utafiti na tathmini ya tatizo la malipo ya fao la kujitoa katika Mifuko ya Hifadhi ya Jamii kwa wafanyakazi watakaopoteza ajira kabla ya umri wa kustaafu.
Alisema mapendekezo ya namna ya kushughulikia suala hilo yameandaliwa na yatajadiliwa na wadau kabla ya kuwasilishwa bungeni katika mwaka ujao wa fedha.
AJIRA MPYA ZA SERIKALI, SEKTA BINAFSI
Waziri Kabaka alisema katika mwaka 2012/13 jumla ya ajira 274,030 zilipatikana na kati ya hizo, ajira 56,746 zilitolewa na serikali, ajira 8,603 zilitangazwa na sekta binafsi kupitia vyombo vya habari na ajira 208,681 zilitokana na utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
VIBALI VYA AJIRA KWA WAGENI.
Kabaka alisema katika kipindi hiki wizara ilipokea na kushughulikia jumla ya maombi 6,424 ya vibali vya ajira za wageni vya daraja B na imefanya ukaguzi katika kampuni 148 kwa lengo la kuhakiki vibali vya ajira.
Alisema rasimu ya muswada wa vibali vya ajira kwa wageni utawasilishwa bungeni katika mwaka ujao wa fedha na kwamba lengo lake ni kuwa na sheria moja ya kusimamia masuala ya vibali vya ajira za wageni, hivyo kuondoa utata na migogoro katika utaratibu unaotumika sasa.

CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment