Utakwenda kwa huyo unayedhani ana fedha, ukashikwa na hadaa kwamba atakupa maisha mazuri, lakini kwa vile naye si tajiri namba moja duniani, akija mwingine mwenye fedha zaidi atakung’oa. Matokeo ya jumla ni wewe kugeuka mtumwa wa wanaume wenye fedha.
Ukishaitwa mtumwa wa wanaume wenye fedha, maana yake hakutakuwa na tofauti kati yako na yule anayejiuza. Je, una amani gani kuhamahama? Dunia hii iliyojaa maradhi, ni vizuri sana ukawa mtulivu. Ukiyatendea haki mapenzi yako, ni rahisi kuwa na maisha bora.
Nakupa mfano: Shania ni binti mrembo. Urembo wake ni wa hali ya juu mno. Amesifiwa na wengi kwamba mvuto wake unatosha kumshawishi kimapenzi mwanaume yeyote yule. Sifa zilipokuwa nyingi, kichwa kikavimba, akapandisha mabega. Yeye ndiye yeye, utamueleza nini?
Akiwa A-Level, alikutana na Shadrack, wakapendana. Kila mwanafunzi akajua uhusiano wao. Wenyewe wakapeana ahadi motomoto kuwa watafika mbali, huku wakila viapo vya kufunga ndoa na kudumisha mapenzi yao bila kuachana mpaka kifo kitakapowatenganisha.
Miezi sita ya uhusiano wao, Shadrack alimuona Shania na mwanaume lakini kutokana na namna anavyomuamini, wala hakumfikiria tofauti. Wakati Shadrack hakujali chochote, Shania kwa sababu lilikuwa tukio baya, alipokutana na mwenzi wake akaanza kujikanyagakanyaga.
“Unajua yule ni rafiki wa kaka yangu, hata nyumbani kwetu huwa anakuja,” Shania alishusha utetezi bila kuulizwa. Shadrack akauliza: “Unamuongelea nani?” Alipopewa majibu akashangaa. Akasema: “Hukuwa na haja ya kunifafanulia chochote, sijahisi chochote, wewe kaa na amani kabisa.”
Haikupita muda, Shadrack akagundua kwamba Shania anatoka kimapenzi na yule jamaa aliyemkuta naye. Ilimuuma sana, kwani walikuwa wamepeana ahadi nyingi mno. Mwisho akakubali yaishe kwa sababu maisha yanaendelea bila mapenzi. Akazingatia masomo yake.
Kumbe tabia ya Shania ni kuzingatia fedha kuliko utu. Hata alipoaamua kujiweka kwa Shadrack ni kwa sababu alimuona ana unafuu wa kimaisha kuliko wanafunzi wengine wa kiume. Shadrack alikuwa anajiweza kiasi, vilevile darasani alikuwa vizuri, kwa hiyo kuwa naye akaona wanafunzi wenzake wa kike watamkoma.
Japo anajiweza lakini Shadrack alikuwa mwanafunzi, kwa hiyo hakuwa na wigo mpaka wa kipato kuweza kumhudumia Shania. Hii ikasababisha Shania ampate huyo jamaa ambaye alikuwa mfanyakazi, ofisi ya Mkuu wa Mkoa. Japo mshahara mdogo lakini aliweza kumudu kumpa huduma za hapa na pale.
Shadrack alipofika Chuo Kikuu, alipata ajira ya muda, hivyo akawa anapanga muda wa kazi na masomo. Asubuhi anakwenda kazini, jioni chuo. Kazini malipo yalikuwa si haba, hivyo kwa kipato, alimshinda yule mfanyakazi wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa. Shania kuona hivyo akarudi tena kwa Shadrack.
Mapenzi yakaendelea. Shadrack alijifanya kusahau yaliyopita lakini kila kitu kilikuwa akilini mwake. Alishajua kwamba Shania si mtu mwenye mapenzi ya kweli kwake, ila humfuata pale anapoona mambo ni mazuri. Japo alikuwa na kinyongo, safari hii Shadrack alijitahidi kuonesha mapenzi makubwa kuliko mwanzo.
Alijitahidi kumjali zaidi, akahakikisha anatimiza kila hitaji la Shania. Siku za mwanzoni Shania alijitahidi kumuonesha Shadrack mapenzi ya kweli lakini kadiri muda ulivyosogea ndivyo ilivyothibitika kuwa mja asili hasahau asili yake. Shania alianza kumtesa kihisia mwenzake, Shadrack akawa mtu wa kulalamika.
Wakati Shadrack analalamika, Shania hakujirekebisha. Akikaa na marafiki zake wanamcheka, anasimulia jinsi wakiwa chumbani Shadrack anavyomwaga machozi kwa ajili yake. Wenzake nao walishangilia, huku wakitamka waziwazi kwamba Shadrack ana tabia kama Bushoke. Eti ni mume bwege.
Kumbe Shania alikuwa na mwanaume mwingine anayeitwa Adili ambaye alimzuzua akili. Adili ni mfanyakazi wa kampuni moja ya bima, kwa hiyo kwa wakati huo alikuwa na kipato kikubwa kuliko Shadrack. Shania alisahau kila alichopanga na Shadrack, akaamua kumtesa.
Siku moja Shadrack alinasa ujumbe kutoka kwa Shania kwenda kwa Adili.
Itaendelea wiki ijayo.
No comments:
Post a Comment