LILIRUSHWA NA POLISI ALIPOSIMAMA
VITUKO na matukio ya hatari kwenye mikutano ya CHADEMA vimeendelea kushika kasi.
Jana Mbunge wa Ubungo, John Mnyika alinusurika kupigwa na bomu la
machozi lililorushwa na polisi waliokuwa wakizuia kufanyika mkutano
ulioitishwa na chama hicho.
Tukio hilo lilitokea katika eneo la Mabibo kwenye viwanja vya Sahara
ambapo bomu hilo lilimpata mtu aliyekuwa karibu na Mnyika anayeitwa
Thomas Jerome, aliyejeruhiwa sehemu ya paja.
Baada ya kurushwa kwa bomu hilo, polisi walitaka kumchukua majeruhi huyo
ili wamweke kwenye gari lao apelekwe hospitalini, lakini Mnyika
aliwaelekeza wafuasi wa CHADEMA kumchukua kwa madai kitendo
kilichofanywa na askari hao kililenga kuficha ushahidi wa jambo hilo.
Polisi waliokuwemo eneo la tukio waliamua kukubaliana na matakwa ya
wafuasi wa CHADEMA waliomchukua Jerome na kumpeleka hospitali ambako
hali yake inadaiwa inaendelea vizuri.
Akielezea hali ilivyokuwa akiwa katika mkutano mwingine uliofanyika
Ubungo, Mnyika alisema polisi walifika katika viwanja vya Sahara wakiwa
na magari matatu kwa lengo la kutawanya wafuasi wa CHADEMA wasifanye
mkutano wakidai haukuwa na baraka za jeshi hilo.
Mnyika alisema polisi hao walisema sababu ya kuuzuia mkutano huo ni
uwepo wa ziara ya Makamu wa Rais katika Wilaya ya Kinondoni, hivyo
walikuwa wameelekeza nguvu zao katika ziara hiyo, kwamba hawakuwa na
uwezo wa kuulinda mkutano wa CHADEMA.
“Nikiwa nimejiandaa kupanda jukwaani ndiyo polisi walikuja kusema tuache
tusifanye mkutano, nilisogea karibu na gari kumlalamikia ofisa wa
polisi kwani kitendo cha kuahirisha mkutano kwa barua waliyoileta saa
sita mchana siku ya mkutano wakati sisi tuliwapa taarifa siku nne
zilizopita ilikuwa sio haki.
“Nilimwambia ofisa huyo wa polisi kuwa nilikuwa najadiliana kwa simu na
viongozi wakuu wa Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam na
Inspekta Jenerali wa Polisi Said Mwema kumlaumu kutumika vibaya kwa
Jeshi la Polisi.
“Nilipokuwa bado najibizana naye bila fujo zozote, bomu lilirushwa
kutoka ndani ya gari ya polisi na kupita karibu na mimi likamjeruhi mtu
aliyekuwa karibu yangu, ki ukweli nimeshangazwa sana na matumizi mabaya
ya silaha za moto,” alisema.
Aliongeza kuwa katika purukushani zilizotokea baada ya bomu kupigwa,
alipoteza nyaraka mbalimbali alizokuwa amebeba kama ushahidi kuwaonyesha
wafuasi wa chama hicho hasa jinsi serikali ya CCM na wabunge wake
walivyopitisha kodi ya huduma za simu, na kodi ya laini za simu.
Slaa anena
Aidha katika mkutano huo ambao awali ulitangazwa kuwa ungehutubiwa na
Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk. Willibrod Slaa, haukuweza kuhutubiwa
naye kwa kile alichosema kuwa watu wake wa usalama walimwambia mapema
hali si salama kwenye mkutano huo.
“Nilipata taarifa kutoka vyanzo vyangu kuwa polisi walikuwa na mpango wa
kuleta fujo, hivyo nikaona kwa kuwa wanatuwinda nisingeenda kuhutubia,
pengine bomu lililomkosa Mnyika lilikusudiwa kwangu au kwa mwingine,”
alisema Dk. Slaa alipozungumza na gazeti hili kwa njia ya simu baada ya
kutoonekana mkutanoni.
Zuio la polisi
Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, jana liliahirisha mkutano huo wa CHADEMA kabla viongozi hao kupanda jukwaani.
Liliwapelekea barua ya zuio CHADEMA inayosomeka: “Kumbuka barua ya
tarehe 17 Julai, yenye kumb. CHADEMA/MKT/UBUN/015/2013 uliyomwandikia
Kamishna wa Polisi Kanda Maalumu Dar es Salaam. Kamishna wa Polisi Kanda
Maalumu ya Dar es Salaam amezuia kufanyika kwa mkutano huo tarehe 21
Julai 2013 katika viwanja vya Sahara, Mabibo kwa sababu siku mliyoomba
kufanya mkutano wenu wa hadhara, Wilaya ya Kinondoni ina mapokezi ya
ugeni wa ziara ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.”
Hata hivyo Mnyika alipinga sababu hiyo ya polisi kwa madai CHADEMA
wamepeleka taarifa kwa Jeshi la Polisi tangu Julai 17 kwamba wangefanya
mkutano katika viwanja hivyo Julai 21, lakini jeshi hilo halikuwajibu
hadi walipokuwa wanaenda mkutanoni.
CHADEMA wabadili mbinu
Kutokana na kuzuiwa kufanya mkutano kwenye viwanja vya Sahara, CHADEMA
waliamua kuufanyia Ubungo kutokana na kuomba vibali viwili kwenye maeneo
tofauti.
Baada ya kuzuiliwa Mabibo, kibali cha Ubungo kilikuwa halali, hivyo
Mbunge wa Ubungo aliyekuwa amefika Sahara kwa ajili ya kuhutubia,
aliandamana kwa miguu na wafuasi wa chama hicho hadi Ubungo, huku kukiwa
na makachero wengi wa polisi waliofuatilia maandamano hayo.
Akizungumza na wananchi katika mkutano uliofanyika Ubungo, Mnyika
alisema polisi walifanya kitendo cha kikatili, kusubiri watu wamalize
maandalizi, wakusanyike uwanjani ndipo wanaleta barua ya kupiga marufuku
mkutano kwa kisingizio kuwa katika Wilaya ya Kinondoni kulikuwa na
ziara ya makamu wa Rais katika Jimbo la Kawe na Kindondoni.
“Sisi tupo Ubungo, Makamu wa Rais yupo Kawe na Kinondoni, sasa suala la
kuzuia mikutano isifanyike lilikuwa na maana gani? Kama Jeshi la Polisi
walisema hawana askari wa kutosha kulinda mkutano wetu mbona katika
kuutawanya wamekuja na magari matatu?” alihoji.
Mnyika alitumia muda mwingi kulilaumu Jeshi la Polisi, kwanza kwa
kuahirisha mkutano muda mfupi kabla ya viongozi kupanda jukwaani, lakini
pia kitendo cha kurushwa bomu mahali ambapo hakukuwepo fujo zozote.
Madudu zaidi ya CCM
Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe ameendelea kuanika madudu ya Chama
Cha Mapinduzi (CCM), safari hii akitoa nyaraka za mikakati ya chama
hicho tawala kufundisha vijana kukabiliana na wapinzani.
Akihutubia mkutano wa hadhara juzi katika Viwanja vya Mahakama ya
Mwanzo, Nguzo Nane, mjini Shinyanga, Mbowe alisema kuwa ili kujilinda
dhidi ya vitendo alivyodai wanafanyiwa na vijana wa Green Guards -
kikosi cha vijana wa CCM, chama chao kitaendelea na mipango ya kuwapatia
vijana wao mafunzo ya ukakamavu.
Mbowe alionyesha nyaraka mbili za CCM zinazoonyesha kuwa chama hicho
tawala kupitia wanachama wa Jumuiya ya Vijana (UVCCM) kimekuwa kikitoa
mafunzo ya ukakamavu kwa vijana wake, huku nyaraka moja ikionyesha kuwa
moja ya malengo ya mafunzo hayo ni kukabiliana na upinzani.
“Tunashambuliwa, watu wetu wanapigwa, wanateswa, wanatekwa na wengine
kuuawa, kwa sababu tu wanataka mabadiliko na wanapenda CHADEMA, majuzi
mlisikia Waziri Mkuu Pinda anasema wamechoka...sasa tunasema Pinda kama
umechoka ondoka upishe ofisi ya umma hiyo, upishe kwenye ofisi ya watu
kama umechoka, maana kuchoka huko ni kuchoka kwa CCM. Pisheni ofisi sio
za kwenu hizo, ni za Watanzania.
“Wananchi hapa mkononi nimeshika nyaraka mbili za CCM, moja ni cheti cha
kuhitimu mafunzo na nyingine hapa juu imeandikwa ‘Sera za Msingi za
CCM’, sasa mi sitawasomea, naomba aje hapa jukwaani mtu yeyote anayejua
kusoma, awasomee mjue tunaposema CCM wamekuwa na kikundi
kinachoshambulia, kupiga, kutesa, kuteka na hata kuua Watanzania wenzao
eti tu kwa sababu wanaunga mkono CHADEMA, huwa tunamaanisha nini,”
alisema Mbowe.
Mmoja wa wananchi aliyehudhuria mkutano huo wa hadhara, ambao ulikuwa ni
sehemu ya shughuli za ukamilishaji wa kuzindua Kanda ya Ziwa Mashariki
(mikoa ya Shinyanga, Simiyu na Mara), alipewa kabrasha kubwa na kusoma
sehemu inayozungumzia majukumu ya jumuiya za chama hicho.
Gazeti hili pia lilifanikiwa kuona kabrasha hilo kwa karibu, ambapo kifungu cha 9.1 kinachozungumzia UVCCM, kinasomeka hivi;
“(i) Umoja wa vijana wa CCM unapaswa kuwajenga vijana katika itikadi,
ukakamavu na mafunzo yatakayowafanya wajiamini, wawe vijana wenye ari ya
kutimiza wajibu wao wakiwa walinzi wa chama, viongozi na wagombea wa
CCM.
“(i) Utaratibu wa kuandaa makambi ya vijana usimamiwe kwa dhati. Chama
kiwe na mipango mizuri ya kutafuta na kuwateua wakufunzi watakaofaa
kuwapatia vijana mwelekeo unaotakiwa ikiwa ni pamoja na elimu ya
uchaguzi/uraia. Mafunzo ya makambi ya vijana, mbali ya kujifunza nyimbo
za hamasa yatilie mkazo pia mafunzo ya ukakamavu kwa lengo la
kukabiliana na vitendo vya kihuni vya baadhi ya vijana wa vyama vya
upinzani.”
Mbowe pia aliwaonyesha wananchi waliofurika kwenye mkutano huo cheti cha
mmoja wa watu waliohitimu mafunzo ya makambi ya vijana wa CCM ambacho
kilionyesha mhusika alianza mafunzo Juni 27, 2009 na kumaliza Julai 4,
2009, mkoani Dodoma.
Cheti hicho kimesainiwa na watu wawili, mmoja mwenye jina la Jumanne
Kitundu, akiwa na nafasi ya Katibu wa UVCCM, Dodoma mjini na mwingine,
Robert Mwinje, Mwenyekiti wa jumuiya hiyo, Wilaya ya Dodoma mjini.
Cheti hicho kinaonyesha mhusika (jina linahifadhiwa) alihitimu mafunzo
ya masomo ya kanuni ya umoja wa vijana, wajibu wa vijana katika chama,
ulinzi na usalama, ujasiriamali, ukakamavu, wajibu wa vijana katika
uchaguzi, rushwa, ukimwi, historia ya TANU na ASP pamoja na maadili.
Msimamo wa CHADEMA
Mbowe alisitiza kuwa CHADEMA kitasimamia azimio la kikao cha Kamati Kuu
ya chama hicho juu ya kuimarisha kitengo chake cha ulinzi na usalama
ikiwemo kuanzisha makambi ya mafunzo ya ukakamavu kwa vijana wa chama
hicho watakaokuwa na jukumu la kulinda viongozi wao.
Ingawa msimamo huo umekuwa ukipingwa na wadau mbalimbali likiwemo Jeshi
la Polisi, Msajili wa Vyama vya Siasa na CCM, Mbowe amesisitiza kuwa
hawatarudi nyuma juu ya mpango huo utakaoimarisha ulinzi.
Kodi ya laini za simu
Hoja ya tozo ya simu imekuwa ajenda kubwa kwenye mikutano iliyofanywa na viongozi mbalimbali wa CHADEMA.
Mwenyekiti wa Baraza la Vijana wa CHADEMA (BAVICHA), John Heche alisema
kama wananchi wasingeipa ushirikiano CHADEMA na kupinga maovu
mbalimbali, CCM ingekuwa imeshauza nchi na wananchi wake.
Alisema tozo la laini za simu lilipitishwa wakati wabunge wa CHADEMA
walipokwenda Arusha kushiriki maombolezo na mazishi ya marehemu wa tukio
la bomu, hivyo serikali ikaona ipeleke jambo hilo lililobarikiwa na
wabunge wengi wa CCM.
“Maana yake ni nini? Kodi hii kwanza mwananchi maskini kabisa ambaye
amedunduliza na kununua simu, atakuwa analipa sawa sawa na matajiri
wakubwa, yaani wewe hapa utakuwa unalipa kodi sawa na Reginald
Mengi...lakini kama hiyo haitoshi, ukipiga mahesabu utakuwa unalipa kodi
takriban shilingi 12,000 kwa mwaka.
“Serikali hii ya CCM inayowaletea kodi ya sh 12,000 kwa mwaka ndiyo
ililazimika kuondoa na kufuta kodi ya kichwa, baada ya CHADEMA kuwa
imefanya hivyo kwenye halmashauri zake, kwa kuanza na Hai ambako
Mwenyekiti Mbowe alikuwa ni mbunge na Karatu kwa Dk. Slaa. Sasa walifuta
kodi ya manyanyaso ya kichwa kwa maelekezo ya CHADEMA iliyokuwa sh
3,000 kwa mwaka, ambapo watu walikuwa wanakimbia nyumba na kujificha
maporini, wengine wakaliwa na wanyama, sasa wanataka mlipe kimya kimya,
sh 12,000 kwa mwaka. Ni matokeo ya kushindwa kwa sera za CCM,” alisema
Heche.
Mkutano wa Geita
Wabunge wa CHADEMA wanaotoka Kanda ya Ziwa na viongozi wa chama hicho
nao waliendelea kufanya mikutano katika maeneo mbalimbali huku
wakilalamikia tozo la laini za simu pamoja na mapendezo ya rasimu ya
katiba mpya yaliyotolewa na CCM hivi karibuni yakipinga mambo mengi
yaliyopendezwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Jana, wabunge hao wa viongozi walifanya mikutano ya hadhara katika mji
wa Kasamwa huko Geita na Sengerema mkoani Mwanza ambako walisema CCM
imekosa sifa ya kuongoza ndiyo maana maisha ya Watanzania yamezidi kuwa
magumu kadiri siku zinavyokwenda mbele.
Wabunge hao pamoja na viongozi na makada wa CHADEMA ambao wapo kwenye
msafara wa kuimarisha chama katika kanda hiyo, ni pamoja na Ezekiel
Wenje (Mbunge wa Nyamagana), Profesa Kulikoyela Kahigi (Bukombe), Dk.
Anthony Mbasa (Biharamulo Magharibi) na Conchesta Rwamlaza (Viti Maalumu
– Kagera).
Viongozi na makada wengine ni pamoja na mjumbe wa Baraza Kanda ya Ziwa
Magharibi, Anwar Kashaga, katibu wa CHADEMA Manispaa ya Bukoba, Lenatus
Kilongozi pamoja na Mwenyekiti wa Wilaya ya Biharamulo Magharibi, George
Kasaiza.
Akizungumza kwenye mikutano hiyo, Wenje alisema CHADEMA inatarajia
kuunda mabaraza ya wananchi kuhusu muundo wa serikali tatu, na
wanatarajia kukusanya saini za Watanzania kupinga tozo ya kodi mpya ya
laini za simu iliyopitishwa hivi karibuni bungeni.
Alisema kwa sasa CCM wametoa mapendekezo ya kutaka kusiwepo uwazi wa
mikataba, maadili ya umma na haki za binadamu kwenye katiba mpya, na
inataka Spika wa Bunge lazima atokane na mbunge, jambo aliloliita ni
kuendeleza ukandamizaji kwa wananchi.
“Wakati CHADEMA tunataka spika na mawaziri wasitokane na wabunge, CCM
wao wamependekeza viongozi hao watokane na wabunge ili waendelee
kuwakandamiza Watanzania. CHADEMA tunataka nchi iwe na mawaziri saba tu,
na siyo 15 wa pendekezo la tume na 64 waliopo sasa.
“Si hilo tu, ibara ya 22 hadi 23 ya rasimu ya katiba mpya, CCM kwa
mapendekezo yao wanataka haki za binadamu zisiwepo kwenye katiba mpya
ijayo, bali ziwepo kwenye sheria tu. CCM haitaki kuwepo malengo ya taifa
kwenye katiba mpya!
“Tutakusanya saini milioni 10 za wananchi kuhusu mapendekezo ya katiba
mpya. Pia tutakusanya saini milioni tano za wananchi kutaka tozo ya
laini za simu ifutwe,” alisema Wenje huku akisisitiza uundwaji wa
serikali tatu; Tanganyika, Zanzibar na Shirikisho.Mbunge wa Biharamuro
Magharibi, Dk. Mbasa, mbunge Conchesta, Katibu wa CHADEMA Manispaa ya
Bukoba, mjumbe wa Baraza Kanda ya Ziwa Magharibi, Anwar pamoja na
mwenyekiti wa chama hicho Biharamulo Magharibi, Kasaiza waliishutumu
serikali kwa kushindwa kuwaondolea umasikini wananchi wake.
Walisema kwa sasa Watanzania walio wengi wanalazimika kuvaa viatu vya
‘yebo yebo’ kwa sababu ya umasikini unaotokana na kushindwa kwa Serikali
ya CCM kuwatumikia wananchi wake kwa kuwanufaisha na rasilimali
zilizopo hapa nchini.
“Serikali ya chama tawala imekosa sifa ya kuwaongoza wananchi.
Tunahitaji tuungane wote kuiondoa CCM mwaka 2015. CHADEMA ni mkombozi wa
Watanzania na ndiyo maana wabunge na viongozi wake wanapambana usiku na
mchana kutwa kupigania maendeleo ya wananchi,” alisema Dk. Mbasa.
No comments:
Post a Comment