Mbunge wa Jimbo la Singida Kaskazini (CCM), Lazaro Samwel Nyalandu amewahimiza madiwani kuwandaa wananchi mapema kwa ajili ya kupokea na kutumia vizuri shilingi Milioni 50 za Rais Magufuli ili ziweze kuwasaidia kuboresha hali zao za kiuchumi.

Nyalandu ametoa wito huo jana wakati akizungumza mbele ya wajumbe wa kamati ya huduma za jamii halmashauri ya wilaya ya Singida.

Alisema mkoa wa Singida umepata bahati ya kuwa miongoni mwa mikoa 10 nchini, ambayo itakuwa ya awamu ya kwanza kunufaika na fedha hizo ambazo ni ahadi ya rais aliyoitoa wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu uliopita.

“Kwa bahati hii sisi wawakilishi wa wananchi tunapaswa kuimba wimbo moja nao ni kuwandaa wananchi wetu mapema ili waweze kuchangamkia fursa hii ambayo itawasaidia kujiongezea kipato kitakachowasaidia kuishi maisha bora,” alisema Nyalandu ambaye ameongoza jimbo hilo kwa vipindi vinne.

Akisisitiza, alisema kuwa wananchi wanapaswa kuelimishwa pia kuwa fedha hizo ni za mzunguko, mwananchi akikopeshwa analazimika kuzirejesha kwa wakati ili mwananchi mwingine naye aweze kunufaika kwa fedha hizo na kudai kwamba hizo fedha zinalenga kuwanufaisha wananchi wote wa kijiji husika.

Aidha, Nyalandu alisema kuwandaa huko kuende sambasamba na kuwasaidia kuanzisha vikundi ujasiriamali na kuvisajili vile vile kuwasaidia kubuni miradi yenye tija itakayowasaidia kurejesha fedha na kupata faida ya kukidhi mahitaji.

“Nimelileta hili mbele yenu mapema ili sote tuweze kujipanga vizuri na mwisho wa siku,jimbo letu liwe mfano wa kuigwa na majimbo mengine mkoani kwetu na hata ya nje ya mkoa kwa matumizi sahihi na mazuri ya fedha za rais Magufuli,” alisema Nyalandu.

Wakati huo huo, mbunge huyo alisema kuwa fedha za mfuko wake wa jimbo zote amezielekeza katika ununuzi wa madawati ya shule za msingi na sekondari.