Banner

Banner

FOLLOW US FACEBOOK

propertyfinder.co.tz

Sunday, May 12, 2013

HADITHI: MWANDISHI AMERUDI (A Journalist is Back) Sehemu ya TATU...

MWANDISHI: NYEMO CHILONGANI.
SIMU: 0718 069 269
Anapoishi: DAR ES SALAAM.
Sehemu ya TATU ..
 
Kama ulikosa kusoma hadithi hii kwenye sehemu ya kwanza bofya hapa http://kingjofa.blogspot.com/2013/05/hadithi-mwandishi-amerudi-journalist-is.html#.UYZcslbXjIU

Kama ulikosa kusoma hadithi hii kwenye sehemu ya pili bofya hapa
http://www.kingjofa.blogspot.com/2013/05/hadithi-mwandishi-amerudi-journalist-is_5.html#.UY-VyVbXjIU 

Ilipoishia...,
“Sawa. Uko wapi ili nije kuichukua habari hiyo?”
“Njoo hapa New Africa Hoteli”
“Nitakuwa hapo baada ya dakika ishirini” Dominick alisema na kukata simu.

  Mlio wa risasi ukasikika, mwanaume yule aliyekuwa chini alisikika akipiga kelele za maumivu. Tayari mzee Mrisho aliona hakukuwa na amani mahali pale, alijiona kuwa na nafasi ya kufanya chochote ili aokoe maisha ya mwanaume yule.
   Wanaume wale watatu walibaki wakicheka hali iliyoonyesha kwamba walikuwa wakiyafurahia maumivu ya mwanaume yule aliyekuwa akilia. Mwanaume yule ambaye alimpiga risasi mwanaume yule aliyekuwa chini, akamuelekezea tena bunduki tayari kwa kumpiga risasi nyingine.
   Mzee Mrisho akajikuta akichukua mgobole wake na kumwelekezea mwanaume yule aliyekuwa ameshika bunduki. Hakutaka kuchelewa, hapo hapo akamfyatulia risasi ya kichwa, mwanaume yule akaanguka chini kama mzigo wa viazi.
   Hata kabla wale wenzake hawakujua wafanye nini, wakashtukia wakipigwa risasi za vifuani, damu zikatapakaa mahali pale. Wote wakaanguka chini ambako wakaanza kurusha mikono na miguu yao, baada ya muda, wakatulia hali iliyoonyesha  tayari walikuwa wamekufa.
   Mzee Mrisho akachomoka kutoka kichakani na kumfuata mwanaume yule aliyekuwa akilia kwa maumivu makali, akambeba na kuanza kuondoka nae pasipo kuongea nae kitu chochote kile. Safari ya kurudi nyumbani ikaanza, ilikuwa safari ndefu huku mwanaume yule akiwa mgongoni mwake.
   Alitumia masaa mawili, akawa amekwishafika nyumbani huku ikiwa saa tisa usiku. Mkewe akamfungulia mlango, mshangao mkubwa ukampata, hakuelewa ni kitu gani ambacho kilikuwa kinaendelea mpaka mumewe kurudi na mtu ambaye alionekana kuwa kama maiti.
   “Kuna nini tena mume wangu?” Bi Sikujua aliuliza.
   “Bandika maji jikoni kwanza” Mzee Mrisho alimwambia mkewe.
   Pasipo kuuliza kitu chochote kile, Bi Sikujua akaelekea jikoni ambako akabandika sufuria iliyokuwa na maji na kisha kurudi sebuleni ambako mzee Mrisho akaanza kumuelezea kila kitu kilichotokea.
   “Kwa hiyo haumfahamu kabisa?”
   “Ndio. Niliamua kumsaidia, niliona akiwa katika hali ya hatari” Mzee Mrisho alimwambia mkewe.
   Maji yalipochemka, yakaletwa na mzee Mrisho kuanza kufanya kazi ya kuiondoa risasi katika mguu wa mwanaume yule. Kilio kikubwa kilisikika lakini mzee Mrisho hakuonekana kujali, aliendelea na kazi ile mpaka risasi ilipotoka na kisha kumfunga bandeji.
   “Asubuhi ikifika, tutaelekea hospitalini kumnunulia dawa” Mzee Mrisho alimwambia mkewe, Bi Sikujua.
   “Kwa nini tusimpeleke hospitalini tu?”
   “Hapana. Maisha yake bado nayaona kuwa katika hatari” Mzee Mrisho alimwambia mkewe.
                                                             ************
   Maisha yaliendelea mbele, Dominick hakuruhusiwa kutoka nje, kila siku maisha yake yalikuwa ndani ya nyumba ya mzee Mrisho. Kila kitu alikuwa akikipata ndani ya nyumba ya mzee Mrisho, maisha yake hayauonekana kuwa na amani nje ya nyumba hiyo.
   Kitu alichokuwa akikifahamu ni kwamba kila siku angekuwa akitafutwa kwa lengo moja tu la kuuawa. Hakuamini kama watu ambao waliwatuma vijana wale wangeridhika kama wangepeta taarifa kuwa mtu ambaye alitakiwa kuuawa hakuuawa kama ilivyotakiwa iwe.
   Dominick akajiona kuingia katika vita, vita ambayo alitakiwa kuimaliza kwa mikono yake mwenyewe. Kila siku maombi yake yalikuwa juu ya kumfahamu mtu au watu ambao walikuwa nyuma ya mpango wa kuuawa kwake.
   Kila siku Dominick alikuwa akiyafikiria maneno yale ya BoT ambayo yalikuwa yameandikwa nje ya geti lake katika siku ambayo nyumba yake ilichomwa moto na familia yake yote kuangamia. Maneno yale yalieleweka vizuri na hata makao makuu ya idara ile alipafahamu vilivyo.
   Kitu alichokijua ni kwamba hakukuwa na mtu yeyote kutoka katika idara ile ambaye alihusika kutokana na yule mtu aliyefanya ufisadi kuuawa kwa kulegezewa breki ya gari lake alipokuwa akielekea Dodoma. Bado Dominick alionekana kuchanganyikiwa, hakuelewa kabisa mtu ambaye alikuwa nyuma ya tukio hilo.
   Kila siku alitamani kuwasiliana na marafiki zake ili kuwapa taarifa juu ya uwepo wake katika nyumba ya mzee Mrisho lakini kila alipotaka kufanya hivyo, alisita kwa kuogopa kujulikana kuwa yuko hai.
   Kila siku alikuwa mtu wa kulala ndani, hakutakiwa kutoka nje wala hakutakiwa mtu yeyote kufahamu kuwa yuko ndani ya nyumba ile.
   Mpaka taarifa za kifo chake zilipokuwa zinatangazwa, yeye mwenyewe alikuwa akiangalia katika televisheni. Dominick alibaki akifurahia kwani alijua kuanzia kipindi hicho asingeweza kupata usumbufu wowote ule.
   Siku ziliendelea kukatika mpaka mwezi mmoja kupita, bado Dominick alikuwa akishinda ndani. Hakutakiwa kutoka kabisa nje ya nyumba hiyo, na kama alitaka kutoka, basi kitendo hicho kilitakiwa kufanyika usiku, muda ambao hakukuwa na watu wengi mtaani.
   Hayo ndio maisha ambayo Dominick alikuwa akiishi. Kila kitu ambacho kilikuwa kinaendelea, alikuwa akipata taarifa kupitia televisheni na magazeti ambayo mzee Mrisho alikuwa akiyaleta.
   “Kila mtu anajua kuwa uliuawa, hakuna mtu ambaye anajua kama uko hai” Mzee Mrisho alimwambia Dominick.
   “Kwa hiyo wanachofahamu kuwa kwa sasa nipo kaburini?”
   “Ndio. Tena umeoza kabisa” Mzee Mrisho alimwambia Dominick.
   Dominick hakutaka kuendelea kukaa sebuleni hapo, moja kwa moja akainuka na kuaelekea chumbani. Mzee Mrisho alibaki sebuleni pale akiangalia televisheni. Dakika ziliendelea kukatika, mzee Mrisho hakutaka kwenda chumbani mpaka muda wa taarifa ya habari utimie, aliendelea kusubiri zaidi na zaidi.
   Huku akiendelea kuwa sebuleni hapo, mara umeme ukakatika na giza kutawala mahali hapo. Mzee Mrisho akaonekana kukasirika, akainuka kutoka pale alipokaa na kuelekea kule ilipokuwa soketi ya umeme na kuizima.
   Hata kabla hajapiga hatua kuelekea chumbani, mara akasikia mlango ukigongwa. Mzee Mrisho hakuonekana kuwa na wasiwasi, akaanza kupiga hatua kuufuata mlango na kuufungua.
   Mzee Mrisho akashtuka kupita kawaida, mdomo wa bunduki ulikuwa umeelekezewa usoni mwake na mtu ambaye hakuweza kumhamu kutokana na giza lililokuwa mahali pale. Hata kabla mzee Mrisho hajaamua ni kitu gani alitakiwa kufanya, akaamriwa kuingia ndani.
   “Jamani, kuna nini tena?” Mzee Mrisho aliuliza huku akionekana kuwa na hofu.
   “Tutakachohitaji, tutataka kupatiwa. Na kama hatutopatiwa, milio ya risasi itakwenda kusikika mahali hapa” Mwanaume yule alimwambia mzee Mrisho huku wenzake wawili wakiwa wamekwishaingia ndani ya nyumba ile.
   “Mnataka nini? Mnataka nini jamani?” Mzee Mrisho aliuliza huku hofu ikizidi kuongezeka.
   Hata kabla mwanaume yule hajajibu chochote juu ya kile walichokuwa wakikitaka, Bi Sikujua akatokea sebueni pale. Akaamriwa anyamaze kimya, sauti yoyote kutoka kwake isisikike. Mwanaume mmoja alimsogelea na kumvuta katika upande aliokuwa mzee Mrisho.
   “Tunamuhitaji mtu wetu” Mwanaume yule alimwambia mzee Mrisho
   “Mtu gani jamani? Mbona mnanichanganya” Mzee Mrisho aliuliza.
   “Unakumbuka nilichokuambia? Unakumbuka nilikwambia nini nilipoingia hapa?” Mwanaume yule aliuliza huku sauti yake ikisikika kama mtu aliyekasirika.
   “Ndio. Ninakumbuka”
   “Basi tunamuhitaji mtu wetu, hatuna muda mwingi wa kukaa mahali hapa” Mwanaume yule alimwambia mzee Mrisho.
   “Jamani, mtu gani ambaye mnataka mimi niwape?” Mzee Mrisho aliuliza huku hofu ikiongezeka kadri muda ulivyozidi kwenda mbele.
   “Tunamuhitaji mwandishi wa habari. Mwandishi yule mbeya” Mwanaume yule alimwambia.
   “Mwandishi gani jamani?”
   Yule mwanaume hakuongea kitu, mpaka muda huo tayari aliona kama anafanyiwa mzaha, akaivuta bunduki yake kwake na kuikoki hali iliyoonyesha alikuwa tayari kumfyatulia risasi mzee Mrisho. Bi Sikujua alikuwa akilia tu, hakuamini kama muda huo walikuwa wamewekwa chini ya ulinzi na watu ambao walionekana hatari, watu waliokuwa wameshika bunduki.
   “Moja... niambie. Mbili.... niambie. Ta...”
   “Subiri baba. Mimi nitakwambia ukweli” Bi Sikujua alimwambia.
   “Ukweli gani?”
   “Juu ya huyo mnayemtafuta”
   “Tuambie yuko wapi?”
   “Chumbani. Yuko chumbani. Naomba mmuache mume wangu” Bi Sikujua alimwambia.
   “Chumba gani?”
   “Chumba cha tatu koridoni upande wa kushoto” Bi Sikujua aliwaambia.
   “Una bahati sana, mkeo ameokoa maisha yako” Mwanaume yule alimwambia mzee Mrisho.
   Hawakutaka kupoteza muda, wote wakaanza kuelekea katika korido ile na kisha kuanza kuufuata mlango wa chumba kila. Walipoufikia, wakajaribu kuufungua, mlango ulikuwa mgumu hali iliyoonyesha kuwa ulifungwa kwa ndani. Wakaanza kuugonga kifujo fujo lakini mlango wala haukufunguka.
   “Tuuvunjeni” Mwanaume yule aliyeonekana kuwa kiongozi aliwaambia wenzake na hatua za kuuvunja mlango kuanza.
   Ni ndani ya dakika moja tu, mlango ukavunjika. Wakawasha tochi ambazo walikuja nazo mahali hapo na kuanza kumulika ndani ya kile chumba alichokuwa Dominick.
“Yule pale kitandani”  Mwanaume mwingine aliwaambia wenzake na wote kuanza kumfuata Domonick kitandani huku bunduki zao zikiwa tayari.
                                                               ***********
  Kikao cha dharura kilikuwa kinaendelea  kufanyika ndani ya chumba kimoja ambacho kilikuwa miongoni mwa vyumba vizuri vilivyokuwa katika nyumba ambayo ilikuwa ikiheshimiwa sana, nyumba ya kifahari iliyojengwa katika mtaa wa kifahari wa Osterbay.
Watu watatu ambao walikuwa wazee wa makamo ndio ambao walikuwa wamejikusanya ndani ya chumba hicho. Bado ajenda ambayo walikuwa wakiizungumzia katika kipindi hicho haikupatiwa muafaka kabisa. Kwa wakati huo, kila mmoja alionekana kuchanganyikiwa.
Dada waliyemtuma katika kufanya kazi ya kumuita Dominick katika hoteli ya New Africa alifanya kazi kama vile ilivyotakiwa kufanywa. Wasiwasi wao bado ulikuwa juu ya vijana wale ambao waliondoka na Dominick kuelekea katika msitu wa Nyakipande.
Bado hawakupata taarifa yoyote juu ya kilichoendelea msituni. Mara kwa mara walikuwa wakijaribu kuwapigia simu, simu hazikuwa zikipokelewa zaidi ya kuita mpaka kuzima. Mambo haya yote yakaonekana kuwatia wasiwasi.
Kikao kikaendelea zaidi na zaidi hadi kufikia muafaka wa kuwatafuta vijana wengine ambao wangeanza kufuatilia ni kitu gani ambacho kilikuwa kimetokea msituni. Kutokana na usiku kuwa umekwenda sana, wakaahirisha kikao ambacho kilitarajiwa kufanyika tena kesho.
Siku iliyofuata vijana watatu wakatafutwa na kupewa mavazi ya kipolisi pamoja na kuwa na mbwa mmoja ambaye angetumika katika kunusa nusa ndani ya msitu ule. Safari ya kuelekea katika msitu wa Nyakipande ikaanza mara moja.
Mara baada ya vijana wale kuingia msituni wakaanza kuwatafuta watu wale ambao walikuwa wametumwa kuifanya kazi waliyopewa jana usiku. Walitembea sana msituni huku wakiongozana na mbwa ambaye alikuwa makini kunusa katika kila njia.
   Hakukuwa na dalili zozote za kuwapata vijana wale kitu ambacho kiliwapelekea kumfuata mbwa kila sehemu alipotaka waelekee. Mbwa aliendelea kunusa ardhini huku akipita katika kila njia ambazo aliziona kuwa sahihi kwake. Ni ndani ya dakika tano tu, wakafika katika eneo ambalo lilikuwa na nyasi fupifupi.
Wote wakaanza kuangalia katika eneo hilo, miili ya watu watatu iliyokuwa na michirizi ya damu ilikuwa ikionekana vizuri machoni mwao. Kwa haraka wakapiga simu kwa wazee wale ambao walikuwa wamewatuma na kuwapa taarifa juu ya kile walichokuwa wamekiona.
“Kama ni hivyo, basi rudini” Sauti ya mzee mmoja iliskika.
“Turudi pamoja nayo?”
“Nini?”
“Hii miili”
“Hapana. Iacheni, hatuna kazi nayo”
“Sawa mkuu”
“Kuna bunduki walizokuwa wanazitumia mahali hapo?”
“Ndio”
“Hizo njooni nazo”
“Sawa” Kijana yule alijibu na kisha kukata simu.
Wazee walionekana kuchanganyikiwa, kitendo cha vijana wao kupigwa risasi na kisha Dominick kutoweka kilionekana kuwachanganya zaidi. Kila wakati walikuwa wakijiuliza ni kwa jinsi gani Dominick aliweza kupambana na vijana wao watatu waliokuwa na bunduki na kuwashinda nguvu.
Walichokifanya baada ya vijana wao kurudi ni kuwapa kazi ambayo vijana wale wengine walishindwa kuifanya. Dominick hakutakiwa kuwa hai tena, tayari alionekana kuwa hatari katika maisha yao kama tu wangemwacha aendelee kuvuta pumzi ya dunia hii.
 Wakawatuma mitaani kuhakikisha Dominick anapatikana na kuuawa. Miezi miwili ilipita na ndipo taarifa za Dominick kufa zikaanza kutapakaa. Wazee wa hawakutaka kukubali kabisa. Ukweli waliujua kwamba Dominick hakuwa amekufa kama ilivyotangazwa, alikuwa hai akiwa amejificha sehemu fulani.
“Mtafuteni katika kila sehemu, ila Mbezi ndio muitolee macho sana” Mzee mmoja aliwaambia vijana wale.
“Sawa mkuu”
Dominick akaanza kutafutwa katika maeneo mengi ya Mbezi. Kazi haikuwa nyepesi hata kidogo, katika kila kona ambayo walikuwa wakifika, Dominick hakuwa akionekana kabisa. Siku ziliendelea kukatika lakini bado Dominick alionekana kuwa adimu kupatikana.
“Kuna tetesi zinasikika kuwa kuna nyumba ina mgeni ambaye hutoka nje usiku sana” Mmoja wa vijana wale waliotumwa na wazee wale, Pius aliwaambia wenzake.
“Nyumba gani?”
“Bado sijaifahamu, ila inatubidi tuendelee kuchunguza”
Uchunguzi wa kuigundua nyumba hiyo ukaanza mara moja, mara kwa mara walikuwa wakiwaaita vijana mbalimbali na kuwauliza swali juu ya nyumba hiyo.
“Hata mimi nimesikia. Ila si unajua umbea, kwanza mtu atakaaje na mtu pasipo kumtoa nje. Huo uzushi” Kijana mmoja alimwambia Pius.
“Kwani nyumba yenyewe ipi?”
“Kwani wewe mgeni maeneo haya? Hata nyumbani kwa mzee Mrisho haupafahamu?” Kijana yule alimuuliza Pius huku akionekana kumshangaa.
“Simjui yeyote huku. Bado mimi ni mgeni, nakaa hapo mtaa wa nyuma. Unamjua mzee Ally Mangushi?” Pius alisema na kuuliza swali.
“Yule mzee mfupi mwenye upara?”
“Ndio. Nyumbani kwake ndipo nilipopanga” Pius alimwambia kijana yule.
Pius hakutaka kuacha kuzungumza na kijana yule, muda wote alikuwa akiongea nae kama njia mojawapo ya kutafuta mazoea. Kijana yule akaonekana kumzoea Pius kana kwamba alikuwa rafiki yake wa muda mrefu.
“Ulisema nyumba ipi?”
“Kwa mzee Mrisho. Mzee mwindaji. Subiri akipita nitakuonyeshea”
“Hapana. Usifanye hivyo, kwani nyumba yenyewe iko wapi?”
“Kule mbele, nyumba yenye bucha kwa nje”
“Nimekwishaikumbuka. Kumbe pale ndipo anapokaa?”
“Ndio hapo hapo”
Pius hakutaka kuendelea kukaa mahali hapo, tayari alikwishaonekana kupata kile ambacho alikuwa akitaka ukipata kwa wakati huo. Moja kwa moja akaanza kuwasiliana na wazee ambao walikuwa wamemtuma na kuwapa taarifa juu ya kile kinachoendelea kwa wakati huo.
“Msimcheleweshe. Mkimpata muueni”
“Sawa. Ila hamtaki hata kiungo kimoja kutoka mwilini mwake?”
“Kama itawezekan, tuleteeni kichwa”
Mipango ikaanza kufanyika usiku huo. Pius akawaita wenzake na kuwaambia kila kitu ambacho kilikuwa kinaendelea. Hawakutaka kupoteza muda, walitaka kumtia mikononi Dominick hata kabla siku nyingine haijafika.
Wakapanga mpango mzima na hatimae wazo la kuzima umeme wa nyumba ile kupewa kipaumbele. Walitaka kuzima kwanza umeme wa nyumba ile kutoka katika chuma la umeme la nyumba ile kwa kutoruhusu umeme kuingia ndani na kisha ndipo wavamie.
“Hilo wazo zuri sana. Tufanyeni hivyo hivyo” Kimbetu alimwambia Pius.
Usiku ulipoingia, kazi ikaanza mara moja Wakaelekea katika duka la vifaa mbalimbali na kununua plaizi kwa ajili ya kukata waya wa umeme ambao ulikuwa ukipitisha umeme katika nyumba ya mzee Mrisho. Mara walipopata kila kitu walichokuwa wakikihitaji, wakajiandaa na kazi.

****************************
JE NI NINI KITAENDELEA ?
USIKOSE KUSOMA MUENDELEZO WA HADITHI HII.

No comments:

Post a Comment