Banner

Banner

FOLLOW US FACEBOOK

propertyfinder.co.tz

Friday, May 15, 2015

TAARIFA YA DHARURA KWA UMMA KUHUSU KUCHANGIA DAMU HOSPITALI YA TAIFA MUHIMBILI

Image result for hospitali ya muhimbili
Menejimenti ya Hospitali ya Taifa Muhimbili inawaomba Watanzania, mashirika ya umma, mashirika yasiyo ya kiserikali, mashule, taasisi za kidini, na vyuo mbalimbali kujitokeza kusaidia kuchangia damu Hospitalini hapa ili kuokoa maisha ya wagonjwa. Hospitali inahitaji chupa za damu kwa wastani wa chupa 70 hadi 100 kwa siku.


Matumizi ya Damu:

Damu inatumika sana kwa wagonjwa wa dharura, akina mama wajawazito, wagonjwa waliofanyiwa upasuaji, watoto pamoja na wagonjwa wa saratani.

Upasuaji wa Moyo:

Kila mgonjwa wa upasuaji wa moyo anahitaji kiasi cha chupa tano mpaka sita za damu. Matumizi haya yanafanyika kabla, wakati na baada ya kufanyiwa upasuaji.

Katika juma hili kuna kambi maalum za madaktari Bingwa wa Moyo kutoka nchi mbalimbali ambao wanashirikiana na madaktari wetu kufanya upasuaji wa moyo kati ya wagonjwa watano hadi sita kwa siku na kufanya wagonjwa wa moyo pekee kuhitaji chupa 30 hadi 36 kwa siku sawa na akiba ndogo ya damu tuliyo nayo kwa siku. Kambi hizi zimeanza mapema Aprili mwaka huu na tunatarajia kuwa nazo katika kipindi cha miezi mitatu ijayo. Ili madaktari hawa waendelee kuja na kufanya upasuaji wa moyo kwa ufanisi wanahitaji uwepo wa damu.

Vyanzo vya Damu kwa MNH

Hospitali inategemea kupata damu kutoka vyanzo vikuu viwili ambavyo ni ndani ya Hospitali na kutoka Mpango wa Taifa wa Damu Salama (NBTS).

Hali Halisi ya Upatikanaji Damu kwa Sasa:

Makusanyo ya damu kutoka vyanzo vya ndani ni kati ya chupa 20 hadi 40 kwa siku zinazoweza kutumika kwa wagonjwa.

Aidha, upatikanaji wa damu kutoka Mpango wa Taifa wa Damu Salama (NBTS) ambao kisheria ndiyo wenye mamlaka ya kukusanya damu na kusambaza nchini umekuwa wa kiwango cha chini na hata wakati mwingine tumeshindwa kupata damu kutoka NBTS. Mathalani kuanzia Aprili 17, 2015 hatukuweza kupata damu hata chupa moja kutoka NBTS hali iliyopelekea upungufu mkubwa wa damu Hospitalini hapa kulingana na mahitaji.

Hospitali imejipanga kupitia Kitengo chake cha Uchangiaji Damu kilichopo Maabara Kuu ya Hospitali ya Taifa Muhimbili kuwapokea watu watakaojitokeza kuchangia damu.

Imetolewa na;
Aminiel Aligaesha
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Umma na Huduma kwa Wateja
Hospitali ya Taifa Muhimbili
Mei 11, 2015

No comments:

Post a Comment