ALIYEKUWA NAIBU KATIBU MKUU WA CHADEMA NA NI MBUNGE WA KIGOMA KASKAZINI MH. ZITTO ZUBERI KABWE AKIZUNGUMZA NAWAANDISHI WA HABARI MAPEMA LEO JIJINI DAR ES SALAAM
1. Utangulizi
Katika kikao chake cha siku mbili kilichofanyika tarehe 20 - 22 Novemba 2013, Kamati Kuu ya CHADEMA, pamoja na mambo mengine, iliazimia kunivua nafasi zangu zote za uongozi ndani ya chama. Kwa mujibu wa taarifa ya chama iliyotolewa katika mkutano na waandishi wa habari siku ya Ijumaa tarehe 22 Novemba 2013, ilielezwa kwamba sababu za kuvuliwa uongozi mimi na Dk Kitila Mkumbo ni uhaini na hujuma kwa chama kutokana na waraka unaojulikana kama mkakati wa uchaguzi 2013. Ukweli ni kwamba waraka uliotajwa si sababu ya mimi kuvuliwa nafasi zangu za uongozi kama ilivyojadiliwa katika Kikao cha Kamati Kuu.
Sababu za kufukuzwa kwangu kama zilizojadiliwa katika kikao cha Kamati Kuu ni tuhuma lukuki ambazo si mara yangu ya kwanza kuzisikia zikijadiliwa ndani na nje ya vikao vya chama. Hitimisho la tuhuma hizi ni kwamba mimi nimekuwa nikikisaliti chama kwa kutumika na CCM na Usalama wa Taifa. Nitazianisha tuhuma hizi na kuzijibu kama ambavyo nimekuwa nikizijibu katika vikao mbalimbali vyama.
Ninatambua kwamba chama changu kinapita katika wakati mgumu sana sasa hivi. Nataka nitamke mapema sana kwamba mimi Zitto Zuberi Kabwe sitokuwa chanzo cha CHADEMA kuvunjika. Hiki ndicho chama kilichonilea na kunifikisha hivi nilivyo. Ningependa chama hiki mtoto wangu atakapokuwa mtu mzima na atakapoamua kujiunga na siasa aingie CHADEMA. Bado nina imani kubwa na chama changu na ninaamini ndicho kinachostahili kuendesha nchi jana, leo na kesho.
2. Kuhusu tuhuma mbalimbali zinazo elekezwa kwangu
Zipo tuhuma nyingi ambazo zimekuwa zikirudiwarudiwa katika vikao vya chama na nje ya vikao na baadhi ya viongozi wenzangu. Tuhuma hizi zinalenga kuonyesha kwamba mimi ni mbinafsi na kwamba ninapokea rushwa ili kukihujumu chama changu. Nitazianisha tuhuma kwa kifupi na kuzijibu kama ambavyo nimekuwa nikizijibu katika vikao mbalimbali vya chama.
i) Tuhuma kwamba sikushiriki kumpigia kampeni mgombea wetu wa urais katika uchaguzi wa mwaka 2010. Ningependa kueleza yafuatayo kuhusu jambo hili:
- Mimi nilikuwa mgombea wa ubunge katika Jimbo la Kaskazini huko Kigoma.
- Pamoja na kuwa mgombea wa ubunge, nilifanya kampeni katika majimbo mengine 16 katika mikoa mbalimbali, ikiwemo Dar es Salaam, Mtwara, Pwani, Shinyanga, Mara na Rukwa. Hakuna kiongozi yeyote wa juu aliyefanya kampeni katika majimbo mengi kama mimi, ukiacha mgombea urais.
- Kote nilipopita nilimpigia kampeni wagombea wetu wa udiwani, ubunge na Rais.
- Katika Mkoa wa Kigoma nilizunguka na mgombea urais katika kata zote za Kigoma Kaskazini na majimbo yote manane ya Mkoa wa Kigoma.
ii) Tuhuma kwamba katika Mkoa wa Kigoma nilishindwa kuwapigia kampeni wagombea wetu kiasi kwamba peke yangu ndiye niliyeshinda katika uchaguzi huo. Ukweli ni kwamba niliwapigia sana kampeni wagombea wetu, na hivyo ndivyo wapiga kura wa Kigoma walivyoamua.
iii) Tuhuma kwamba nilishiriki kuwashawishi wagombea wetu katika baadhi ya majimbo kujitoa katika uchaguzi wa mwaka 2010 ili kuwapisha wagombea wa CCM wapite bila kupingwa kwa njia ya rushwa. Majimbo yanayotajwa ni pamoja na Sumbawanga, Musoma Vijijini na Singida Mjini. Kama nilivyokwisha kueleza katika vikao mbalimbali vya chama jambo hili si la kweli na hakuna popote ambapo watoa tuhuma hizi wamewahi kutoa ushahidi kwamba nilifanya jambo hili. Nipo tayari kwa uchunguzi ndani ya chama na watoa tuhuma waje na ushahidi bayana wa jambo hili. Si afya kwa chama kuendelea kurudiarudia tuhuma hizi kila mara tangu mwaka 2010 bila uchunguzi wowote kufanyika na jambo hili lifikie mwisho.
iv) Tuhuma kwamba nimekuwa sishiriki katika operesheni mbalimbali za chama: Ukweli ni kwamba nimeshiriki sana katika operesheni mbalimbali za chama ndani na nje ya nchi. Kwa mfano, mwaka 2011 tulikuwa na operesheni kubwa katika mikoa ya Kanda ya Nyanda za Juu Kusini na nilikwenda katika mikoa yote tuliyotembelea. Mwaka 2012 baada ya hoja ya mkonge bungeni nilifanya ziara Mkoa wa Tanga. Mwaka 2012 kulikuwa na operesheni kubwa moja katika mikoa ya kusini ya Mtwara na Lindi. Operesheni hii sikushiriki kwa sababu nilikuwa nchini Marekani kufungua matawi kwa mwaliko wa Watanzania wanaoishi huko.
v) Tuhuma kwamba nimekidhalilisha chama kwa tamko la PAC kwamba Hesabu za Vyama hazijakaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG): Katika jambo hili ninatuhumiwa kwamba mimi kama Naibu Katibu nilipaswa kuwasiliana kwanza na viongozi wa chama 'kuwatonya' ili wajiandae. Kwamba kutokuwatonya kumekidhalilisha chama na kukiweka kundi moja na CCM na nastahili kuadhibiwa vikali kwa kuwa katika taarifa yangu nilikuwa na nia mbaya na chama chetu. Maelezo yangu niliyoyatoa na ambayo ningependa kuyakariri hapa kuhusu jambo hili ni kama ifuatavyo:
- Utawala bora hautaki mimi kutumia nafasi yangu ya uenyekiti wa PAC kulinda chama changu na kuonea vyama vingine. Kufanya hivyo ni kuendeleza tabia zile zile ambazo tunazipinga na ambazo tunapigania kuzibadilisha
- Napenda kusisitiza kwamba hakuna chama ambacho kimewahi kukaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG). Natambua kwamba mahesabu ya chama changu yamekuwa yakikaguliwa na wakaguzi wa nje kwa utaratibu tuliojiwekea. Lakini matakwa ya kisheria ni kwamba mahesabu ya vyama vya siasa hayajakaguliwa na CAG, na hili ni kosa la kisheria, bila kujali kosa hili ni la nani.
vi) Tuhuma kwamba mimi ni mnafiki katika kukataa kwangu kuchukua Posho za Vikao
Mtakumbuka kwamba mimi nilikataa kuchukua posho tangu mwaka 2011 kama ishara ya kuonyesha kwa vitendo msimamo wa chama chetu wa kupinga posho za kukaa na matumizi mengine yasiyofaa katika fedha za umma kama ilivyoanishwa kwenye Ilani yetu ya mwaka 2010-2015. Mtakumbuka kwamba hivi karibuni Mheshimiwa Lema amenishutumu kwamba kukataa kwangu kuchukua posho ni unafiki kwa sababu ninapokea posho kubwa zaidi katika mashirika ya umma ambapo mimi ni mwenyekiti wa kamati husika. Ninapenda kueleza yafuatayo kuhusu jambo hili:
- Sipokei posho yeyote ya vikao (sitting allowance) ndani na nje ya Bunge tangu mwaka 2011. Hii ni pamoja na vikao vyote katika Kamati za Bunge ninavyohudhuria. Mtu yeyote mwenye ushahidi vinginevyo auweke hadharani.
- Swala la kukataa posho (sitting allowance) ni swala la kiilani katika chama chetu, na kwangu ni swala la kimisingi zaidi. Katika Wilaya yangu vifo vya kina mama wajawazito ni 1900 kati ya wanawake 100,000 wenye ujauzito. Vifo hivi vinatokana na ukosefu wa huduma kwa sababu ya bajeti finyu. Ndiyo maana nilifurahi sana kwa chama chetu kuliweka swala la kupunguza matumizi ya Serikali katika Ilani, na kuondoa posho za wabunge, ambao tayari wanapokea mishahara mikubwa, kungesaidia sana kupatikana fedha ambazo zingeokoa vifo vingi vya kina mama.
- Jambo hili si suala la ugomvi baina yangu na Mheshimiwa Lema. Ni suala la msingi katika chama chetu.
3. Usambazaji wa Ripoti ya Siri kuhusu Zitto Kabwe
Hivi karibuni kulisambazwa waraka unaoitwa ripoti ya siri kuhusu mimi ukibeba lundo la tuhuma kwamba nimehongwa fedha nyingi ili kukihujumu chama changu. Waraka huu ulidaiwa kuwa umechomolewa kutoka makao makuu ya CHADEMA. Jambo hili pia lilijadiliwa katika kikao cha juzi kwa kifupi, na majibu ya viongozi wa chama ilikuwa ni kwamba waraka huu haukuandaliwa wala kusambazwa na makao makuu. Katika mchango wangu nililalamikia mambo matatu yafuatayo:
- Kwamba baadhi ya waliokuwa wanasambaza waraka ule walikuwa ni viongozi wa chama chetu. Bahati mbaya hadi leo hakuna hata mmoja ambaye amekwishachukuliwa hatua za kinidhamu. Ninaamini kwamba kuna siku watu hao watachukuliwa hatua kwa mujibu wa taratibu za chama chetu.
- Kwa kuwa chama kimekana rasmi kuhusika na waraka huu, nitaendelea na taratibu za kisheria ili kuhakikisha kwamba wote waliohusika kutengeneza hekaya ile wanachukuliwa hatua stahiki za kisheria.
4. Hitimisho
Ninatambua kwamba kuna watu walitegemea leo ningejibu mapigo na ningewazodoa watu kwa majina kama ilivyo kawaida katika siasa za Tanzania. Natambua pia kwamba, kama ilivyo kawaida wakati wa migogoro katika vyama vya siasa hapa Tanzania, kuna watu walitegemea leo ningetangaza 'maamuzi magumu'. Natambua kwamba wapo ambao wangependa kupata nafasi ya kuendelea kutumia suala hili katika harakati zao za kudhoofisha mapambano ya demokrasia na uthabiti wa siasa za ushindani nchini mwetu. Napenda wanachama wa CHADEMA na wapenda demokrasia na siasa safi wote nchini watambue kwamba mimi bado ni mwanachama mwaminifu wa chama hiki na nitakuwa wa mwisho kutoka kwenye chama hiki kwa hiari yangu. Nitafuata taratibu zote ndani ya chama katika kuhitimisha jambo hili.
Naomba wanachama waelewe kwamba mimi kama binadamu ninaumia ninapopigwa. Tuhuma ninazorushiwa ni kubwa na zinanikwaza. Tuache siasa za uzushi ili tujenge chama chetu na nchi yetu, ili hatimaye tuwakomboe Watanzania wenye matarajio na imani kubwa kwa chama chetu.
Kama mwanasiasa kijana niliyekaa katika siasa kwa muda sasa yapo mengi mazuri nimeyafanya. Lakini kuna maeneo nilipojikwaa na yapo makosa niliyofanya kisiasa katika maisha yangu ya siasa.
Kinachoendelea ndani ya chama chetu ni mapambano ya kukuza demokrasia. Ni mapambano baina ya wapenda demokrasia dhidi ya wahafidhina, waumini wa uwajibikaji dhidi ya wabadhirifu na wapenda siasa safi dhidi ya watukuzao siasa majitaka. Hii ni changamoto kubwa ndani ya chama chetu inayohitaji uongozi shupavu kuikabili. Nitasimama daima upande wa demokrasia. Kama alivyopata kunena mmoja ya wanasiasa maarufu, 'kiwango cha juu kabisa cha uzalendo katika nchi ni kukubali kutofautiana kimawazo', na ninatamani huu ndio uwe utamaduni wa chama chetu.
Kabwe Zuberi Zitto, Mb
Dar es Salaam.
24 Novemba, 2013
ALIYEKUWA MAKAMU MWENYEKITI WA CHADEMA DR. KITILA MKUMBO AKIZUNGUMZA NA WAANDISHI WA HABARI.
1. Katika kikao cha Kamati Kuu ya CHADEMA kilichofanyika tarehe 20-22 Novemba 2013, pamoja na mambo mengine, kulijadiliwa waraka wa siri unaojulikana kama Mkakati wa Mabadiliko 2013. Waraka huu ulilenga kujenga hoja ya kufanya mabadiliko ya uongozi na kuanisha mikakati ya ushindi kwa mgombea mlengwa katika uchaguzi mkuu ndani ya CHADEMA. Nilikiri kuwa nilikuwa naufahamu waraka huu, na kwamba nilishiriki kuuandaa na kuuhariri, na kwamba mimi ni mmoja wa wanachama wanaoamini kwamba kuna haja ya kubadilisha uongozi wa juu wa chama katika uchaguzi ujao ndani ya chama.
2. Katika mjadala, maudhui ya waraka huu yalionekana kwa wajumbe kwamba yalikuwa na mapungufu na yalikiuka misingi na kanuni zilizoanishwa katika Katiba ya Chama. Kwa kuwa katika chama cha siasa hoja za watu wengi ndizo hupewa uzito, na kwa kuwa dhamira na nia yangu ndani ya chama hiki imekuwa ni kusukuma mabadiliko ambayo watanzania wanayatazamia nje ya mfumo wa sasa wa utawala, nilikiri makosa yangu na kuwaomba msamaha wajumbe wa Kamati Kuu na viongozi wakuu wa chama, na kueleza kwamba nilikuwa tayari kujiuzulu na kubaki kuwa mwanachama wa kawaida. Wajumbe walikataa kukubali ombi langu la kujizulu bali walipitisha azimio la kunivua mimi na Mhe. Zitto Zuberi Kabwe nafasi zetu za uongozi. Nilipokea kwa unyenyekevu adhabu ya kuvuliwa nafasi zote za mamlaka nilizokuwa nazo ndani ya chama hiki na kueleza kuwa nitaendelea kutoa mchango wangu kama mwanachama wa kawaida hadi hapo chama kitakapoona ninafaa kukitumikia katika nafasi yeyote.
3. Kufuatia mkutano wa waandishi wa habari siku ya Ijumaa tarehe 22 Novemba 2013 ambapo, pamoja na mambo mengine, ilielezwa na viongozi wa CHADEMA kwamba mimi na wenzangu (Samson Mwigamba na Zitto Kabwe) tumehujumu chama na tumefanya uhaini kwa kuandaa mkakati wa ushindi kwa mgombea tunayemtaka, ningependa nieleza mambo yafuatayo:
a. Siamini hata kidogo kwamba kugombea nafasi yeyote iliyo wazi ndani ya chama cha siasa ni uhaini na hujuma. Msingi namba moja wa CHADEMA ni demokrasia na hakuna namna ya kudhihirisha mapenzi kwa demokrasia zaidi ya kuruhusu ushindani katika nafasi za uongozi na hasa uongozi wa juu kabisa. Hiki kinachoitwa uhaini ni wasiwasi wa siasa za ushindani katika chama chetu.
b. Sijawahi na sitarajii kushiriki vitendo vyovyote vya kuhujumu chama changu cha CHADEMA na harakati za mabadiliko hapa nchini. Chama hiki kiliniamini katika nafasi nyingi nyeti sana na kama mie ningekuwa mhujumu nilikuwa na fursa nzuri za kufanya uhujumu huo. Nimeshiriki kuandaa ilani ya chama ya 2010-2015, kuratibu kampeni za mwaka 2010 nikiwa makamu mwenyekiti wa kampeni chini ya Profesa Baregu na nilishiriki kutengeneza na kusimamia utaratibu mzuri wa kupata wabunge wa viti maalumu katika chama chetu. Zote hizi ni nafasi nyeti mno ambazo kamwe huwezi kumkabidhi mtu ambaye ni ‘mhaini’ na ‘mhujumu’. Nilishiriki katika shughuli za chama kwa kiwango ambacho nilijisababishia matatizo makubwa katika familia yangu na kazini, lakini sijawahi kutetereka na sijaterereka. Nilifanya yote haya kwa mapenzi yangu ya dhati na imani yangu kwa CHADEMA kwamba ndicho chama kinachostahili kuongoza harakati za mabadiliko hapa nchini kwa sasa.
c. Nasikitika kwamba nimesababisha usumbufu kwa viongozi wangu wa CHADEMA kutokana na dhamira yangu ya kutaka mabadiliko ya uongozi ndani ya chama chetu kwa njia halali za kidemokrasia. Nilifanya hivi kwa imani niliyo nayo kwa misingi ambayo CHADEMA inasimamia, ikiwemo demokrasia, na imani yangu kwamba chama hiki kinahitaji kufanya mabadiliko makubwa katika uongozi wa juu wa chama, ikiwa ni maandalizi muhimu kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2015. Nasisitiza tena kwamba siamini hata kidogo kwamba matamanio ya mabadiliko ya uongozi ndani ya chama, na kuandaa mikakati ya kufikia matamanio hayo kwa njia za kidemokrasia ni uhaini.
d. Tunaweza kujifunza kutokana na historia. Siasa za ushindani ndani ya vyama katika nchi hii sio kitu kigeni. Enzi za TAA na kabla TANU haijazaliwa wanachama walikuwa wanagawana nafasi za uongozi mezani. Lakini mwaka TANU ilipozaliwa (mwaka 1954) kulikuwa na uchaguzi mkali sana kwa nafasi ya uenyekiti. Mwalimu Nyerere alimshinda Mzee Skyes kwa kura chache sana. Rais Obama wa Marekani alianza mkakati wa kushinda uteuzi wa kugombea nafasi ya urais kupitia chama chake cha Democrat mapema kabisa mwaka 2006 kupitia waraka maalumu wa siri ulioainisha mikakati yake. Waraka huu uliandaliwa na watu wanne tu bila yeye mwenyewe kujua. Waandaji wa mkakati huu walikuja kumshirikisha baadaye mwaka 2007 na kumshawishi yeye ajitokeze kugombea dhidi ya Hillary Clinton aliyekuwa anachukuliwa kama mrithi halali wa kiti cha urais. Yaliyobaki ni historia. Hivi ndivyo ambavyo siasa za ushindani ndani ya vyama hatimaye huzaa wagombea na viongozi imara katika nchi.
e. Zitto Zuberi Kabwe hajafukuzwa kwa sababu ya waraka huu kwa sababu yeye hakuhusika kwa namna yoyote kuuandaa, ingawa alikuwa ni mlengwa mkuu. Yeye amefukuzwa kwa sababu ambazo yeye atazieleza na ambazo viongozi wa CHADEMA hawakuzieleza katika mkutano na waandishi wa habari.
f. Napenda ijulikane kwamba sikuomba kujiuzulu kwa sababu ya kuogopa aibu ya kufukuzwa. Niliomba kujiuzulu kwa sababu nilitambua kwamba wenzangu katika Kamati Kuu walikuwa hawana imani nami tena, na ni uungwana kujiuzulu mkifika mahala hamuaminiani. Nilitambua vilevile kwamba, kwa mujibu wa Katiba yetu, Kamati Kuu ilikuwa haina uwezo wa kunivua nafasi yangu moja kwa moja.
Kwa mujibu wa Katiba ya CHADEMA, Sura ya Sita, Ibara ya 6.3.6 (b), inasomeka hivi “Kiongozi aliyeteuliwa na vikao vya uongozi ataweza kusimamishwa au kuachishwa uongozi na kikao kilichomteua”. Mimi nilichaguliwa na Baraza Kuu na ni kikao hiki pekee chenye uwezo wa kunivua nafasi niliyokuwa nayo. Ninaamini wajumbe wa Kamati Kuu walipitiwa katika hili kwa sababu siamini kwamba hawajui takwa hili la kikatiba ukizingatia kwamba ndani yake kuna wajumbe waliobobea kabisa katika tasnia ya sheria.
4. Hiki kilichotokea ndani ya chama sio kitu kibaya. Vyama vingi imara hupitia katika migogoro na misukosuko kama hii na zaidi. Naamini tutavuka na tutakuwa imara zaidi. Muhimu ni kwamba ni lazima tuaminiane. Katika kuaminiana sio lazima tufanane kimawazo na kimtazamo kwa sababu hili ni jambo lisilowezekana kibinadamu na zaidi katika siasa.
5. Ninapohitimisha, ninawasihi wanachama wa CHADEMA na wapenzi wa mabadiliko popote walipo wapiganie kwa dhati MISINGI mama ya CHADEMA ikiwemo demokrasia ndani ya chama. Hakuna namna ambavyo chama chochote kinaweza kushawishi umma kwamba kitapigania demokrasia katika nchi wakati kinayahainisha mapambano ya kidemokrasia ndani ya chama chenyewe.
Kukataa siasa za ushindani ndani ya chama ni kuhujumu demokrasia na ni usaliti kwa misingi mama ya chama ambayo ni uhuru wa kweli na mabadiliko ya kweli. Hisia za usaliti na umamluki zilitumika enzi za ukomunisti katika kunyamazisha wapinzani ndani ya vyama vya siasa na katika nchi. Zilikuwa ni njia haramu zilizozoeleka ambazo hatimaye zilizaa udikteta wa kutisha katika mataifa ya kikomunisti. Tusikubali utamaduni wa kuhisiana usaliti na umamluki ukaota mizizi katika chama chetu na katika nchi kwa sababu utaua demokrasia na mfumo wa vyama vingi utakuwa hauna maana tena.
6. Nitafuata taratibu zote za chama kama zilivyoelekezwa na Kamati Kuu na kwa mujibu wa katiba yetu, na nitashiriki kikamilifu katika kutuliza hali ya kisiasa ndani ya chama ili kuhakikisha kwamba tunabaki imara, na CHADEMA inaendelea kuwa tumaini la watanzania.
Mungu ibariki Tanzania.
Dkt. Kitila Mkumbo
Dar es Salaam
Jumapili, 24 Novemba 2013.
No comments:
Post a Comment