HIKI NDICHO ALICHO KIANDIKA Mh. ZITTO KABWE KUHUSU KUSHINDWA KUHUDHURIA KATIKA TAMASHA LA MATUMAINI.
Global
Publishers leo 7.7.2013 waliandaa Tamasha la Matumaini. Bahati mbaya
sana sikuweza kuwahi kutokana na safari nilizonazo. Hii ni hotuba
niliyopanga kuitoa na kuwatumia waandaaji.
TAMASHA LA MATUMAINI
Leo nilikuwa niwe nanyi kwa ajili ya siku hii muhimu sana kwa nchi
yetu, siku ya matumaini kama inavyoandaliwa na Kampuni ya Global
Publishers. Napenda kutoa shukrani zangu za dhati kabisa kwa ndugu yangu
Erick Shigongo kwa kuandaa tamasha hili kila mwaka. Nasikitika kuwa
sitaweza kufanya pambano la ngumi na ndugu Ray na pia kuchezea timu
yangu ya Wabunge wa Simba dhidi ya watani zetu Yanga. Hata hivyo naamini
kuwa tamasha litakuwa na mafanikio makubwa na nipo nanyi japo sipo Dar
es Salaam.
Ilikuwa niwepo Dar es Salaam leo, lakini nimeshindwa
kuondoka Marekani kwa sababu Spika wa Bunge Mama Anna Makinda
ameniagiza kwenye safari nyingine ndefu kwenda visiwa vya Cayman na
baadaye Namibia kwa shughuli za Umoja wa Wabunge wa Jumuiya ya Madola.
Sikuweza kukwepa jukumu hili la kitaifa maana limekuja ghafla na mimi
nipo huku jirani na maeneo hayo. Naomba radhi sana kwamba sipo nanyi
leo.
Nawaomba muiombee amani nchi yetu na msimamie haki kwa
wananchi wote bila kubagua dini zao, rangi zao, hali yao kimaisha na
ufuasi wa vyama vya siasa. Mwaka huu tumeshuhudia matukio ambayo
yanatikisa msingi wa Taifa letu – Umoja. Hivi sasa msingi wetu una nyufa
ambazo kwa kweli hatujajua bado nini kinacholeteleza mambo haya kama
kulipua makanisa, kulipua mikutano ya vyama vya siasa na kuua viongozi
wa dini.
Matukio haya yanatuelekeza kuwa makini sana na kauli
zetu kwani baadala ya kuunganisha wananchi tunawezajikuta tunawagawa
zaidi Watanzania na hivyo kuwa na mzunguko wa machafuko (vicious circle
of violence). Ni wajibu wa viongozi wa kisiasa na wananchi kuepuka
kabisa kuanza kurushiana maneno na lawama kuhusu matukio haya, kwani
inawezekana lawama na maneno yetu yakawa yanampa nguvu adui wetu ambayo
hatujamjua bado.
Napenda niwakumbushe kwamba ni rahisi sana
kusambaza chuki na ni vigumu sana kuondoa chuki miongoni mwa wananchi.
Viongozi hatari kama Hitler walitumia sana mbinu ya kueneza chuki dhidi
ya jamii ya Jews na matokeo yake yalikuwa ni vita vikuu vya pili vya
dunia na zaidi ya watu milioni 6 wasio na hatia kupoteza maisha. Sisi
sote tuna jukumu moja la kuhakikisha tunajenga Taifa lenye kujali HAKI
na lenye mshikamano mkubwa miongoni mwa raia. Kwa nia hii tu ndio
tutaweza kuwa na Taifa imara lenye heshima mbele ya mataifa mengine
duniani. Ni kwa njia hiyo tu ndio tutaweza kutokomeza umasikini
uliokithiri mijini na vijijini hapa nchini kwa kuongeza uzalishaji na
kupanua ajira. Ikumbukwe bila HAKI hakuna AMANI na bila UWAJIBIKAJI
hakuna UTULIVU.
Tukiegemea siasa za CHUKI. Tukashindwa kuwa na
mahusiano ya kawaida miongoni mwa viongozi kuhusu masuala ya msingi ya
nchi. Tukashindwa kujadiliana kwa hoja kuhusu sera zetu. Tutapata
viongozi aina ya Hitler nchini mwetu. Wote tukatae. Sisi ni Watanzania.
Muwe na Tamasha jema la Matumaini.
Zitto Kabwe
7.7.2013, Aspen Colorado, USA.
No comments:
Post a Comment