LICHA
ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kuwataka madaktari nchini kurejea
katika meza ya mazungumzo, kwa maelezo kuwa baadhi ya madai yao
yameshughulikiwa, wataalamu hao wamemjibu wakisisitiza kwamba mgomo wao
upo pale pale kuanzia kesho.
Madaktari
hao wamesema kuwa Waziri Mkuu, amelidanganya Bunge jana wakati akijibu
maswali ya papo kwa hapo, kwa kuesema kuwa kati ya madai yao kumi
waliyowasilisha, matano yameafikiwa na kila upande.
Kwa
mujibu wa madaktari, wiki mbili za mgogoro na serikali walizozitoa
zinamalizika leo, hivyo kuanzia kesho kada zote wanaingia katika mgomo
usiokuwa na kikomo.
Majibu
ya madaktari hao, yalitoka na kauli ya Pinda bungeni jana wakati
akijibu swali la Kiongozi wa Kambi ya Upinzani, Freeman Mbowe
(CHADEMA), aliyetaka kujua malumbano kati ya serikali, madaktari na
walimu yatatatuliwa lini ili kuepusha mgomo.
Katika
hilo, Pinda, alilieleza Bunge kuwa tangu awali serikali iliunda kamati
maalumu ya kushughulikia suala hilo ambapo miongoni mwa madai yao
kumi, matano yameafikiwa na kila upande.
“Ninajua
uzito wa hili jambo na lilipotokea tulijitahidi kuhakikisha tunaunda
kamati maalumu ili kuweza kushughulikia masuala haya, na kwa mujibu wa
kamati ni mambo matano kati ya kumi, tumeafikiana kwa pamoja,” alisema
na kuongeza kuwa:
“Baada
ya hatua zote hizo kwa mujibu wa sheria ni lazima makubaliano yao
yasajiliwe na Tume ya Usuluhishi (CMA), na kwamba hilo limefanyika
ambapo tume ya serikali na upande wa madaktari wamemaliza kazi yake.
“Hata
hivyo mambo matano yaliyobaki, nilimuagiza tena Waziri wa Afya
awaandikie barua madaktari ili waweze kukutana, lakini hadi juzi
wanajibu barua ile wanasema hawazezi kukutana tena na serikali kwa
sababu haijatelekeza madai yao,” alisema Pinda.
Kwamba
kati ya madai waliyotaka na serikali imeyatekeleza ni pamoja na
kuondolewa kwa mawaziri wa wizara hiyo, kuongezwa posho ya kuitwa
kazini, kufanya uchunguzi wa maiti na nyinginezo.
“Lakini
pamoja na hali hii serikali ilifungua kesi ikilalamikia mgomo wa
madaktari uliotokea mwanzoni mwa mwaka huu, tume ya usuluhishi
ilizitaka pande mbili, kamati ya serikali na wawakilishi wa madaktari
kukaa meza moja na kuzungumza Juni 19, mwaka huu,” alisema.
Alifafanua
kuwa mambo matano waliyoafikiana ni serikali kukubali kuongeza posho
ya kuitwa kazini kutoka sh 10,000 hadi sh 15,000 kwa madaktari walio
kwenye mafunzo kazini na sh 20,000 kwa madaktari na sh 25,000 kwa
madaktari bingwa.
“Pia
serikali iliongeza posho ya uchunguzi wa maiti kutoka sh 10,000 hadi
100,000 kwa madaktari na sh 50,000 kwa wasaidizi,” alisema Waziri Mkuu
Pinda.
Aliongeza
kuwa serikali ilikubali kuwapa kadi ya Bima ya Afya ya rangi ya kijani
ambayo ina hadhi ya huduma za daraja la kwanza kwa madaktari, pia
kutoa chanjo ya ugonjwa wa ini ambapo fedha za chanjo hiyo zimo kwenye
bajeti ya mwaka ujao wa fedha 2012/2013.
Hata
hivyo, maelezo yake ylipingwa na Chama cha Madaktari (MAT), ambapo kwa
niaba yao, Mwenyekiti wa Jumuiya ya wanataaluma hao, Dk. Steven
Ulimboka, alisema kuwa hawako tayari kupeleka suala hilo katika
Mahakama ya Kazi kama alivyoeleza waziri mkuu.
Alisema
ni jambo la aibu kwa viongozi wakuu wa serikali kuamua kwa makusudi
kulidanganya Bunge wakati wakijua wazi hakuna utekelezaji wa aina
yoyote uliofanywa.
Mwenyekiti
huyo alisema kuwa katika madai yote ya madaktari hakuna dai hata moja
ambalo limetekelezwa kama inavyoelezwa na viongozi.
Alisema kitu cha kushangaza hata taarifa ya ufafanuzi wa madai yao hakuna eneo ambalo serikali imeweka saini.
“Mgomo
huu ni wa madaktari wa ngazi zote nchini ambao hauna kikomo na
tunachohitaji ni kuelezwa na serikali hatua waliyofanya kuliko
wanavyoendesha propaganda na kuweka siasa katika madai yetu,” alisema.
Alisema
pamoja na madai yaliyotolewa na madaktari lakini kitu cha ajabu
kilichofanywa na serikali ni kuamua kuchomeka dai la posho ya uchunguzi
wa maiti ambalo halijawahi kutolewa na madaktari.
“Serikali
inataka kutafuta ionekane imetenda mema kwa madaktari kwa kudai
kupandisha kima cha posho ya uchunguzi wa maiti kutoka sh 10,000 hadi
sh 100,000 wakati sisi hatujawahi kuomba posho hiyo,” alisema.
Alisema
posho hiyo si muhimu kwa madaktari kwa kuwa wapo baadhi ya madaktari
wanaoweza kufanya kazi kwa zaidi ya miaka 30 bila kufanya uchunguzi
huo.
Dk.
Ulimboka alisema kuwa Watanzania hawapaswi kuwalaumu madaktari kwa
kuwa anayepaswa kubebeshwa lawama hizo ni serikali iliyoshindwa
kuboresha afya pamoja na kutatua migogoro.
Alisema
walitegemea kwa siku 90 walizokaa katika meza ya majadiliano na kamati
iliyoundwa na serikali wangepata ufumbuzi wa madai yao, matokeo yake
imekuwa ni matatizo zaidi.
“Kuhusu huduma za dharura katika maeneo nyeti watakaa na kutafuta ufumbuzi hapo baadaye,” alisema.
Habari hii imeandaliwa na Charles Misango na Danson Kaijage (Dodoma), Betty Kangonga na Chalila Kibuda (Dar).
No comments:
Post a Comment