Banner

Banner

FOLLOW US FACEBOOK

propertyfinder.co.tz

Sunday, July 1, 2012

Serikali yawataka madaktari warudini kwenye meza ya mazungumzo...!



KATIKA mgogoro unaoendelea hivi sasa kati ya Serikali na madaktari, yapo mambo matano ambayo sisi hatutaki kuyaamini. Kwanza, hatutaki kuamini kwamba unyama aliofanyiwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari Tanzania, Dk Steven Ulimboka juzi ulifanywa na Serikali au washirika wake kwa lengo la kumnyamazisha na kusitisha harakati za madaktari nchini  kudai haki zao pamoja na kuboreshwa kwa mazingira ya kazi katika hospitali zetu hapa nchini.
 
Pili, hatutaki kuamini kwamba mgogoro huo unaweza kumalizwa kwa vitendo vya ubabe na vitisho, ikiwa pamoja na kudhani kwamba suluhisho la mgogoro huo ni kwenda mahakamani. Jambo la tatu ambalo hatutaki kuliamini ni kwamba mgogoro huo utatoa mshindi iwe isiwe, kwa maana ya kumpata mshindi katika mazingira hayo ya uhasama na chuki pasipo kuwapo maridhiano kati ya pande zote mbili kupitia meza ya mazungumzo.
 
Nne, hatutaki kuamini kwamba Serikali inaweza kuwa mchezaji na wakati huo ikawa mwamuzi wa mgogoro huo kutokana na ukweli kwamba nayo, kama walivyo madaktari ni sehemu ya tatizo. Kutokana na mgogoro huo kuwapo kwa muda mrefu, pande hizo mbili tayari zimejikuta katika  mazingira ya uhasama, chuki, utengano na kutoaminiana kiasi cha kutoweza kufanya mawasiliano ya moja kwa moja pasipo kuwapo kiungo kati yao cha kuwaleta pamoja.
 
Tano, hatutaki kuamini kwamba Serikali imekata tamaa kiasi cha kushawishika kutumia mabavu ya dola kuwafukuza kazi madaktari wote au viongozi wao wanaoratibu mgomo wao nchi nzima. Hii ni kwa sababu hatua hiyo itazaa balaa nchi nzima kwa sababu hatuoni mbadala wa madaktari hao wote waliogoma na kwamba kuwachukua madaktari wastaafu au wale walio katika majeshi yetu itakuwa ni kukuza tatizo, ikiwa ni pamoja na kuwafanya wauguzi na madaktari wanaofanya kazi kwa vitendo (interns) katika hospitali zetu kukasirika na kuamua kujiunga na mgomo huo.
 
Tangu mgogoro huo uanze mwishoni mwa mwaka jana, tumekuwa tukiishauri Serikali bila mafanikio kwamba itulie na ijiepushe kufanya maamuzi ya ovyo, bali ifungue milango yote ya mawasiliano kati yake na upande wa pili. Kadri mgogoro huo ulivyokua na kuchukua sura ya migomo na uhasama wa kutisha tulishauri kuwa, watafutwe wasuluhishi waadilifu wanaokubalika pande zote mbili ambao busara, weledi na uwezo wao utazijengea pande hizo mazingira ya kuaminiana ili kila upande uweze kuzungumza na mwingine.
 
Hivi ndivyo inavyofanyika sasa duniani kote. Katika kufuata kanuni  na taratibu za usuluhishi, Serikali zimeacha utamaduni wa kujihusisha na usuluhishi wa migogoro ambayo serikali hizo zinahusika kwa namna moja ama nyingine kama njia ya kupata suluhisho la kudumu la migogoro. Kama tulivyosema hapo juu, haiwezekani Serikali ambayo inatuhumiwa na madaktari ikubalike kama msuluhishi wa mgogoro ambao pia unaihusu. Ndiyo maana tunasema kukua na kushindwa kutatuliwa kwa  mgogoro huo kumesababishwa na Serikali yenyewe ambayo imekuwa kama mchezaji na mwamuzi wa mchezo kwa wakati mmoja.
 
Serikali sasa itakuwa imetambua kwamba baadhi ya watu wamelihusisha na mgogoro wa madaktari, tukio la juzi ambapo  Dk Ulimboka alifanyiwa unyama wa kutisha kwa kupigwa, kuteswa na kutupwa msituni. Bila shaka tukio hilo linafanya utatuzi wa mgogoro huo kuwa mgumu zaidi na ndiyo maana tunasema kuwa, kama Serikali inayo dhamira ya kweli ya kumaliza mgogoro huo, lazima ishirikiane na madaktari hao kupata watu waadilifu na wasiokuwa na maslahi binafsi katika mgogoro huo ili wawe wasuluhishi.
 
Wakati suala hilo likifanyiwa kazi, ni matumaini yetu kwamba Serikali itahakikisha wahusika wote waliomfanyia unyama Dk Ulimboka wanatiwa mbaroni na kushtakiwa. Ushauri wetu ni kwamba pengine Serikali ingeunda tume huru kuchunguza suala hilo badala ya kuliachia Jeshi la Polisi ambalo pia ni moja ya watuhumiwa.

No comments:

Post a Comment