Banner

Banner

FOLLOW US FACEBOOK

propertyfinder.co.tz

Monday, March 16, 2015

Wananchi wa Mijohoroni wataka kituo cha polisi kulinda usalama wao na mali zao


KILIMANJARO baadhi ya wananchi wanaoishi katika eneo la Mijohoroni, kando kando ya Barabara Kuu ya Arusha-Moshi, mkoani Kilimanjaro, wamelitaka Jeshi la Polisi mkoani humo kuendesha doria nyakati za mchana na usiku pamoja na kujenga Kituo kidogo cha Polisi katika eneo hilo, ili kulinda usalama wa raia na mali zao kutokana na mfululizo wa matukio ya kihalifu yanayotokea ikiwemo mauaji ya watu.

Eneo hilo pia ndipo alipouwawa Mfanyabiashara maarufu wa madini jijini Arusha, Erasto Msuya, aliyeuwawa kwa kupigwa risasi 21 katika sehemu mbalimbali za mwili wake Agosti 7, 2013 na kufa papo hapo.

Uchunguzi wa FikraPevu umebaini kuwa katika eneo hilo linasifika kwa kusababisha mauaji ya watu na serikali ya mkoa wa Kilimanjaro bado haijaamua kulitafutia ufumbuzi tatizo hilo.

Eneo hili lililowekwa mawe ndipo aliuliwa mfanyabiashara wa madini ya Tanzanite.

Kwa mujibu wa wakazi wa eneo hilo, mara kadhaa vituo vya kuuzia mafuta vimevamiwa zaidi ya mara mbili, na waporaji kufanikiwa kuchukua fedha kutoka kwa wauzaji na kuwajeruhi na kwamba hali hiyo imesababisha baadhi ya vituo kufungwa kwa muda ambao unakadiriwa kuwa miaka miwili sasa.

Licha ya matukio hayo kutokea kwa nyakati tofauti, wakazi wa eneo hilo wanasema wanaishi kwa hofu kufuatia matukio ya kuvamiwa kwa vituo hivyo na kupelekea moja ya vituo hivyo cha mafuta kufungwa na wamiliki wake kwa kuhofia kuendelea kufanya kazi kwa hofu ya kuibiwa kila wakati.

Wameitaka serikali kuweka mikakati ya kuimarisha ulinzi katika eneo hilo haraka iwezekanavyo, kwakuwa kuendelea kukaa kimya ni kuonesha kuridhika na hali ya mauaji yanayoendelea katika eneo hilo.

Mmoja wa waathirika wa matukio hayo aliyejitambulisha kwa jina la Fraisca Simon, ambaye ni Mwalimu katika Shule ya Sekondari Orkolili, amesema kwamba alipofika katika eneo la Mijohoroni alipokuwa akienda katika eneo lake la kezi (shuleni), alikwapuliwa mkoba (pochi) uliokuwa na fedha pamoja na simu na vijana wawili waliokuwa wameshikilia silaha za jadi ikiwemo visu na hivyo kunusurika kujeruhiwa na wahalifu hao.

Mwalimu Fraisca Simon akionesha eneo ambalo kibaka huyo alikua amesimama na kutoa kisu na kumtishia Mwalimu Fraisca na hatimaye kufanikiwa kumpora pochi.

Ameeleza aliposhuka kwenye gari katika kituo hicho na kukutana na vijana hao aliulizwa kama ana zawadi na alipowajibu kuwa hana, mmoja wa vijana hao alitoa kisu na kumtishia kuwa watamdhuru hivyo atoe pochi yake na mara baada ya kutekeleza agizo hilo waliifungua na kuchukua simu pamoja na fedha taslimu kisha kutokomea kusikojulikana.

Katika tukio jingine lililotokea Aprili 3, 2014 katika eneo hilo, watoto wa jamii ya kimasai wenye umri kati ya miaka (8-13) walipokuwa wakichunga mifugo katika eneo hilo walikuta miili ya watu watatu wakiwa wamekufa (inasadikiwa walinyongwa) hali iliyowafanya wapige kelele na kukimbia kwa woga, ndipo wananchi waliokua karibu waliweza kufika katika eneo la tukio na wao kutoa taarifa Polisi.

Hii ni baadhi ya mifugo ikiwa na mchungaji katika eneo la Mijohoroni.

Habari zinasema mara baada ya tukio hilo, wananchi walioshuhudia tukio hilo walitoa taarifa Polisi katika Kituo kidogo cha Polisi cha Bomang'ombe na askari wa kituo hicho walifika katika eneo la tukio na kuichukua miili ya marehemu na kuipeleka katika chumba cha kuhifadhia maiti cha Hospitali ya Wilaya ya Hai kwa ajili ya utambuzi ambapo baada ya wiki moja watu wawili walitambuliwa kwa majina ya Erick Mbando na mwingine aliyetambuliwa kwa jina moja la Bobu wote wakazi wa Kimandolu Jijini Arusha.

Mwaka huo huo, mwezi Juni, 2014 saa 12:30 mchana aliokotwa mtu mmoja ambaye hakuweza kutambulika jina akiwa ameuwawa na kutupwa kwenye shamba la mahindi kandokando mwa barabara ya Moshi – Arusha katika eneo hilo hilo la Mijohoroni.

Aidha, mwezi Februari, 2015 Mzee mmoja anayesadikiwa kuwa na umri wa miaka (60) aligongwa na gari na kutelekezwa barabarani (Gari lililomgonga halikutambulika namba mara moja).

Thomas Mcha akionesha eneo ambalo miili ya ya watu watatu ilikuwa imetupwa.

Mwaka 2013 mwezi Oktoba, mtu mmoja asiyefahamika jina wala makazi, aliyekadiriwa kuwa na miaka (50), alikutwa akiwa amekufa na kukutwa na majeraha sehemu za kifuani huku kichwa chake kikiwa kimepasuka.

Kufuatia tukio la Machi 6, 2013 wananchi wa eneo hilo wameiambia FikraPevu kuwa walipokuwa waenda kanisani walishuhudia kuona kiwiliwili cha binadamu ambacho kinasadikika kuwa kiligongwa na gari na kutelekezwa barabarani majira ya saa mbili asubuhi, huku Mbwa walikuwa wanakigombania na baada ya kutoa taarifa katika Kituo cha Polisi cha Bomang’ombe, polisi waliondoka na mwili wa marehemu.

Kamanda wa Polisi mkoani Kilimanjaro, Geofrey Kamwela alipotafutwa juu ya tukio hilo, simu yake ya mkononi ilipokelewa na Afisa ambaye hakutaka kutaja jina lake na kusema “Afande yuko Hospitalini mpigie wakati mwingine”. Juhudi za kumtafuta zinaendelea.

Hii ni makala yangu ya kwanza ndani ya Fikra pevu
==>>http://www.fikrapevu.com/hai-wananchi-mijohoroni-wataka-kituo-cha-polisi-ili-kulinda-usalama-na-mali-zao/







No comments:

Post a Comment