Omar
Mwamnuadzi (kati), kiongozi wa kundi la Mombasa Republican Council
(MRC) akiwasili katika kizuizi cha mahakama pamoja na wenzake.
Miongoni mwa watu hao ni mwenyekiti wa MRC Omar Khamis Mwamnuadzi, na alikamatwa katika Oparesheni ambapo watu wanne waliuawa.
Omar Mwamnuadzi ni miongoni mwa viongozi wa juu katika vugu-vugu la Mombasa Republican Council –MRC, ambalo kwa muda sasa limekuwa likipigania Pwani ijitengena kutoka Jamhuri ya Kenya.
Vyombo vya usalama mkoani pwani wanamtaja kiongozi huyo kuwa ni mtu aliyewahi kuhudumu katika jeshi la Ulinzi nchini Kenya, kati ya mwaka 1975 na 1983. Mwamnuadzi pamoja na wafuasi wake 36 akiwemo mke wake, wameshtakiwa katika mahakama moja ya Mombasa.
Mashtaka saba waliyosomewa baada ya kufika mbele ya hakimu mkuu wa Mombasa Stephen Riechi, ni pamoja na tuhuma ya uchochezi na umiliki wa silaha kinyume cha sheria.
Lakini wote walikana kuhusika ambapoo waongoza-mashtaka waliomba mahakama iwanyime dhamana, wakisema kuwa polisi wanahitaji muda zaidi wa kufanya uchunguzi.
Hatma yao itabainika baada ya majuma mawili, watakaporudishwa kortini kubaini iwapo watapeta dhamana.
Mwamnuazi na wanachama wenzake walikamatwa Jumapili usiku kwenye msako wa polisi katika boma lake, wilaya ya Kwale inayopakana na jiji la Mombasa.
Oparesheni hiyo ilisababisha makabiliano ambapo watu WANNE walifariki, akiwemo naibu-chifu wa eneo la Kombani, ambaye anasemakana kuuawa na wanachama wa MRC.
Afisa mkuu wa polisi mkoani Pwani Aggrey Adoli aliwaarifu wanahabari kwamba wanachama wa MRC waliojihami walimwuua naibu chifu katika shehemu hiyo, kuonyesha hasira pale iongozi wao alipokamatwa.
Wakuu wa polisi wanasema Wengine waliouwawa ni watu wawili, wanaosemekana walikuwa walinzi wa kiongozi huyo wa MRC, Omar Mwamnuadzi.
Tangu mapema Oktoba msako dhidi ya wafuasi wa Mombasa Republican –MRC wanaodaiwa kuhusika na uchochezi, wamekuwa wakikamatwa katika pembe tofauti za Pwani ya Kenya.
Msamaji wake Rashid Mohamed Mraja pamoja na katibu mkuu Randu Rua Nzai walishtakiwa wiki jana kwa makosa kama hayo ya uchochezi, na hadi sasa wako gerezani wakisubiri kutoka kwa dhamana.
Serikali tayari imezundua uchunguzi kuhusu wanasiasa na matajiri fulani katika eneo hilo la pwani, kwa tuhuma za kufadhili kifedha sughuli za MRC.
Mtazamo wa serikali umeibua hisia kali na tofauti, kutoka kwa raia na viongozi.
Mwezi Agosti mwaka huu mahakama kuu ya Kenya iliondoa MRC katika orodha ya makundi haramu, ambapo jaji Francis Tuiyot alishauri viogozi wa kundi hilo kutafuta usajili iwapo wanataka siasa.
Sheikh Mohammed Dor -katibu mkuu wa Baraza la Waislamu, na pia mbunge maalum, alinukuliwa na vyombo vya haabri mwishoni mwa wiki akitetea Vugu-vugu la Mombasa Republican Council.
Kama hatua inayo-onekana kama kukataa shughuli za MRC kuna kundi jipya lililochipuka PWANI NI KENYA INITIATIVE, kwa lengo la kueneza amani katika mkoa wa Pwani na kushauri wanachama wa MRC wasitishe msimamo wa kutaka kujitenga kutoka Kenya.
Wakati malumbano hayo ya maneno na pia “kamata-kamata” ya polisi inapoendelea, serikali imezindua mkutano wa kujadili hali ya usalama katika mkoa huu wa Pwani, kufuatia mauaji ya zaidi ya watu 130 katika miezi miwili iliyopita.
Mkutano huo ulioanza Jumatatu asubuhi unaongozwa na waziri wa usalama wa ndani huko Kenya Katoo Ole Metitu, na kuhudhuriwa na zaidi ya viongozi 300 kutoka majimbo tofauti ya Pwani.
Baadhi ya ajenda ni vuguvugu la MRC lililochipuka huko Pwani ya Kenya, na vitisho vya kuvuruga usala wa taifa.
Chanzo: www.voaswahili.com
No comments:
Post a Comment