Banner

Banner

FOLLOW US FACEBOOK

propertyfinder.co.tz

Sunday, July 1, 2012

OFA YA SERIKALI KUMTIBIA DK ULIMBOKA INDIA YATUPWA...!

MUHIMBILI WAITING ROOM
 
Hali  ya afya ya Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari Tanzania, Dk Steven Ulimboka imeendelea kuwa siri,  huku mipango ya haraka ya kumpeleka nchini India kwa matibabu zaidi ikifanywa na madaktari wenyewe wanaodaiwa kukataa msaada wa Serikali.
Inaelezwa hisia za madaktari dhidi ya Serikali kuwa huenda ina mkono katika kutekwa na kuteswa kwa kiongozi huyo wa mgomo wa madaktari, ndizo zinazowasukuma kuizuia Serikali kushiriki katika kumpatia tiba Ulimboka ambaye kufikia leo asubuhi alikuwa anatibiwa na jopo la madaktari katika Taasisi ya Mifupa ya Muhimbili (MOI).
Kuzuiwa kwa Serikali kuchangia tiba za Ulimboka kulithibitishwa leo na Msemaji wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Nsachris Mwamaja aliyesema kuwa, Serikali ilikuwa tayari kutoa msaada wa kumsafirisha Dk Ulimboka kwenda India kwa matibabu zaidi, lakini madaktari wamegomea msaada huo wa Serikali.
Alisema wizara  hiyo ilipata taarifa kwamba Dk Ulimboka alikuwa anahitajika kupata matibabu zaidi nchini India au Nairobi, Kenya na hivyo iliamua kutoa msaada wa usafiri na matibabu kwa daktari huyo, lakini madaktari wenzake wamegoma Serikali kushiriki katika suala hilo.
Habari kutoka Muhimbili zilisema zilikuwa zinahitajika Dola za Marekani 40,000 (zaidi ya Sh milioni 60) kumwezesha Dk Ulimboka kusafirishwa nje kwa matibabu zaidi, na mwito ulitolewa kwa wahisani na wasamaria  kujitolea kusaidia mpango huo.
Na kufikia leo mchana, habari zilizonaswa zinasema madaktari na baadhi ya makundi ya watu, wamekuwa wakikamuana kuhakikisha wanapata fedha za kumsafirisha Dk Ulimboka.
Huku mgomo ukiendelea na kuwaumiza wagonjwa katika taasisi ya MOI na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, madaktari wameunda Jopo la Madaktari sita wakiongozwa na Profesa Joseph Kahamba kumtibu na kumlinda Dk Ulimboka hospitalini hapo.
Wakati mipango ya safari ikikamilishwa leo, milango ya MOI iliendelea kuwa chini ya ulinzi wa madaktari wenyewe, huku wageni wachache wakiruhusiwa kuingia ndani, huku wageni wengine wakiwemo waandishi wa habari na wapigapicha wakiagizwa kusubiri maelekezo zaidi.
Hali ya ulinzi ilionekana pia katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) huku shughuli zikionekana kusimama, ikiwa pamoja na kutoonekana kwa pilika za wauguzi na ndugu wa wagonjwa. 
Aidha, kutokana na mazingira yaliyowekwa na madaktari, ilikuwa ni vigumu kwa watu wa nje kuweza kuingia MOI ambalo Dk Ulimboka anapatiwa matibabu.
Wagonjwa waliokuwa wamekusanyika nje ya hospitali hiyo wakisubiri huduma walilaani kuendelea kwa mgomo huo huku wakiziomba pande hizo mbili zinazovutana kumaliza mgogoro uliopo ili kuwezesha huduma kurejea katika hali ya kawaida.
Wakati mgomo ukiendelea kutesa wananchi, Serikali imechukua hatua kadhaa za kunusuru maisha ya wagonjwa ikiwa pamoja na kuingia makubaliano ya kushirikiana na  hospitali binafsi kadhaa zikiwemo TMJ, Regency, Aga Khan, Hindu Mandal, CCBRT za jijini Dar es Salaam na ile ya Jeshi iliyopo Lugalo.
Alisema hatua hiyo ilifikiwa kutokana na maelekezo yaliyotolewa na Waziri Mkuu,  Mizengo Pinda, ambaye alisema Hospitali ya Lugalo ambayo ni ya Jeshi itatumika kama Hospitali ya Rufaa.
"Serikali itaelekeza nguvu zake moja kwa moja katika  Hospitali za  Mwananyamala, Amana na Temeke ambako hakuna mgomo, ili kuhakikisha kwamba hazilemewi na mzigo wa wagonjwa,” alisema.
Utafiti umebaini huduma kuendelea bila matatizo katika hospitali hizo za Amana, Temeke na Mwananyamala.

No comments:

Post a Comment