Banner

Banner

FOLLOW US FACEBOOK

propertyfinder.co.tz

Monday, June 15, 2026

TAARIFA KWA UMMA

 

Ofisi ya Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, inapinga na kukanusha vikali taarifa ya uongo na upotoshaji inayosambaa mitandaoni, ikidai kuwa Dkt. Kikwete anahusishwa na mradi unaodaiwa kuwa wa uwekezaji unaowaahidi Watanzania kipato cha uhakika kupitia jukwaa la kifedha linalotumia teknolojia ya akili mnemba.

Taarifa hiyo inadai kuwa maelfu ya Watanzania tayari wamenufaika na mradi huo baada ya kuwekeza kiasi cha shilingi 653,000, huku wakiahidiwa kupata zaidi ya shilingi 9,200,000 kwa mwezi. Madai hayo si ya kweli hata kidogo.

Ofisi ya Rais Mstaafu inapenda kuweka wazi kwamba Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete hajawahi kushiriki, kuidhinisha, kutangaza, kuunga mkono, wala kuhusika kwa namna yoyote ile na mpango huo wa kifedha. Ofisi yake haijawahi kuruhusu matumizi ya jina, picha, au heshima yake kuhusishwa na mradi huo unaodaiwa, na haitajihusisha na shughuli za aina hiyo.

Wananchi wanashauriwa kupuuza taarifa hiyo ya uongo na kuwa makini dhidi ya miradi ya kitapeli na vitendo haramu vya aina hiyo. Mtu yeyote atakayekutana na taarifa kama hizo za upotoshaji anapaswa kuzichukulia kama habari za uongo, kuepuka kuzisambaza, kujisajili, au kutuma fedha kwa mtu au jukwaa lolote linalohusishwa nazo.

TAARIFA YA UONGO IPUUZWE.

Marekani na Iran Zafikia Makubaliano ya Amani

 


#HABARI Baada ya miezi ya mvutano uliotikisa Mashariki ya Kati, Marekani na Iran zimetangaza kufikia makubaliano ya awali ya kumaliza mzozo uliokuwa ukiendelea kati yao. 

Hatua hiyo imeelezwa kama mafanikio makubwa ya kidiplomasia yanayolenga kurejesha utulivu katika eneo hilo.

Rais wa Marekani Donald Trump alitangaza kuwa makubaliano hayo yamekamilika, huku Waziri Mkuu wa Pakistan Shehbaz Sharif akisema nchi yake ilisaidia katika mazungumzo yaliyowezesha kufikiwa kwa mwafaka huo. 

Makubaliano hayo yanajumuisha kusitishwa mara moja kwa operesheni zote za kijeshi katika maeneo ya mapigano, ikiwemo Lebanon.

Aidha, Iran imethibitisha kuwa shughuli za kijeshi zitasitishwa kuanzia Jumatatu usiku. 

Makubaliano hayo pia yanatarajiwa kufungua tena Mlango-Bahari wa Hormuz, njia muhimu ya usafirishaji wa mafuta na gesi duniani, hatua inayoweza kusaidia kuimarisha biashara na uchumi wa kimataifa.

Sunday, June 14, 2026

WAZIRI SHEMDOE AAGIZA UJENZI WA BARABARA ZA AFCON KUJENGWA USIKU NA MCHANA

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM -TAMISEMI) Prof. Riziki Shemdoe amemshukuru Rais wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uwekezaji mkubwa alioufanya Mkoani Arusha katika ujenzi wa barabara kuelekea katika mashindano ya Mpira wa miguu kwa Mataifa ya Afrika (AFCON 2027) inayotarajiwa kuchezwa katika Mikoa ya Arusha, Dar Es Salaam na Visiwani Zanzibar.

Profesa Shemdoe ametoa shukrani hizo leo Jumapili Juni 14, 2026 wakati wa ziara yake Mkoani Arusha, akiambatana na Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. CPA Amos Gabriel Makalla na viongozi wengine wa Serikali na Chama Cha Mapinduzi CCM, kukagua mradi wa uwanja wa AFCON pamoja na barabara ya kuingia katika uwanja huo unaojengwa kwenye Kata ya Olmot, Jijini Arusha, akiagiza kasi zaidi katika kukamilisha kazi hizo.

"Kwa kazi hizi kwakweli najisikia fahari kuwa Mtanzania. Nielekeze kazi ya ujenzi wa barabara ifanyike usiku na mchana, niagize pia uadilifu katika usimamizi na utoaji wa  fidia kwa wananchi waliopisha ujenzi wa barabara hii. Nimshukuru sana Mhe. Rais kwa kutoa zaidi ya Shilingi Bilioni 80 ya ujenzi wa barabara hizi na zipo pia Bilioni 14.8 kwaajili ya fidia kwa wananchi." Amesema Mhe. Waziri.

Kwa upande wake Mhe. Makalla ameahidi kusimamia kikamilifu maelekezo yote ya Mhe. Waziri Shemdoe, ikiwemo usimamizi wa ujenzi wa uwanja huo wa AFCON pamoja na miundombinu ya barabara na maboresho ya viwanja vya ndege, ikiwemo barabara za kutoka Uwanja wa Ndege wa Kilimanjaro mpaka kufika katika uwanja huo wa Michezo.

Mapema katika maelezo yao, Msimamizi wa uwanja wa AFCON kutoka Wizara ya Habari, Utamaduni, sanaa na Michezo Bw. Martin Chomo na Mkurugenzi wa barabara kutoka Wakala wa barabara za Vijijini na Mijini TARURA, Injinia Venant Komba, wameeleza kuhusu maendeleo ya miradi hiyo na kuahidi kukamilisha kwa wakati ikiwemo viwanja vidogo vitano vitakavyotumika kwaajili ya mazoezi kwa Timu zitakazopangiwa kucheza Michezo yake Mkoani hapa.

Saturday, June 13, 2026

WAZIRI MKUU AAGIZA BIDHAA ZILIZOCHUKULIWA KWA WAFANYABIASHARA SHELUI KUREJESHWA MARA MOJA

Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba ameagiza bidhaa zilizochukuliwa kutoka kwa baadhi ya wafanyabiashara wadogo wa Tarafa ya Shelui, Wilaya ya Iramba mkoani Singida kurejeshwa mara moja na kuwataka watendaji wa taasisi za udhibiti kuacha kuchukua mitaji ya wananchi wakati wa utekelezaji wa shughuli za ukaguzi.

Dkt. Mwigulu ametoa maelekezo hayo leo, Jumamosi Juni 13, 2026, alipokuwa akizungumza, kusikiliza na kutatua changamoto za wananchi wa Tarafa ya Shelui katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Uwanja wa Mnadani, Kata ya Mgongo, Wilaya ya Iramba.

Ametoa agizo hilo baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa wafanyabiashara wadogo waliodai kuchukuliwa kwa mafuta yao na baadhi ya watendaji wa taasisi za udhibiti, hali iliyowaathiri katika shughuli zao za kujipatia kipato.

Akizungumza kuhusu suala hilo, Waziri Mkuu alihoji sababu za kuchukuliwa kwa bidhaa hizo na kusisitiza kuwa Serikali haitaki kuona wananchi wanaojitafutia kipato kupitia biashara ndogo ndogo wakinyang’anywa mitaji yao.

“Ulikuwa unafuatilia ziara za Waziri Mkuu? Nilisemaje kuhusu kuchukua bidhaa za wananchi? Kwa nini mmechukua? Huo ni mtaji wake. Dumu moja la mafuta ndiyo mtaji wake. Nimewaambia msikamate hata bakuli la maharage, nyinyi kwa nini mmeenda kuchukua mafuta yao?” amesema Dkt. Mwigulu.

Aidha, aliagiza bidhaa hizo kurejeshwa mara moja kwa wahusika.

“Itarudishwa leo leo. Muwatafute leo leo muwarudishie bidhaa zao. Nimeshaelekeza yarudishwe leo leo na waendelee na shughuli zao,” amesema.

Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo kuwataka watendaji wote wanaosimamia shughuli za udhibiti nchini kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia sheria, kanuni na miongozo bila kuathiri shughuli halali za kiuchumi za wananchi.

“Narejea tena, watu wote mnaosimamia mambo ya udhibiti, msichukue bidhaa za wananchi. Hizo ni ofisi zao, hiyo ni mitaji yao. Msichukue bidhaa za wananchi, msichukue bidhaa za Watanzania. Hizo ni ofisi zao,” amesema.

Katika hatua nyingine, Dkt. Mwigulu amesema Serikali itaendelea kuimarisha huduma za maji nchini kupitia utekelezaji wa Mradi wa Maji wa Ziwa Victoria, miradi ya miji 28 pamoja na miradi ya visima kwa lengo la kuongeza upatikanaji wa maji safi na salama kwa wananchi wa Mkoa wa Singida na maeneo mengine nchini.

Amesema miradi hiyo ni sehemu ya jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan za kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za maji na kupunguza changamoto ya upatikanaji wa huduma hiyo katika maeneo mbalimbali nchini.

“Tunao mradi huu wa kutokea Ziwa Victoria, tunao mradi wa visima, tunao mradi wa miji 28. Miradi yote hii inalenga kuhakikisha wananchi wanapata maji safi na salama. Kabla maji ya Ziwa Victoria hayajafika Dodoma, yatakuwa yameshasambaa katika vijiji mbalimbali vya Wilaya ya Iramba pamoja na maeneo mengine ya Mkoa wa Singida,” amesema.

Waziri Mkuu amesema Serikali itaendelea kufuatilia utekelezaji wa miradi hiyo katika mwaka mpya wa fedha ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya maji kwa uhakika zaidi.

Kuhusu huduma za afya, Dkt. Mwigulu ameagiza kupelekwa kwa gari la wagonjwa (ambulance) katika Tarafa ya Shelui ndani ya wiki mbili ili kuboresha huduma za dharura kwa wananchi wa eneo hilo.

“Ndani ya wiki hizi mbili tutakuwa tumeleta gari la wagonjwa katika Tarafa ya Shelui. Hivi tunavyoongea dereva wa kwenda kulichukua yuko Dar es Salaam. Kwa hiyo ambulance itakuja ili tumalize changamoto hii ambayo wananchi wameiwasilisha,” amesema.

Aidha, amesema Serikali itaendelea kuboresha miundombinu ya afya ikiwemo Kituo cha Afya Mgongo pamoja na kuendeleza mipango ya ujenzi wa miundombinu mingine ya afya katika wilaya hiyo.

Akizungumzia miundombinu ya barabara, Waziri Mkuu amesema Serikali inaendelea na usanifu wa miradi mbalimbali ya barabara na madaraja ili kuboresha mawasiliano na kurahisisha shughuli za kiuchumi na kijamii kwa wananchi wa Wilaya ya Iramba na maeneo jirani.

Wakati huo huo, Dkt. Mwigulu ameagiza viongozi wa Wilaya ya Iramba pamoja na mamlaka husika kukutana na wadau wa sekta ya madini ili kujadili changamoto zilizowasilishwa na wachimbaji wadogo na kutafuta suluhisho litakalolinda maslahi ya wananchi, wawekezaji na Serikali.

“Kesho tukutane tujadili kwa pamoja. Tutawasikiliza wote ili tuweze kupata suluhisho ambalo litalinda maslahi ya wananchi wetu na wakati huo huo kuendeleza uwekezaji,” amesema.

Friday, June 12, 2026

DKT. MWIGULU: SERIKALI INATHAMINI MCHANGO WA SEKTA BINAFSI KATIKA KUINUA UBORA WA ELIMU NCHINI

 


Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba amesema Serikali itaendelea kuthamini na kuimarisha ushirikiano na sekta binafsi katika sekta ya elimu kutokana na mchango wake mkubwa kwenye kuongeza ubora wa elimu na kuandaa rasilimali watu yenye maarifa, ujuzi na maadili yanayohitajika katika maendeleo ya Taifa.

Dkt. Mwigulu amesema hayo alipokuwa Mgeni Rasmi katika Mahafali ya 11 ya wahitimu wa Kidato cha Nne (Year 11–IGCSE) wa mwaka wa masomo 2025/2026 ya Shule ya Kimataifa ya Feza yaliyofanyika Salasala, Dar es Salaam, leo Ijumaa, Juni 12, 2026.

"Nimekuja leo kwa kuwa Serikali inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inatambua ubia huu muhimu ambao shule yenu imekuwa ikifanya katika sekta ya elimu. Hatuwezi kuyataja mafanikio katika sekta ya elimu bila kutaja mchango wa shule za sekta binafsi, na kwa umuhususi shule za Feza," amesema Dkt. Mwigulu.

Amesema Taasisi ya Feza ni miongoni mwa taasisi zilizochangia kwa kiasi kikubwa mageuzi ya elimu nchini kwa kuweka viwango vya juu vya ubora wa elimu vinavyotambulika ndani na nje ya Tanzania.

"Hatungeweza kutaja mabadiliko na mageuzi makubwa yaliyofanyika katika sekta ya elimu bila kutaja mchango wa shule za Feza. Mmekuwa chachu ya mageuzi makubwa yaliyofanyika katika sekta ya elimu," amesema.

Aidha, Waziri Mkuu ameipongeza Taasisi ya Feza kwa kuendelea kuvutia wanafunzi kutoka mataifa mbalimbali duniani, hatua inayoonesha kiwango cha ubora wa elimu inayotolewa na taasisi hiyo.

"Sina shaka nyote mtakubaliana nami kuwa viwango vya ubora wa shule hizi vimekuwa chachu ya kuvutia wanafunzi kutoka mataifa mbalimbali ikiwemo India, Uturuki, China, Falme za Kiarabu, Lebanon, Somalia, Marekani na nchi nyingine," amesema.

Waziri Mkuu amesema Serikali inaendelea kutekeleza mageuzi mbalimbali katika sekta ya elimu ili kuhakikisha mfumo wa elimu unaendana na mahitaji ya sasa ya dunia pamoja na maendeleo ya sayansi na teknolojia.

Amesema mojawapo ya hatua hizo ni utekelezaji wa Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014, Toleo la 2023, inayolenga kuimarisha upatikanaji wa elimu bora na kufanya elimu ya lazima kuwa ya miaka 10.

"Tumeyafanya mageuzi haya kwa kuzingatia mabadiliko makubwa yanayotokea duniani na kwa lengo la kuwaandaa vijana wa Kitanzania kukabiliana na changamoto na fursa za dunia ya sasa," amesema.

Sambamba na hilo, Dkt. Mwigulu ameipongeza Taasisi ya Feza kwa mchango wake katika utekelezaji wa miradi ya uwajibikaji kwa jamii ikiwemo kusaidia wanafunzi wenye uhitaji, kuboresha miundombinu ya shule za umma na kuchimba visima vya maji katika maeneo mbalimbali nchini.

Akizungumzia nafasi ya elimu katika maendeleo ya Taifa, Waziri Mkuu amesema uwekezaji katika rasilimali watu ndiyo msingi wa maendeleo endelevu ya nchi yoyote duniani.

"Hakuna nchi yoyote iliyowahi kuendelea bila kuwekeza katika rasilimali watu ya kiwango cha juu. Hizi rasilimali nyingine zinaweza zisiwepo, lakini ukiwa na watu wenye maarifa, ujuzi na maadili unaweza kujenga Taifa lenye maendeleo makubwa," amesema.

Aidha, amewataka wahitimu kuendelea kuwa na nidhamu, kutumia maarifa waliyojifunza kwa manufaa ya jamii na Taifa, pamoja na kutumia mitandao ya kijamii kwa tija.

"Mkawe mabalozi wazuri wa mafunzo mliyoyapata hapa. Mafanikio ya kweli hayatapimwa kwa matokeo ya mitihani pekee, bali kwa aina ya watu mtakaokuwa baada ya hapa," amesema.

RAIS SAMIA AONGOZA MAADHIMISHO YA MIAKA 60 YA BENKI KUU YA TANZANIA




Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameshiriki Maadhimisho ya Miaka 60 ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) yaliyofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam tarehe 12 Juni, 2026.

Maadhimisho hayo yamekuwa fursa ya kutafakari mchango mkubwa wa Benki Kuu katika kusimamia uthabiti wa uchumi, mfumo wa fedha na maendeleo ya sekta ya kifedha nchini kwa kipindi cha miongo sita.

Katika kipindi cha miaka 60, Benki Kuu ya Tanzania imeendelea kuwa nguzo muhimu katika kuimarisha uchumi wa taifa, kudhibiti mfumuko wa bei, kusimamia sera za fedha na kuimarisha mazingira ya uwekezaji yanayochochea ukuaji wa uchumi na maendeleo ya wananchi.

Ushiriki wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika maadhimisho hayo unaonesha dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kuendelea kuimarisha sekta ya fedha na kujenga uchumi imara, shindani na jumuishi kwa manufaa ya Watanzania wote.

Thursday, June 11, 2026

NDG RABIA KUZUNGUMZA NA MAKUNDI MBALIMBALI YA KIJAMII, TAASISI, NGO’s NA VYAMA MBALIMBALI VYA KIJAMII

Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa Idara ya Mambo ya Siasa na Uhusiano wa Kimataifa-SUKI Ndg Rabia Abdalla Hamid anatarajia kufanya ziara ya kuzungumza na Makundi mbalimbali ya Kijamii, Taasisi, NGO’s na vyama vya kijamii katika mikoa ya Lindi, Mtwara, Ruvuma na Njombe, kama ifuatavyo;

1. Tarehe 14/06/2026 Lindi

2. ⁠Tarehe 15/06/2026 Mtwara

3. ⁠Tarehe 17/06/2026 Ruvuma

4. ⁠Tarehe 18/06/2026 Njombe

Makundi ya kijamii ya wakulima, wafugaji, wachimbaji wa madini, wavuvi, wenye mahitaji Maalum, wanavyuo, Vyama vya ushirika, Wajane, Mama Lishe na Baba lishe, Maafisa Usafirishaji (Bodaboda, bajaji, daladala, maguta), vikundi mbalimbali vya wajasiliamali nyote mnakaribishwa kusema changamoto mbalimbali zinazowakabili, CCM ndio kimbilio la Makundi yote ya kijamii, Ndg Rabia Abdalla Hamid atakusikiliza na kutatua kero inayokabili kikundi chochote cha jamii katika jamii.

Aidha, Mwenyekiti wa CCM na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amedhamiria kuacha Tabasamu kwa kila Mtanzania.