Banner

Banner

FOLLOW US FACEBOOK

propertyfinder.co.tz

Sunday, May 12, 2013

ZITTO KABWE AHOJIWA NA KIKOSI KAZI KILICHOUNDWA NA SERIKALI KUHUSU MABILIONI YALIYOFICHWA USWISI

MBUNGE wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (CHADEMA), jana alihojiwa na Kikosi Kazi kilichoundwa na serikali kwa ajili ya kupata taarifa kuhusu vigogo walioficha mabilioni ya fedha kwenye akaunti za nje ya nchi ikiwemo Uswisi.

Kuitwa kwa Zitto ambaye pia ni Naibu Katibu mkuu wa CHADEMA, kunatokana na kuwa mwanzilishi wa hoja hiyo bungeni Novemba mwaka jana, huku akieleza kuwa na orodha ya majina ya vigogo hao wanaodaiwa kuficha mabilioni nje ya nchi.

Akizungumza na Tanzania Daima jana mchana katika ofisi za Bunge mjini hapa muda mfupi kabla ya kuingia kwenye mahojiano na Kikosi Kazi hicho, Zitto alisema kuwa si kwamba wanahojiwa bali wanashirikiana ili kutoa taarifa walizonazo ziweze kusaidia upatikanaji wa ukweli kuhusu jambo hilo.

Zitto alisema kuwa baadhi ya wabunge wameombwa na kamati ya kikosi kazi hicho kinachoongozwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Fredrick Werema, ili kuwasilisha taarifa walizonazo.

“Ni jambo la kawaida na si kwamba tunahojiwa kama watuhumiwa bali ni kujaribu kusaidia upatikanaji wa taarifa muhimu. Wako baadhi ya wabunge wameombwa; si mimi peke yangu,” alisema.

Tanzania Daima, ilipomtaka kuwataja wabunge wengine walioitwa, Zitto alisema, “Mimi namjua Kangi Lugola wa Mwibara(CCM) japo wapo na wengine.”

Jaji Werema hakuweza kupatikana ili kutaja idadi ya wabunge walioitwa na kikosi chake pamoja na wajumbe anaounda kikosi kazi hicho, kwani hata Zitto alipoulizwa kuhusu wajumbe wengine wa kikosi kazi hicho, alisema hajui.

Tanzania Daima ilishindwa kuthibitisha kama Lugola alikuwa amehojiwa au la, kwani alipotafutwa kufafanua juu ya hilo, simu yake iliita bila kupokelewa.

Itakumbukwa kuwa chimbuko la sakata hilo ni Zitto ambaye aliwasilisha bungeni hoja binafsi Novemba 9 mwaka jana, akilitaka Bunge kuchunguza na kuielekeza serikali hatua dhidi ya raia wa Tanzania walioficha fedha na mali haramu nje ya nchi.

Hata hivyo, hoja yake iliyokuwa na maazimio saba ya kufanikisha fedha hizo kurejeshwa iliporwa na serikali na kuyabadili maazimio hayo.

Kitendo cha serikali kubadili maazimio takriban matano kati ya saba, kilizua ubishani mkali wa kutofikia muafaka baina ya mtoa hoja, wabunge na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Werema, ambaye alipendekeza mabadiliko hayo.

Miongoni mwa mapendekezo yaliyozua mvutano katika hoja hiyo ni pamoja na pendekezo lililotaka serikali ishirikiane na Benki ya Dunia kupitia kitengo cha Assets Recovery.

Katika marekebisho yake, Werema alitaka pendekezo hilo lifutwe kwa madai kuwa jambo hilo linafanywa na vyombo vya uchunguzi vya ndani.

Pendekezo la pili ambalo lilipingwa na Werema ni kuhusu viongozi wa umma kuwa na akaunti katika benki za nje kwa madai kuwa suala hilo linahusu benki za nje, na ipo sheria ya fedha za kigeni inayoshughulikia.

Pendekezo la tatu ni kutangaza akaunti za watu wenye fedha nje ya nchi katika vyombo vya habari, ambapo Werema alisema kipengele hicho kiondolewe kwa sababu kinavunja usiri wa benki mbalimbali.

Pendekezo la nne ambalo linataka Watanzania waeleze wamezipataje fedha hizo pia alitaka liondolewe kwa sababu vipo vyombo vinavyohusika na uchunguzi kama Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) na kile cha Intelligence Union Unit.

Mbali na hayo, Werema alipendekeza suala la Meremeta lipelekwe kwenye Kamati ya Ulinzi na Usalama kwa sababu linahitaji hoja mahususi na kwamba anakubaliana na Zitto kwamba serikali haiwezi kujivua nguo.

“Mimi sikubaliani na mapendekezo ya Mwanasheria Mkuu, mapendekezo haya anayotaka yafutwe ndiyo msingi wa hoja yenyewe, kuyafuta ni kuifuta hoja,” alisema Zitto.

Mbunge wa Kisesa, Luhaga Mpina (CCM), alipinga msimamo wa Werema wa kutaka kufuta mapendekezo hayo kwa maelezo kuwa kufanya hivyo ni kutoitendea haki hoja hiyo.

Hata hivyo, Mpina alimtaka Zitto pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje, Benard Membe, kuanza kutekeleza mapendekezo ya hoja hiyo kwa kutaja majina ya watu walioficha fedha nje ya nchi.

Hata hivyo, ilionekana kuibuka hoja upande wa serikali kumtaka Zitto ayataje majina ya watu anaodai wametorosha fedha nje ya nchi kwa kile kilichoonekana kutaka kumfanya akubaliane na kile ambacho kinapendekezwa.

Kauli za kumtaka Zitto awataje kwa majina ya watu hao ilizungumzwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera na Uratibu wa Bunge), William Lukuvi, na Waziri wa Tamisemi, Hawa Ghasia.

Baada ya mjadala huo mrefu huku hali ya kutoafikiana ikionekana kushindwa, alisimama Waziri Mkuu Mizengo Pinda ambaye alimtaka Zitto pamoja na wabunge wengine wakubali vyombo viendeleze uchunguzi.

Waziri Mkuu alimuomba Zitto awaunganishe na mchunguzi binafsi ambaye atawawezesha kukamilisha kazi hiyo na kisha matokeo yake kuyaleta katika mkutano wa 11.

Katika hoja hiyo, Zitto aliitaka serikali kuchukua hatua dhidi ya Watanzania walioficha fedha haramu nje ya nchi, ambapo sh bilioni 312 zinadaiwa kufichwa nchini Uswisi.

Zitto alisema watu walioficha fedha nje ya nchi wamekiuka sheria ya fedha za kigeni, ambayo inakataza mtu yeyote kuweka fedha nje hadi apate kibali cha Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Source: Tanzania Daima

No comments:

Post a Comment