Banner

Banner

FOLLOW US FACEBOOK

propertyfinder.co.tz

Tuesday, July 10, 2012

KILIO CHA ABIRIA WA ARUSHA NA MOSHI...!

Abiria wakiwa stand ya Moshi wakisubiri wenye mabasi watakacho kiamua kuhusu mgomo.

Daniel Mjema, Moshi na Peter Saramba, Arusha
MGOMO mkubwa wa wamiliki wa mabasi jana uliathiri huduma za usafiri kati ya Miji ya Arusha na Moshi mkoani Kilimanjaro, na kusababisha adha ya usafiri kwa abiria na ulanguzi wa nauli kutoka Sh2,500 ya kusafiri kati ya miji hiyo miwili hadi kufikia Sh10,000.

Juzi, mgomo huo ulitikisa zaidi usafiri wa mabasi ndani ya Mkoa wa Kilimanjaro baada ya wamiliki kupinga hatua ya Halmashauri ya Manispaa ya  Moshi kuongeza ushuru kutoka kiasi cha Sh1,000 hadi kufikia Sh2,000 bila kushirikishwa.

Mgomo huo jana, uliingia katika hatua mpya baada ya wamiliki wenzao wa Mkoa wa Arusha nao kuingia katika mgomo na kusababisha msururu wa watu barabarani, huku watoa huduma za pikipiki maarufu kama bodaboda wakineemeka na mgomo huo.

Mbali ya bodaboda kutoa huduma, baadhi ya abiria waliokuwa wakisafiri kati ya Arusha na Moshi  walilazimika kutumia usafiri wa magari madogo aina ya Naoh, ambayo yalikuwa yakipakia abiria kwa kificho pembezoni mwa miji hiyo kuepuka kushambuliwa na wasafirishaji waliokuwa kwenye mgomo.

Abiria walioathiriwa zaidi na mgomo huo ulioanza saa 11:00 alfajiri ni wale waliokuwa wakisafiri kati ya Moshi-Arusha na wilaya nyingine za Mkoa wa  Kilimanjaro na wanaotegemea usafiri wa daladala.

Misururu mirefu ya abiria wakiwamo wanafunzi walionekana wakitembea kwa miguu kutoka majumbani kwenda shuleni, huku watu wengine wanaokwenda kazini nao wakijikuta katika adha hiyo na kulazimika kutumia usafiri wa malori na toyota aina ya Pick-Up.


Manispaa ya Moshi imepandisha ushuru kutoka Sh1,000 kwa siku kwa basi dogo hadi Sh1,500 na kutoka Sh1,000 hadi Sh2,000, sawa na ongezeko la asilimia 100.

Kauli ya Akiboa
Katibu wa Chama cha Wasafirishaji abiria Mikoa ya Arusha na Kilimanjaro (Akiboa), Locken Adolf alithibitisha jana wanachama wake
kugoma kushinikiza Halmashauri ya Manispaa ya Moshi kukaa nao mezani kujadili ongezeko hilo.

“Kimsingi, hatupingi ushuru wa Serikali, tunachopinga ni manispaa kuongeza ushuru wa maegesho kwenye stendi za Moshi kwa asilimia 100 kutoka Sh1,000 ya awali hadi Sh2,000 bila hata kushauriana na sisi wadau wa usafirishaji,” alisema Locken.

Alifafanua kwamba, baada ya juhudi zao kutafuta ufumbuzi wa suala hilo kupitia
vikao walivyofanya kati yao na uongozi wa Manispaa ya Moshi pamoja na
ofisi ya mkuu wa wilaya kushindikana, wameamua kusitisha huduma hadi mwafaka utakapopatikana.

Katibu huyo wa Akiboa alisema, kilichowasukuma kugoma ni kauli aliyodai kutolewa na Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Dk Ibrahim Msengi na
uongozi wa Manispaa kuwa mfanyabiashara asiyemudu kulipa ushuru huo
aegeshe gari lake nyumbani.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Akiboa, Hussein Mfinanga alisema mgomo huo unatarajiwa kudumu kwa siku tatu mfululizo.Mfinanga alisema kwa ongezeko hilo la ushuru kwa halmashauri hizo mbili, kunaamaanisha kuwa mmiliki wa mabasi atalipa ushuru mkubwa kuliko unaotozwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania(TRA).

“TRA ambako ndio sheria mama ya kodi ipo na inapitishwa na Bunge tunalipa Sh190,000 kwa Hiace na 520,000 kwa mabasi makubwa kwa mwaka, iweje ushuru wa halmashauri uwe juu ya TRA?,”alihoji.

Kiongozi huyo alisema kwa siku ya jana baadhi ya mabasi makubwa ya abiria kwenda Dar es Salaam  na Morogoro, yaliendelea na safari kwa kuwa tayari walikuwa wamewakatia abiria wao tiketi.

Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani mkoani  Kilimanjaro, Peter Simma alipoulizwa juu ya msimamo huo, alisema wanaopaswa kubebeshwa mzigo wa suala hilo ni Halmashauri ya Manispaa ya Moshi.

Meya wa Manispaa hiyo, Jaffar Michael alisema ushuru huo ulipandishwa kwa nia njema ili kupanua wigo wa mapato ambayo yatatumika katika shughuli za miradi ya maendeleo ya wananchi.

Alifafanua kwamba kwa sasa wapo kwenye mazungumzo na mkurugenzi wa halmashauri hiyo kuangalia kama wasitishe viwango hivyo vipya kwa muda wakati wakiendelea kujadiliana na wadau

Hata hivyo, kwa Arusha magari madogo ya abiria maarufu kama daladala yanayofanya safari zake ndani ya jiji hilo na vitongoji vyake, yaliendelea kutoa huduma wakati usafiri wa ndani ya Mkoa ya  Kilimanjaro hakukuwa na huduma hizo za usafiri baada ya daladala nazo kuingia kwenye mgomo huo.

Kwa upande wao wamiliki wa daladala, wanapinga ongezeko la ushuru kutoka Sh1,000 hadi Sh1,500 kwa madai hayo ya kutoshirikishwa kabla ya uamuzi huo kufikiwa na Halmashauri ya Manispaa ya Moshi.

Wakati hali ikiwa hivyo, kuna madai kuwa mgomo huo una mkono wa vyama vya siasa huku Chama Cha Mapinduzi (CCM) kikituhumiwa kuhujumu Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ambacho kinaongoza halmashauri hiyo.

Hata hivyo, Katibu wa CCM Wilaya ya Moshi, Alu Sigamba alikanusha tuhuma hizo akisema, chama hicho kiliingilia kati kutafuta ufumbuzi wa
mgomo huo baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa wasafirishaji kupitia chama chao cha Akiboa.

“Sisi hatuchochei mgomo wa mabasi kama inavyodaiwa, ila tulikutana na
kujadili suala hilo na kutoa mapendekezo ngazi za juu baada ya kupokea malalamiko kutoka Akiboa,”alisema Sigamba.

Kwa upande wake Kaimu Mkuu wa Mkoa, Dk Msengi alisema ofisi yake imeanza kushughulikia
suala hilo kuhakikisha hali ya usafiri inarejea kama kawaida kuwaondolea adha wananchi wanaolazimika kutumia usafiri wa taxi na
pikipiki maarufu kama bodaboda kama njia ya kuu ya usafiri kuanzia jana.

“Hilo la Akiboa kudai tumewajibu wasioweza kulipa ushuru waegeshe magari yao nyumbani siwezi kulizungumzia kwa sababu siwezi kuingilia
fikra zao. Jambo la msingi ni kwamba Serikali ya wilaya na mkoa kwa jumla tunafanya jitihada kutatua suala hilo kwani hakuna lisilowezekana watu
wakizungumza,” alisema Dk Msengi.

Msengi akisema hayo, taarifa zaidi zinasema usafiri wa mabasi makubwa yanayofanya safari zake kutoka Arusha kwenda Mikoa ya Dares Salaam, Morogoro, Mbeya, Iringa na Tanga kupitia Moshi nayo yalitarajiwa kusitisha huduma kuanzia leo.


Mgomo ulivyoanza
Kwa mara ya kwanza, daladala za Moshi ziligoma juzi Jumamosi kabla ya mgomo huo kusitishwa baada ya wamiliki kujadiliana na uongozi
wa Manispaa na Wilaya ya Moshi, lakini ulirejea tena jana baada ya mwafaka kuhusu ushuru kupunguzwa kushindikana.


No comments:

Post a Comment