Jeshi la
Polisi Wilaya ya Temeke jijini Dar es Salaam limekumbwa na kashfa baada
ya askari wake mmoja kudaiwa kushiriki kumpa kipigo fundi magari mkazi
wa Temeke Mikorosheni, Gaspa Mlay, hivyo kusababisha kifo chake na kisha
mwili wake kutelekezwa nyuma ya kituo cha polisi. Tukio
hilo lilitokea Jumamosi wiki iliyopita baada ya askari mmoja (jina
tunalo), wa kituo kidogo cha polisi cha Sandali kwa kushirikiana na
mmiliki wa nyumba aliyokuwa amepanga marehemu (Gaspa) kumshambulia kwa
kipigo na kusababisha kifo.
Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Temeke, Engelbert Kiondo, amethibitisha kutokea kwa
tukio hilo, hata hivyo, amekana kuwa askari wake ameshiriki katika
mauaji hayo.
“Nasita kufanya kazi na nyie kupitia kwenye simu, tukio lenyewe
limetokea tangu Jumamosi, na muda huu sipo ofisini, lakini kimsingi siyo
kweli kwamba kuna askari ameshiriki katika mauaji hayo, njoo kesho
(leo), nitakueleza tukio lilivyo na OCCID (Mkuu wa Upelelezi wa Kituo)
atakuwapo,” alisema Kiondo.
Hata hivyo, akizungumza na NIPASHE jana akiwa katika Hospitali ya Wilaya
ya Temeke ambako mwili wa marehemu umehifadhiwa, mjomba wa marehemu,
Peter Masoyi, alisema Gaspa ambaye sasa ni marehemu alipewa notisi na
mwenye nyumba kutakiwa kuhama katika nyumba aliyopanga eneo la Temeke
Mikorosheni.
Alisema bahati mbaya kwa takribani mwezi mmoja marehemu (Gaspa),
hakufanikiwa kupata nyumba nyingine ya kupanga na hivyo aliendelea
kuishi katika nyumba aliyokuwa amepewa notisi ya kuhama.
Masoyi alisema kitendo cha Gaspa kuendelea kuishi katika nyumba hiyo
kilimuudhi mwenye nyumba ambaye aliamua kuchukua umuazi wa kwenda kutoa
taarifa katika kituo cha polisi cha Sandali kuomba msaada ili aondolewe
kwa nguvu kutoka katika nyumba hiyo.
Baadaye polisi mmoja wa kituo hicho, mwenye nyumba na mjumbe wa mtaa
walikwenda katika nyumbani aliyokuwa anaishi Gaspa na kumgongea mlango
katika chumba alichokuwa amelala, lakini aligoma kufungua mlango.
Alisema baadaye askari huyo na mjumbe waliamua kuvunja kitasa na kufuli
la mlango huo na kuingia ndani kwa lengo la kumtoa kwa nguvu Gaspa
kutoka katika chumba alichokuwa amelala na kutokea vurugu kubwa
zilizosababisha Gaspa kupigwa na kujeruhiwa vibaya na kusababisha
ashindwe kutembea.
Baada ya tukio hilo, polisi na mjumbe huyo walikodi pikipiki na
kumpeleka Gaspa kituoni na baadaye walimfuata mdogo wake Gaspa aitwaye
Elias Mlay anayefanya kazi gereji eneo la Temeke Sterio kumweleza kuwa
ndugu yake amesababisha uharibifu kwa kuvunja mlango wa nyumba ya watu.
Aliongeza kuwa askari hao walimweleza Elias kuwa kama anataka ndugu yake aachiwe huru kutoka kituoni hapo atoe Sh. 300,000.
Hata hivyo, Elias kabla ya kukubali kutoa kiasi hicho cha fedha,
alimweleza askari huyo kwamba akajionee uharibifu aliofanya ndugu yake
na baada ya kufika eneo la tukio, alikuta kilichoharibiwa ni kitasa na
kufuli na hivyo kugoma kutoa fedha hizo badala yake akamweleza kuwa yupo
tayari kutoa Sh. 20,000.
Askari huyo alikubali kupokea Sh. 20,000 kwa makubaliano kuwa atamuachia
Gaspa huru, lakini wakati anakwenda kufanya kazi hiyo, alimweleza Elias
kuwa asiambatana naye kwenda kituoni badala yake ikifika mchana ampigie
simu kuuliza kama atakuwa ameachiwa.
Masoyi alisema ilipofika saa 7:00 mchana, Elias alipompigia simu askari
huyo kufahamu kama amemwachia ndugu yake alijibiwa kuwa ameshafariki
dunia na mwili wake upo kituoni hapo.
“Eliasi alivyoelezwa hivyo hakuamini badala yake alikwenda mwenye
kituoni na baada ya kufika alikuta kweli ndugu yake ameshafariki (dunia)
na mwili wake umewekwa nyuma ya kituo cha polisi huku ukiwa umevimba
tumbo,” alisema Masoyi.
Alisema baadaye Elias alikwenda kutoa taarifa kituo kikubwa cha polisi
Chang’ombe na polisi wa kituo hicho walifika eneo la tukio na kuchukua
mwili wa marehemu kuupeleka Hospitali ya Wilaya ya Temeke na baadaye
walimkamata mwenye nyumba alikokuwa akiishi Gaspa siku ya Jumamosi
jioni.
Hata hivyo, ndugu wa marehemu Gaspa walianza kuhoji kwanini askari
anayedaiwa kushiriki katika tukio hajakamatwa, lakini walijibiwa na
askari waliokuwa wakifuatilia suala hilo kwamba kama wana ushahidi na
jambo hilo watoe ushahidi na askari huyo atakamatwa.
Jumanne wiki hii ndugu wa marehemu walipokwenda Hospitali ya Wilaya ya
Temeke, walielezwa na askari waliokuwa wakifuatilia suala hilo kuwa
mwili wa marehemu unatakiwa kwenda kufanyiwa uchunguzi katika Hospitali
ya Taifa ya Muhimbili, lakini itashindikana kwenda huko sababu gari la
polisi halina mafuta.
Majibu hayo hayakuwafurahisha ndugu za marehemu ambao waliamua kwenda
kumwona Kamanda Kiondo ambaye baada ya kuwaita askari wa kituo hicho
walimweleza kuwa askari anayetuhumiwa amekamatwa na walipoomba waende
kumtambua walikuta ndiyo anahojiwa muda huo kituoni.
SOURCE: NIPASHE
No comments:
Post a Comment