Shirika la Viwango Tanzania (TBS), limebaini kuwa mafuta ya kula aina
ya Oki na Viking yaliyoenea sokoni nchini, yamebainika kuwa hayafai kwa
matumizi ya binadamu.
Kwa mujibu wa TBS, vipimo vyote vitatu
vilivyotumika kuyapima kuonyesha ubora, vimefeli na vimeonyesha mafuta
hayo kuharibika kwa haraka tangu yalipotengenezwa na mpaka leo.
Pamoja na Oki, mafuta mengine yenye
walakini ni Asma, Vikingi, Partiner na Premier Gold ambayo huuzwa kwa
dumu lenye ujazo wa lita 20 kwa bei ya kuanzia Sh 38,000 hadi 45,000,
wakati bei ya mafuta ya kula yanayotengenezwa nchini kwa ujazo huo
huuzwa kati ya Sh. 52,000 na Sh.55,000.
Baada ya kupimwa, Kaimu Mkuu wa Kitengo
cha Udhibiti Ubora TBS, Lazaro Msasalaga, anasema ilithibitika kuwa
mafuta ya Oki yanayozalishwa Malaysia na kupakiwa Singapore hayana
ubora.
Alisema mafuta hayo yametengenezwa 2011 na
kuonyesha mwisho wa kutumika ni Oktoba mwaka huu. Msasalaga alisema
walipoyachunguza wamebaini hayana namba ya ufuatiliaji wakati suala hilo
ni la muhimu kuwekwa.
Isitoshe, wawalipoyapima kutoka kipimo
kimoja kwenda kingine, majibu yake yalishindwa na kuzidi kuonyesha
mafuta hayo kuharibika kila walipoyapima.
Alisema kuna vipimo vya maabara ukipima vinaeleza mafuta kama yanafaa kutumika lakini kipimo hicho hakikufanikiwa.
“Inawezekana wakati wanayapakia
walichanganya na mafuta mengine kwani vipimo vyote vitatu vinavyoonyesha
ubora vimefeli na imeonyesha mafuta hayo kuharibika kwa haraka tangu
yalipotengenezwa na mpaka leo hii yapo masokoni wakati hayatakiwi kukaa
kwa muda huo,” alisema.
Msasalaga alisema kiasi cha maji yaliyopo
kwenye mafuta ukijumlisha na vitu vingine ni uchafu kwani hayakusafishwa
vizuri kuyaondoa maji hayo.
Kuhusu mafuta ya Viking, alisema na
yenyewe hayapo katika ubora kutokana na baadhi ya vipimo kushindwa kutoa
majibu. Alisema vipimo vitatu ambavyo vinatambulisha mafuta kuwa katika
ubora ni viwili na kimoja kimeshindwa.
Alisema maji yaliyochanganywa yapo sawa
ila kuna kipimo kimoja kimeshindwa kinachoashiria utunzaji wa mafuta kwa
muda mrefu bila kuharibika. Aidha, mafuta hayo hayatakiwi kukaa muda
mrefu kwani siyo salama.
Pia kiasi cha madini ambayo yana athari
kwenye afya kimezidi kiwango kinachotakiwa jambo ambalo halikutakiwi.
Mafuta haya kuingizwa nchini kinyemela ni jambo lingine la kuchukuliwa
hatua kisheria dhidi ya wahusika.
Mafuta hayo yanatokea nchini Malaysia na
kushushwa kisiwani Unguja, kisha kuingizwa Tanzania Bara kwa kutumia
majahazi yenye uwezo wa kubeba madumu zaidi ya 900 na kupakuliwa katika
‘bandari bubu’ ya Mbweni, Dar es Salaam.
Imedaiwa kuwa mafuta hayo yamekuwa
yakishushwa katika bandari bubu kwa lengo la kukwepa kodi na kuuzwa kwa
wafanyabiashara wa Tanzania. Hali hiyo inayohujumu uchumi wa taifa na
kuathiri afya za walaji, inafanyika huku jiji hili likiwa Makao Makuu ya
vyombo vya dola vyenye mamlaka na jukumu la kudhibiti uovu huu.
Uchunguzi wa NIPASHE Jumapili umebaini
kuwa licha ya mafuta hayo kutoka nje na kuuzwa kwa bei rahisi nchini,
viwanda vya ndani vilikuwa katika hali mbaya kutokana na mafuta hayo
kuua soko lake.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TBS, Joseph
Masikitiko, alisema shirika lake litatoa taarifa kupitia vyombo vya
habari ili wananchi wasiyatumie mafuta hayo.
TBS itahakikisha mafuta hayo yanaondolewa kwenye soko na wafanyabiashara wanayoagiza waache mara moja, alisistiza.
NIPASHE Jumapili ilibaini mafuta hayo
kuendelea kushushwa katika bandari 'bubu' ya Mbweni huku mengine
yakifichwa kwenye nyumba za jirani na eneo hilo.
Naye, Afisa Uhusiano wa Mamlaka ya TFDA,
Gaudensia Simwanza alisema kuwa mafuta hayo wameyasajili na kwamba
kitendo cha kuingizwa kinyemela nchini kitakuwa na walakini.
Alisema changamoto iliyopo ni bidhaa hizo
kupitishwa njia za panya na hata ubora wake unaweza usiwe salama na ndio
maana wanazipitishia huko.
Simwanza alisema huwa wanafuatilia sampuli
mbalimbali zilizopo masokoni na kwamba kwa sasa TFDA imejipanga
kuimarisha ukaguzi ili bidhaa hizo zisiingizwe katika soko pale
zinapobainika zimepitia njia za panya.
No comments:
Post a Comment