Banner

Banner

FOLLOW US FACEBOOK

propertyfinder.co.tz

Sunday, July 7, 2013

TBS YAPIGA MARUFUKU UUZWAJI WA MAFUTA YA KUPIKIA YA 'OKI' WADAI YANA MADHARA KIAFYA...!

Shirika la Viwango Tanzania (TBS), limebaini kuwa mafuta ya kula aina ya Oki na Viking yaliyoenea sokoni nchini, yamebainika kuwa hayafai kwa matumizi ya binadamu.
Kwa mujibu wa TBS, vipimo vyote vitatu vilivyotumika kuyapima kuonyesha ubora, vimefeli na vimeonyesha mafuta hayo kuharibika kwa haraka tangu yalipotengenezwa na mpaka leo.
Pamoja na Oki, mafuta mengine yenye walakini ni Asma, Vikingi, Partiner na Premier Gold ambayo huuzwa kwa dumu lenye ujazo wa lita 20 kwa bei ya kuanzia Sh 38,000 hadi 45,000, wakati bei ya mafuta ya kula yanayotengenezwa nchini kwa ujazo huo huuzwa kati ya Sh. 52,000 na Sh.55,000.
 
http://www.ippmedia.com/media/picture/large/OKI.jpg
Baada ya kupimwa, Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Udhibiti Ubora TBS, Lazaro Msasalaga, anasema ilithibitika kuwa mafuta ya Oki yanayozalishwa Malaysia na kupakiwa Singapore hayana ubora.
Alisema mafuta hayo yametengenezwa 2011 na kuonyesha mwisho wa kutumika ni Oktoba mwaka huu. Msasalaga alisema walipoyachunguza wamebaini hayana namba ya ufuatiliaji wakati suala hilo ni la muhimu kuwekwa.
Isitoshe, wawalipoyapima kutoka kipimo kimoja kwenda kingine, majibu yake yalishindwa na kuzidi kuonyesha mafuta hayo kuharibika kila walipoyapima.
Alisema kuna vipimo vya maabara ukipima vinaeleza mafuta kama yanafaa kutumika lakini kipimo hicho hakikufanikiwa.
“Inawezekana wakati wanayapakia walichanganya na mafuta mengine kwani vipimo vyote vitatu vinavyoonyesha ubora vimefeli na imeonyesha mafuta hayo kuharibika kwa haraka tangu yalipotengenezwa na mpaka leo hii yapo masokoni wakati hayatakiwi kukaa kwa muda huo,” alisema.
Msasalaga alisema kiasi cha maji yaliyopo kwenye mafuta ukijumlisha na vitu vingine ni uchafu kwani hayakusafishwa vizuri kuyaondoa maji hayo.
Kuhusu mafuta ya Viking, alisema na yenyewe hayapo katika ubora kutokana na baadhi ya vipimo kushindwa kutoa majibu. Alisema vipimo vitatu ambavyo vinatambulisha mafuta kuwa katika ubora ni viwili na kimoja kimeshindwa.
Alisema maji yaliyochanganywa yapo sawa ila kuna kipimo kimoja kimeshindwa kinachoashiria utunzaji wa mafuta kwa muda mrefu bila kuharibika. Aidha, mafuta hayo hayatakiwi kukaa muda mrefu kwani siyo salama.
Pia kiasi cha madini ambayo yana athari kwenye afya kimezidi kiwango kinachotakiwa jambo ambalo halikutakiwi. Mafuta haya kuingizwa nchini kinyemela ni jambo lingine la kuchukuliwa hatua kisheria dhidi ya wahusika.
Mafuta hayo yanatokea nchini Malaysia na kushushwa kisiwani Unguja, kisha kuingizwa Tanzania Bara kwa kutumia majahazi yenye uwezo wa kubeba madumu zaidi ya 900 na kupakuliwa katika ‘bandari bubu’ ya Mbweni, Dar es Salaam.
Imedaiwa kuwa mafuta hayo yamekuwa yakishushwa katika bandari bubu kwa lengo la kukwepa kodi na kuuzwa kwa wafanyabiashara wa Tanzania. Hali hiyo inayohujumu uchumi wa taifa na kuathiri afya za walaji, inafanyika huku jiji hili likiwa Makao Makuu ya vyombo vya dola vyenye mamlaka na jukumu la kudhibiti uovu huu.
Uchunguzi wa NIPASHE Jumapili umebaini kuwa licha ya mafuta hayo kutoka nje na kuuzwa kwa bei rahisi nchini, viwanda vya ndani vilikuwa katika hali mbaya kutokana na mafuta hayo kuua soko lake.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TBS, Joseph Masikitiko, alisema shirika lake litatoa taarifa kupitia vyombo vya habari ili wananchi wasiyatumie mafuta hayo.
TBS itahakikisha mafuta hayo yanaondolewa kwenye soko na wafanyabiashara wanayoagiza waache mara moja, alisistiza.
NIPASHE Jumapili ilibaini mafuta hayo kuendelea kushushwa katika bandari 'bubu' ya Mbweni huku mengine yakifichwa kwenye nyumba za jirani na eneo hilo.
Naye, Afisa Uhusiano wa Mamlaka ya TFDA, Gaudensia Simwanza alisema kuwa mafuta hayo wameyasajili na kwamba kitendo cha kuingizwa kinyemela nchini kitakuwa na walakini.
Alisema changamoto iliyopo ni bidhaa hizo kupitishwa njia za panya na hata ubora wake unaweza usiwe salama na ndio maana wanazipitishia huko.
Simwanza alisema huwa wanafuatilia sampuli mbalimbali zilizopo masokoni na kwamba kwa sasa TFDA imejipanga kuimarisha ukaguzi ili bidhaa hizo zisiingizwe katika soko pale zinapobainika zimepitia njia za panya.
Awali baada ya kuandikwa kwa taarifa hii, ilidaiwa kufukuzwa kazi baadhi ya askari baada ya kugundulika hupokea rushwa ili kuwasaidia wafanyabiashara hao kuingiza mafuta hayo sokoni.

No comments:

Post a Comment