TAREHE
9 Mei 2013, Mhe. Dkt. Hussein A. Mwinyi (Mb) Waziri wa Afya na Ustawi
wa Jamii, katika kuhitimisha hoja ya bajeti ya Wizara alitolea ufafanuzi
suala la dawa bandia ya ARV kufuatia hoja zilizokuwa zimetolewa na Mhe.
Zarina S. Madabida (Mb) kuhusu kuhusika kwa kiwanda cha dawa
chaTanzania Pharmaceutical Industries Ltd (TPI) katika sakata la dawa
bandia za ARV.
Baada
ya ufafanuzi huo wa Mhe. Waziri kutolewa, kumekuwa na taarifa
mbalimbali kupitia vyombo vya habari zinazoleta mkanganyiko kwa wananchi
kuhusu suala hili.
Ili kuondoa mkanganyiko ambao umeanza kujitokeza, Wizara inapenda kutoa
ufafanuzi kuhusu tamko lililotolewa na Mhe. Waziri wa Afya na Ustawi wa
Jamii.
Aidha, kama ilivyoelezwa katika taarifa mbalimbali za umma zilizokwisha
kutolewa na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii pamoja na TFDA kuhusiana
na suala hili, bado inasisitizwa kwamba kampuni ya TPI Ltd iliiuzia
Bohari ya Dawa (MSD) dawa bandia aina ya TT-VIR 30 toleo Na. 0C.01.85,
kwa mujibu wa nyaraka zilizopo.
Tunapenda kusisitiza kwamba, Mhe. Waziri katika hotuba yake hakukanusha
kuwa kampuni ya TPI Ltd iliiuzia MSD dawa bandia bali alieleza kwamba
uchunguzi wa awali katika kiwanda cha kampuni hiyo haukuonesha dawa hiyo
ilizalishwa na TPI Ltd bali vifungashio ni vya TPI Ltd na nyaraka
zinaonesha TPI Ltd kuiuzia MSD dawa hizo bandia.
Aidha, alieleza kuwa vyombo vya usalama bado vinaendelea kulichunguza
suala hilo ili kubaini chanzo na wahusika wakuu wa dawa hizo bandia.
Kwa kuzingatia unyeti wa suala hili, Wizara inatoa wito kwa vyombo vya
habari kusubiri hatma ya uchunguzi unaofanywa na vyombo vya usalama na
kuepuka kutoa taarifa ambazo zinaweza kupotosha umma na jitihada kubwa
za Serikali katika kupambana na dawa bandia nchini.
Imetolewa na:
N. Mwamwaja
MSEMAJI
16 Mei 2013
No comments:
Post a Comment