Mamlaka
ya Chakula na Dawa (TFDA) ni taasisi iliyoundwa chini ya Sheria ya
Chakula Dawa na Vipodozi Sura ya 219, ili kudhibiti ubora na usalama wa
vyakula, dawa, vipodozi, na vifaa tiba kwa lengo la kulinda afya ya
jamii dhidi ya madhara yatokanayo na matumizi ya bidhaa hizo. Imefahamika
kuwa mafuta yatokanayo na mimea hupendwa zaidi kuliko mafuta ya wanyama
kutokana na manufaa yake kiafya. Ili mafuta ya mimea yaweze kukidhi
vigezo vya ubora na usalama ni lazima yafanyiwe usafishaji (refining)
wakati wa usindikaji.
Hivi
karibuni kumekuwepo na ongezeko kubwa la matumizi ya bidhaa
zinazotokana na ubuyu ikiwa ni pamoja na mafuta yanayotokana na mbegu,
unga wa mbegu na majani ya mbuyu.
Taarifa za kisayansi zinaonesha kuwa mafuta ya ubuyu yana kiwango kikubwa cha tindikali ya mafuta aina ya cyclopropenoic
fatty acids ambayo huweza kusababisha athari ya kiafya endapo mafuta
hayo yatatumika kama chakula. Kiwango cha tindikali ya cyclopropenoic
fatty acids huweza tu kupunguzwa katika mafuta ya mbegu za ubuyu kwa
kuchemsha mafuta hayo katika nyuzi joto 180 kwa muda wa saa nane (8) au
kwa kutumia teknolojia ya kutengeneza mafuta mgando (hydrogenation). Kwa
sasa hapa nchini hakuna aina ya usindikaji unaofanyika wenye uwezo wa
kuondoa tindikali ya cyclopropenoic fatty acids katika mafuta ya mbegu
za ubuyu.
Baadhi ya athari zinazoweza kutokana na
matumizi ya mafuta ya ubuyu yenye tindikali ya cyclopropenoic fatty
acids ni pamoja na kuathiri vimeng’enyo (enzymes) vinavyosaidia katika
uchakataji wa tindikali za mafuta mwilini (fatty acid biosynthesis).
Aidha, taarifa za kisayansi zinaonesha
kuwa matumizi ya mafuta yenye kiasi kikubwa cha cyclopropenoic fatty
acids sanjari na matumizi ya vyakula vilivyochafuliwa na sumu kuvu aina
ya aflatoxin B1 ambayo inazalishwa na ukungu (fungus) katika baadhi ya
vyakula kama vile mahindi na karanga huongeza uwezekano wa kuugua
saratani.
Hadi sasa hakuna kiwango chochote cha
ubora na usalama cha kitaifa au kimataifa cha mafuta yatokanayo na mbegu
za ubuyu. Ili kuepuka athari zinazoweza kujitokeza kutokana na matumizi
ya mafuta ya mbegu za ubuyu, jamii inashauriwa kuepuka ulaji wa mafuta
hayo.
Hata hivyo, tafiti za kisayansi
hazijabainisha athari za kiafya zinazoweza kutokana na ulaji wa bidhaa
nyingine zitokanazo na ubuyu kama vile unga wa ubuyu na majani ya mbuyu.
TFDA inatoa wito kwa wananchi na jamii
kwa ujumla kushirikiana katika jukumu la kulinda afya za walaji kwa
kutoa taarifa pale wanapouziwa au kuhisi kuwepo kwa chakula, dawa,
vipodozi na vifaa tiba duni na bandia ambavyo havikidhi viwango vya
usalama na ubora au pale sheria inapovunjwa ili hatua stahiki ziweze
kuchukuliwa kwa wahusika.
Kwa maelezo zaidi usisite kuwasiliana nasi kupitia;
Mkurugenzi Mkuu,
Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA)
Barabara ya Mandela, Mabibo External,
S.L.P 77150
Dar Es Salaam, Tanzania
Simu: +255 22 2450512/2450751/2452108
Fax: +255 22 2450793
Barua pepe: info@tfda.or.tz
Tovuti: www.tfda.or.tz
No comments:
Post a Comment