Ndugu zangu, huzuiwi kubisha au kubishana, lakini uwe na hoja za msingi zinazoshibisha kile unachokikataa. Ndivyo ilivyo hata katika mapenzi.
Ni vyema kuwa mtu wa kujifunza kila siku. Usishangae kuona ndoa ya Antony na Loveness inadumu kwa muda mrefu. Wanaishi kwa amani na maendeleo katika maisha yao yanaonekana wakati kwako moto unawaka kila siku.
Kujifunza!
Ili uwe bora na uhusiano wako uwe wenye amani siku zote, kubali kujifunza. Mwangalie mpenzi wako, yukoje? Jifunze kutoka kwake. Anapenda nini? Anachukia nini?
Ukijifunza hayo tu pekee, itakuwa hatua ya kwanza ya kuelekea kwenye kujenga uhusiano wenye amani na upendo. Angalizo moja muhimu, wakati unajifunza au upo na mpenzi wako katika uhusiano, achana kabisa na maisha ya maigizo.
Ukianza maigizo katika uhusiano wako, ni wazi kwamba hata kwenye ndoa vile vile utakuwa mtu wa maigizo tu! Unajua kati ya mambo muhimu ambayo binadamu anatakiwa kuwa nayo makini kwa kiwango cha mwisho cha uwezo wake wa kufikiria ni pamoja na ndoa.
Unapozungumzia ndoa, ujue moja kwa moja unajadili suala la maisha yako. Hapo ndipo ukomavu wa upeo wako unapoonekana. Ndoa si fasheni. Haihitaji kukurupuka...unakutana na mtu disko leo, halafu miezi mitatu baadaye unatangaza ndoa, ni vichekesho!
Kama ndoa ingekuwa ni fasheni, basi mtu angeweza kufunga ndoa na huyu leo, halafu fasheni mpya ikija anaacha na kuoana na mwingine.
Kwa bahati mbaya si hivyo. Ndoa ni maridhiano ya moyo. Unatakiwa kutulia sana wakati wa kufanya uchaguzi wa mtu wa kuingia naye kwenye ndoa. Iko hivi; kama umechagua mwenzi asiye sahihi, uwe tayari kuumia maisha yako yote. Kulia maisha yako yote. Kutokuwa na furaha maisha yako.
Nani anayependa jambo hili litokee? Bila shaka hakuna. Hii ndiyo sababu mada hii ikawepo hapa kwa ajili yako.
Yapo mambo muhimu sana ambayo watu wamekuwa wakiyapuuza kabla ya kufanya uamuzi wa kuingia kwenye ndoa. Ukishaingia ndani ya ndoa, hakuna njia ya kutoka tena, hata ikiwepo si sahihi. Inakuchafua. Inaharibu historia ya maisha yako ya uhusiano.
Uamuzi wa ndoa si wa kujaribu. Unatakiwa kujihakikishia kwamba ni kweli umevutiwa na kila kitu cha mwenzako, kwamba utakuwa naye katika shida na raha. Hayo ndiyo mambo ya kuzingatia.
Nimeshaandika mengi kuhusu sifa za anayetakiwa kuoa au kuolewa (gazeti hili na gazeti dada Risasi Mchanganyiko), lakini nasogea mbele zaidi na kuangalia sababu za kumpenda mtarajiwa wako katika ndoa.
Zipo sababu za msingi sana ambazo unatakiwa kuwa nazo kabla ya kuingia kwenye ndoa ambayo mimi hapa kwenye Let’s Talk About Love naiita kifungo!
Twende tukaone.
KWA NINI HASA?
Lazima nifafanue hili kwanza kabla ya kuendelea. Hivi unafikiri ni kwa nini ni lazima kujiuliza sababu za kumpenda mwenzi wako?
Yes! Ni kwa lengo la kujiwekea usalama katika ndoa yako ijayo. Kujiandalia amani na pumziko la kweli. Kwenye mapenzi ya dhati pekee ndipo vinapopatikana vitu nilivyovitaja hapo juu.
Kwa maneno mengine unatakiwa kuelewa kwamba, ndoa siyo maigizo. Unatakiwa kuangalia vigezo vya muhimu kabla ya kuamua kuchukua uamuzi huo.
NDIYE ULIYEMTARAJIA?
Jambo kubwa kuliko yote ambalo unatakiwa kuliangalia kwa jicho la tatu ni kama mwenzi huyo ni wa ndoto zako. Je, yukoje? Marafiki, siku zote kabla ya kuamua kufanya chochote lazima ujiulize kama ndicho ulichokuwa ukikifikiria.
Hata kwa upande wa mwenzi wako, lazima ujiridhishe. Ni kweli ni yule uliyekuwa unamtarajia? Ana sifa unazohitaji? Acha tabia ya kujifariji kwamba utampenda taratibu ndani ya ndoa, hicho kitu hakipo!
Hakuna kujifunza kupenda katika ndoa, lazima ujihakikishie mwenyewe kuwa mwenzi wako ni yule mwenye sifa ulizokuwa ukizitarajia. Hili ni la msingi, maana unaweza kuwa naye siku mbili, ukatamani mwingine nje, kwa nini? Kwa sababu si yule mwenye sifa ulizotarajia.
Umenipata? Wiki ijayo tutaendelea na vipengele vingine.
Joseph Shaluwa ni Mshauri wa Mambo ya Mapenzi anayeandikia magazeti ya Global Publishers. Ameandika vitabu vya True Love, Let’s Talk About Love na Who is Your Valentine? vilivyopo mitaani.
No comments:
Post a Comment