Banner

Banner

FOLLOW US FACEBOOK

propertyfinder.co.tz

Thursday, December 18, 2025

MSIGWA: SERIKALI YAIMARISHA USHIRIKIANO NA WAANDISHI WA HABARI MTANDAONI



 

Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, ambaye pia ni Msemaji Mkuu wa Serikali, Ndg. Gerson Msigwa, amesema Serikali ya Awamu ya Sita imeendelea kuimarisha ushirikiano na waandishi wa habari wa mitandaoni pamoja na mabloga kwa lengo la kujenga tasnia ya habari iliyo imara, yenye weledi na inayolinda maslahi ya taifa.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Ndg. Msigwa alisema Serikali imechagua mkondo wa kushirikiana na kuwalea wadau wa habari badala ya kuchukua hatua za adhabu, akibainisha kuwa mitandao ya kijamii imekuwa sehemu muhimu ya mawasiliano ya kisasa na ujenzi wa taifa.

Alieleza kuwa katika dunia ya sasa, mapambano mengi yamehama kutoka kwenye uwanja wa kijeshi kwenda kwenye uwanja wa taarifa, hali inayofanya kazi ya waandishi wa habari kuwa nyeti kwa mustakabali wa nchi.

“Habari mnazozitoa zinaweza kuijenga nchi au kuharibu taswira yake. Ndiyo maana Serikali inaona umuhimu wa kushirikiana nanyi,” alisema Msigwa.

Katibu Mkuu huyo aliipongeza Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kwa mwelekeo wake wa kulea wadau wa sekta ya habari, akisema hatua hiyo imeongeza imani kati ya Serikali na waandishi wa habari wa mitandaoni. Aidha, aliitaja TBN na JUMIKITA kuwa ni wadau wakubwa wa Serikali katika kusambaza taarifa sahihi kwa umma.


Ndg. Msigwa aliwahakikishia waandishi wa habari ulinzi wa Serikali, akieleza kuwa endapo sheria, kanuni au sera zitabainika kuwa kikwazo katika utekelezaji wa majukumu yao, Serikali iko tayari kuzifanyia marekebisho kwa maslahi mapana ya taifa.

Ameongeza kuwa Serikali, kwa kushirikiana na TCRA na Wizara ya Habari, ipo katika maandalizi ya kutoa mafunzo maalum kwa waandishi wa habari wa mitandaoni pamoja na kuandaa mikakati ya kuwawezesha kiuchumi.

Kuhusu masuala ya kodi, alisema Serikali itaendelea kushirikiana na TRA ili kutatua changamoto zinazowakabili waandishi wa habari wa mitandaoni, huku ikitambua mchango wao mkubwa katika kuitangaza Tanzania na kuvutia wawekezaji.

Akihitimisha, Ndg. Msigwa aliwataka waandishi wa habari kutumia majukwaa yao kwa uzalendo, uwajibikaji na weledi, akisisitiza kuwa Serikali inawaona kama washirika muhimu katika ujenzi wa taifa na kuimarisha demokrasia.














No comments:

Post a Comment