Banner

Banner

FOLLOW US FACEBOOK

propertyfinder.co.tz

Friday, October 24, 2014

Taharuki ya ugonjwa wa Ebola kufika mjini Moshi, mkoani Kilimanjaro

 
KILIMANJARO  wakazii wa kata ya Shirimatunda, katika manispaa ya Moshi, mkoani Kilimanjaro, wamejikuta katika hali ya taharuki kufuatia taarifa za kuwepo kwa mgonjwa anayedhaniwa kuwa anaugua ugonjwa hatari  wa Ebola, ambaye amelazwa katika zahanati ya shirimatunda iliyopo kwenye kata hiyo.Mgonjwa huyo aliyefikishwa katika Zahanati hiyo Juzi majira ya Jioni, ambapo hali hiyo ilisababisha huduma za afya katika zahanati hiyo kusitishwa kwa muda usiojulikana, ambapo wagonjwa waliokuwa wakipatiwa matibabu kutoka ndani na nje ya kata hiyo kuondolewa na watoto waliokuwa wakipata chanzo katika zahanati hiyo walihamishiwa katika ofisi ya afisa mtendaji wa kata hiyo.Taarifa za awali zinadai kuwa, mgonjwa ni Raia wa Tanzania mzaliwa wa Marangu wilayani Moshi, mwenye makazi yake jijini Dar es Salaam, alipokelewa katika uwanja wa ndege wa kimataifa Kilimanjaro (KIA), akitokea nchini Senegal kikazi, ambapo alisafirishwa hadi kwenye zahanati hiyo baada ya kudai kupatwa na maumivu makali ya kichwa.Mgonjwa huyo (jina halijafahamika),  ameendelea kutibiwa hospitalini hapo na wataalam wa afya waliopo katika zahanati hiyo.Aidha taarifa zaidi zinadai kuwa wataalam wamechukua sampuli ya damu kutoka kwa mgonjwa huyo kwa ajili ya vipimo, ili kujiridhisha, wakati huduma nyingine za matibabu zikiendelea kutolewa kwa mgonjwa huyo anayedaiwa kusafiri kutoka nchini Senegal.Aidha jopo la wataalam wa afya likiongozwa na mganga mkuu wa mkoa Dk. Mtumwa Mwako, mganga wa manispaa ya Moshi Dk. Christopher Mtamakaya pamoja na watendaji wakiongozwa na mkurugenzi wa manispaa Shaban Mtarambe na viongozi wengine walionekana wakiendelea na kikao katika eneo hilo la zahanati.

Alipohojiwa na waandishi wa habari kuhusiana na tukio hilo, mkurugenzi wa manispaa ya Moshi Shaban Mtarambe, alisema hayuko tayari kuzungumza kwa maelezo kuwa suala hilo ni la kitaalam zaidi linalohitaji waataalam wa kada ya afya kulizungumzia.Jitihada za kina kumpata mganga mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro Dk. Mtumwa Mwako, kuweza kutolea ufafanuzi suala hilo zilishindikana huku kukiwa na taarifa kwamba hakuwa tayari kulizungumzia mpaka pale uchunguzi wa kina kuhusu mgonjwa huyo utakapokamilika.Kwa upande wake mwenyekiti wa mtaa wa Kigongoni kata ya Shirimatunda, Juma Sambeke, alithibitisha kuwepo kwa mgonjwa huyo baada ya kupokea taarifa kutoka viongozi wa wenzake.Mwenyekiti huyo alisema licha ya mgonjwa kufikishwa katika zahanati hiyo, uongozi wa kijiji haukuwa na taarifa huku akipokea majibu kutoka ngazi ya manispaa kuwa suala hilo linaratibiwa na mkoa.Naye diwani wa kata ya Shirimatunda Felix Mushi, alilaumu uongozi wa manispaa ya Moshi, kwa uamuzi wake wa kutenga eneo hilo kwa ajili ya wagonjwa wa ebola, jambo alilosema ni hatari kwa jamii inayozunguka zahanati hiyo.Diwani Mushi, alisema eneo hilo limezungukwa na huduma zote za kijamii, ambapo baadhi ya wazazi wamekuwa na mashaka hivyo kuzuia watoto wao kwenda shuleni.Hata hivyo waandishi wa habari waliofika eneo la tukio walishuhudia watoa huduma za afya katika zahanati hiyo wakiingia na kutoka ndani ya jengo alikolazwa mgonjwa huyo, ingawa baadhi yao hawakuwa na mavazi rasmi ya kujikinga kama ilivyo kwa wataalam wanaotoa huduma katika nchi zilizokumbwa na ugonjwa huo.

No comments:

Post a Comment