Banner

Banner

FOLLOW US FACEBOOK

propertyfinder.co.tz

Thursday, October 18, 2012

HALI TETE KATIKA TAASISI ZA KIISLAMU TANZANIA

Wakati Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, Sheikh Ponda Issa Ponda, amekamatwa usiku wa juzi na Jeshi la Polisi,  kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo ya kumtishia Rais Jakaya Kikwete kuwaachia waumini wa dini ya Kiislamu waliokamatwa kwa kosa la kuchoma makanisa Mbagala, jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, alisema makosa mengine anayotuhumiwa nayo Ponda pamoja na wafuasi wake, ni kufanya uchochezi wa kidini, kuongoza vurugu za kuchoma makanisa na kusababisha uharibifu wa mali.

Sababu nyingine ni kutishia kumuua na kumng`oa madarakani Sheikh Mkuu wa Tanzania, Mufti Shaaban Issa Bin Simba, kuingilia uhuru wa mahakama na kuvamia kiwanja namba 311/3/4 Block T mali ya kampuni ya Agritanza, kilichopo eneo la Chang`ombe wilayani Temeke.

Akielezea kuhusiana na kuingilia uhuru wa mahakama, Kamanda Kova alisema kuwa juzi, Ponda alitoa kauli kwa waandishi wa habari ya kumtaka Rais wa nchi kuwaachilia huru Waislamu waliokamatwa katika vurugu za kuchoma makanisa Mbagala ndani ya siku saba,  huku akitambua kuwa suala hilo lipo mahakamani.

“Sheikh Ponda amekuwa akilifanya Jiji la Dar es Salaam kuwa na hali tete na kusababisha baadhi ya watu kupatwa na tumbo joto na hata wengine kuogopa kufika kazini kwa kuhofia vurugu zinazohamasishwa na yeye,” alisema Kova.

Aliongeza: “Jeshi la Polisi haliwezi kuvumilia kuona vurugu hizo zinaendelea, kila mtu lazima atii sheria, na yeyote atakayeonekana kuvunja atachukuliwa hatua kali.”

Kuhusiana na suala la kuvamia kiwanja, Kova alifafanua kuwa uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa kiwanja hicho kina hati miliki namba 93773,  iliyotolewa na Wizara ya Ardhi pamoja na mikataba mbalimbali ya kuuziana kati ya Bakwata na kampuni ya Agritanza.

WAVAMIZI WA KIWANJA MBARONI
Aidha, Kova alisema sambamba na kukamatwa kwa Sheikh Ponda, Jeshi la Polisi lilifanikiwa kuwaondoa wavamizi wa kiwanja hicho usiku wa Oktoba 17, mwaka huu.

Alisema watu 38 walikamatwa katika eneo la kiwanja hicho,  na kati ya hao saba ni wanawake na 31 wanaume.

Aidha, kikundi kinachosadikiwa kuwa ni wafuasi wa Sheikh Ponda, jana walijitokeza katika Kituo Kikuu cha Polisi anaposhikiliwa kiongozi huyo, na  kushinikiza kuachiwa kwake.

MABOMU YATUMIKA


Mkusanyiko wa wafuasi wa Ponda katika kituo cha polisi uliwalazimisha baadhi ya wafanyabiashara wa maeneo ya Mnazi Mmoja na Kariakoo, kufunga maduka yao kwa kuhofia vurugu za wafuasi wanaoshinikiza kuachiwa huru kiongozi huyo.

Polisi waliokuwa wameimarisha ulinzi, walitumia mabomu ya machozi kuwatawanya wafuasi hao.

Akizungumzia tukio hilo, Kova alisema Jeshi la Polisi halitamuachia kiongozi huyo kwa sababu ya shinikizo la watu, isipokuwa kwa kufuata sheria.

“Hatuwezi kumuachia mtu eti kwa sababu ya shinikizo kutoka kwa baadhi ya watu, tumechoshwa na tabia ya watu kushindwa kufuata sheria, mtu anayetaka kuishi Dar es Salaam lazima afuate sheria, bila hivyo tutamchukulia hatua,” alisema.

Aliongeza: “Sisi hatuna kisa na Sheikh Ponda, isipokuwa yeye anakabiliwa na sheria, bado anahojiwa na kama ikigundulika amevunja sheria, atachukuliwa hatua na ni vizuri kiongozi kufuata sheria na endapo ataenda kinyume, sheria itachukua mkondo wake,” alisema.

Kamanda Kova alitoa wito kwa wafuasi wa Sheikh Ponda, kujisalimisha wenyewe Polisi kabla hawajaanza kufanya msako wa kuwakamata.

ASKOFU GADI ALAANI


Mwenyekiti wa Huduma ya Good News for All Ministry, Askofu Charles Gadi, amelaani vikali kitendo cha kuchomwa makanisa.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Askofu Gadi, alisema hakukuwa na sababu ya Waislamu kuchoma makanisa kwa sababu mtoto ambaye ni chanzo cha tukio hakutumwa na mtu yeyote.

 “Sisi tunalaani kwa nguvu zote kuhusiana na kitendo cha kuchomwa makanisa kilichofanywa na baadhi ya Waislamu huko Mbagala kwa sababu hakukuwa na sababu ya msingi ya kufanya hivyo,” alisema.

Aliongeza: “Yule mtoto hakutumwa na mtu yeyote kudhalilisha Msahafu, hivyo si jambo jema kuvamia makanisa na kuyachoma.”

Aidha, Askofu Gadi alisema jambo hilo linahitaji uvumilivu na nguvu ya Mungu katika kulitatua.

UAMSHO YAITESA ZANZIBAR

Vurugu kubwa zimetokea katika mji wa Zanzibar na kusababisha uharibifu wa mali, maduka, baa, kuporwa na maskani za CCM kuchomwa moto.

Vurugu hizo zilianza baada ya kuenea kwa taarifa kuwa Kiongozi wa Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu Zanzibar, Sheikh Farid Hadi, ametoweka katika mazingira ya kutatanisha.

Wafuasi hao wa Uamsho walianza kukusanyika katika Msikiti wa Mbuyuni mtaa wa Malindi huku wakijadili taarifa za kutoweka kwa kiongozi huyo.

Wakati watu wakiendelea kukusanyika katika msikiti huo, vurugu kubwa ziliibuka katika Mtaa wa Darajani baada ya watu kuanza kurusha mawe katika maduka na kuchoma moto matairi ya magari.

Wengine walionekana wakipanga mawe na kuchoma matairi ya magari barabarani na kupanga vizuizi katika mitaa ya Mlandege, Michezani, Kijangwani, Bizeredi, Darajani na Amani Darajabovu.

Katika mtaa wa Michezani, watu waliokuwa wameficha sura zao kwa vitambaa usoni, walivamia maskani mbili za CCM ikiwemo Kisonge Maskani na Kachorora na kuzichoma moto wakiwa na silaha za kienyeji yakiwamo mapanga.

KAMISHNA WA POLISI ZANZIBAR ANENA


Kamishna wa Jeshi la Polisi Zanzibar, Mussa Ali Mussa, amekanusha taarifa za Sheikh Farid Hadi, kukamatwa na jeshi hilo usiku wa kuamkia jana mjini Zanzibar.

Alisema Polisi hawahusiki na kupotea kwa kiongozi huyo na kwamba wanaendelea kufanya uchunguzi juu ya tukio hilo.

“Jeshi la Polisi hatujamkamata Sheikh Faridi wala hatuhusiki na tukio la kutoweka kwake,” alisema Kamishna huyo.

Katibu wa Jumuiya ya Uamsho, Said Abdallah Ali, alisema hawezi kuzungumza chochote kwa vile yupo safari nje ya kisiwa cha Unguja na kutaka watafutwe viongozi waandamizi wa Uamsho.

“Nakuomba watafute viongozi wezangu watakuwa na taarifa zaidi juu ya tukio hilo, mie nipo safari kisiwani Pemba, sifahamu chochote,” alisema Sheikh Said alipozungumza na NIPASHE kwa simu jana.

Miongoni mwa waathirika wa vurugu hizo ni walimu na wanafunzi wa shule mbalimbali za sekondari ambao walikuwa wakitoka kufanya mtihani wa kidato cha nne.

Katika Kituo cha Polisi Mkunazini, kulitokea shambulio la watu waliokuwa wakirusha mawe na kusababisha askari waliokuwa kazini kutokea mlango wa nyuma kuokoa maisha yao.

MAWE YARUSHWA, MADUKA YA POMBE YAVUNJWA

Baada ya kituo hicho kupigwa mawe, watu hao walifanya jaribio la kutaka kuchoma moto pikipiki aina ya Vespa iliyokuwa nje ya kituo hicho.

Mbali na maduka ya pombe kuvunjwa na kuporwa vinywaji vikali na baridi, wananchi walikuwa katika wakati mgumu kutokana na huduma za usafiri kusimama katika Kituo Kikuu cha daladala ha Darajani.

Watumishi wa umma walilazimika kutembea kwa miguu na wengi wao kupita katika njia ambazo si rasmi huku watu wazima wakionekana kusaidiwa kwa kushikwa mikono.

“Njia ya Amani Darajabovu imefungwa kwa kutumia mawe na mbele yangu kuna moshi mkubwa, nimeshindwa kuendelea na safari yangu kwenda Mtoni,” alisema Khamis Juma, kwa njia ya simu.

Makundi ya vijana walionekana wakivunja duka moja la vinywaji la jumla karibu na Soko Kuu la Darajani na kuondoka na vinywaji.

Vurugu katika Manispaa ya Mji wa Zanzibar na uharibifu wa mali yamekuwa matukio ya kawaida tangu Jumuiya ya Uamsho kuanza kampeni za kutaka Zanzibar kujitenga katika Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Imeandikwa na Elizabeth Zaya, Enles Mbegalo, Jacqueline Yeuda, Dar na Mwinyi Sadallah, Zanzibar.

No comments:

Post a Comment