Banner

Banner

FOLLOW US FACEBOOK

propertyfinder.co.tz

Monday, October 27, 2014

Waziri wa Maliasili na Utalii aagiza uchunguzi kufanyika dhidi ya askari wa KINAPA wanaotuhumiwa kuwabaka wanawakeKILIMANJARO waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, ameagiza kufanyika uchunguzi wa haraka juu ya tuhuma za ubakaji unaodaiwa kufanywa na askari wa   hifadhi ya  Taifa ya Mlima Kilimanjaro (KINAPA) dhidi ya wanawake waliokuwa wakikata majani ndani ya hifadhi hiyo kwa nyakati tofauti.

Nyalandu ametoa agizo hilo katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika kijiji cha Mbahe wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro, kufuatia malalamiko yaliyotolewa na Mbunge wa Jimbo la Vunjo (TLP), Augustino Mrema  juu ya vitendo vya askari hao kuendesha vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadamu.

Kabla ya agizo hilo, wananchi wa kijiji hicho ambacho ni moja ya vijiji vinavyozunguka hifadhi hiyo, walimweleza waziri huyo kuwepo kwa baadhi ya askari hao, kuwabaka pindi wanapoingia katika hifadhi hiyo kwa lengo la kukata majani ya ng’ombe.

Alisema askari yeyote wa wanyamapori haruhusiwa kuwapiga, kuwatesa wala kuwafanyia vitendo vya udhalilishaji,  na kwamba hayo siyo sehemu ya majukumu yao na kuongeza kuwa  askari anapomkamata mharifu sharti  amfikishe kwenye vyombo vya sheria.

Waziri Nyalandu alisema  askari yeyote atakaye bainika  kuhusika na matukio hayo atafikishwa katika vyombo vya maamuzi na sehemu yake ya ajira  katika  wizara ya maliasili haitakuwepo akatafute kazi kwingine.

Amefafanua kuwa wapo baadhi ya askari wamekuwa wakitumia vyeo vyao vibaya, jambo ambalo limepelekea kuwepo kwa mahusiano mabaya baina ya wahifadhi na wananchi wa kawaida.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti katika mkutano huo, wananchi hao walisema askari hao wamekuwa  wakiwachapa viboko, na vitendo vya udhalilishaji  pindi  wanapoingia ndani ya hifadhi hiyo.

Mmoja wa waathirika wa matukio hayo ya ubakaji aliyejitambulisha kwa jina la  Therecia Minja mkazi wa Kijiji hicho cha Mbahe, alimweleza waziri Nyalandu kuwa alikumbwa na mkasa huo  Septemba 17 mwaka huu wakati akikata majani ambako alilazimishwa na askari hao kuvua nguo zake zote na kisha kubakwa.

Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Vunjo, Dkt Agustino Lyatonga Mrema, alisema kumekuwepo na matukio ya ubakaji na udhalilishaji wa wananchi yanayofanywa na askari wa KINAPA.

Alisema mahusiano ya askari wa hifadhi ya mlima Kilimanjaro, KINAPA na wananchi sio mazuri kwani wananchi hao wamekuwa wakibambikiziwa kesi huku wanawake wakifanyiwa vitendo vya kinyama ndani ya hifadhi hiyo.

No comments:

Post a Comment