Wasanii wa Bonngo Movie wakitoa misaada kwenye hospital ya Rufaa ya Bombo jijini Tanga Vicky Kimaro WASANII wa Bongo movie usiku wa kuamkia jana, walikonga nyoyo za mashabiki na wapenzi wa filamu walipoonyesha umahiri wao katika tasnia ya unenguaji jukwaani. Wasanii hao walionyesha ufundi wa kulisakata sebene kisanola linaloangushwa na bendi ya African Stars 'Twanga Pepeta'. Burudani zaidi ilikuwa kwa msanii Jacob Steven 'JB', Vicent Kigosi 'Ray' na Davina walioonyesha umahiri katika kunengua na kushangiliwa na umati wa watu uliokuwa umefurika kwenye uwanja wa Tangamano linapofanyika tamasha la filamu. Tamasha ilo limezinduliwa jana kwa kuonyesha filamu mbali mbali za msanii Steven Kanumba 'The Great' aliyefariki mapema mwezi Aprili. Filamu hizo ni Big Dady na Kijiji cha Tambua Haki. Filamu ya Big Dady ndio ilikuwa ya kwanza kuonyeshwa, wasanii waliokuwapo uwanjani hapo baadhi yao walishindwa kujizuia na kuangua kilio akiwamo Lisa, Irene Owoya, Mayasa na Catty Rupia ambaye katika filamu hiyo aliigiza kama mke wa Kanumba. Wasanii hao walishindwa kujizuia na kuamua kuondoka kwenye viwanja hivyo huku wakiwaacha wasanii wachache ambao nao walionekana kujikunyata kwa ukiwa kama Cloud, JB, Ray na Steve Nyerere ambao nao baada ya muda walianza kuondoka mmoja baada ya mwingine. Katika kumuenzi Kanumba, mratibu wa tamasha hilo, Musa Kisoki alisema wameamua kuweka mfululizo wa filamu za Kanumba katika siku ya uzinduzi ili kuenzi mchango wake katika tasnia hiyo ya filamu. Kabla ya uzinduzi huo wasanii hao walikabidhi misaada mbali mbali ikiwa ni pamoja na vyandarua 200 kwenye wodi ya akina mama na watoto katika hospitali ya Bombo mkoani Tanga. Mwenyekiti wa Bongo Movie, Jacob Steven 'JB' alisema vyandarua hivyo vina thamani ya zaidi ya Sh1.6milioni. Alisema wameamua kutoa misaada kwenye wodi hiyo ya kinamama na watoto kwa vile ndio wateja wao wakubwa wa filamu zao hivyo wameamua kurudisha shukrani zao kwa jamii kwa kuwaunga mkono. Akizungumza kwa niaba ya uongozi wa hospitali ya Bombo, Matron wa hospitali hiyo, Halima Msengi alisema amefurahishwa na kitendo cha wasanii wa Bongo movie kwa kuwakumbuka na kutoa misaada hiyo. "Tunashukuru sana kwa msaada wao, ukizingatia wajawazito na watoto ndio wapo kwenye hatari kubwa ya kupoteza maisha kutokana na ugonjwa wa malaria,"alisema Msengi. |
Banner
FOLLOW US FACEBOOK
propertyfinder.co.tz
Monday, July 2, 2012
Wasanii wa Bongo Movie wapagawisha Tanga...!
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment