Kwa niaba ya baraza la uongozi la mkoa wa Arusha, napenda kuujulisha
umma wote kwa ujumla kuwa mwenyekiti wa wilaya ya monduli Mchungaji
Amani Silanga Mollel amekoma/amesimamishwa kuwa Mwenyekiti wa CHADEMA
wilaya ya monduli kuanzia tarehe 29 Novemba 2013 kufuatia tuhuma nzito
za uvunjifu wa kanuni za maadili ya chama.
Hatua hii imefikiwa
baada ya kuthibitika na yeyé mwenyewe kukiri mbele ya kikao cha kamati
tendaji ya wilaya ya monduli kilichoketi tarehe 29 Novemba 2913 saa NNE
asubuhi kuwa alitoa tamko batili akitumia wadhifa wa mwenyekiti wa
wilaya bila ridhaa ya kamati tendaji na huku akidanganya kuwa ni tamko
kwa niaba ya wilaya ya Monduli.
Katika tamko lake ametoa tuhuma
dhidi ya wajumbe wa kamati kuu na viongozi wakuu wa kitaifa kwa maamuzi
halali ya kikao cha kamati kuu huku akijua kuwa anavunja kanuni za
chama kwa mujibu wa katiba ya chama toleo la mwaka 2006 ya Kanuni za
uendeshaji kazi za chama, sura ya KUMI, ibara ya 10 (X) “Kiongozi asitoe
tuhuma zozote juu ya viongozi wenzake pasipo kupitia vikao halali na
kuzingatia taratibu na ngazi zilizoelezwa kwenye kanuni za chama”.
Sambamba na hilo, Mchungaji Amani Silanga ametoa tuhuma za uzushi,
uongo na upotoshaji na kutaka kuaminisha jamii kuwa chadema ina makundi
ya CHADEMA Asili na CHADEMA Family kitu ambacho ni upotoshaji mkubwa na
wa hatari kwa ustawi na umoja wa chama na kinyume na kanuni za
uendeshaji kazi za chama, sura ya KUMI, ibara ya 10 (VII), “Kiongozi
anatakiwa kuwa mkweli na muwazi wakati wote hususani katika vikao halali
na aachane na vikundi vya majungu, wadanganyifu (Rumour Mongers). Ni
mwiko kwa kiongozi kujihusisha na upotoshaji wa maamuzi wa vikao
halali”.
Kamati tendaji ya wilaya ilipomtaka aonyeshe CHADEMA
asili ni kina nani na CHADEMA family ni kina nani alishindwa kutoa
maelezo yoyote ya maana na kufikia hatua ya kutaka kuvuruga kikao kwa
kuleta vijana wahuni wapatao 17 ndani ya kikao ambao wengi walijulikana
kuwa sio WANACHADEMA. Katika utambulisho wake wa majigambo Mchungaji
Amani SIlanga kwa kiburi na kejeli amejitambulisha na kukiri kuwa yeye
yupo kambi ya Zito Kabwe na hakuna wa kumfanya kitu maana ni mjumbe wa
baraza kuu la chama. Maneno yake yalidhihirisha kuwa Mchungaji Amani
Silanga anashiriki mpango wa kuunda makundi yasiyo na tija ndani ya
chama na hivyo kuwa kinyume na sura hiyo hiyo ya kumi ya kanuni za
uendeshaji kazi za chama ibara ya 10 (IX), “Kiongozi asijihusishe au
kushiriki na vikundi au vitendo vya kuchonganisha au kuzua migogoro
ndani ya uongozi wa chama au wanachama wake”.
AZIMIO LA BARAZA LA UONGOZI LA MKOA WA ARUSHA:
Baraza la uongozi la mkoa lililoketi tarehe 29 Novemba 2013, limepokea
mapendekezo ya kamati tendaji ya wilaya na kuzingatia hofu kubwa
iliyoainishwa na kamati tendaji kufuatia matendo mengi yanayotia shaka
ya uadilifu na uwezo wa kiuongozi wa Mchungaji Amani Silanga na hivyo
baraza la uongozi la mkoa limeridhia kuwa amevunja kanuni za maadili ya
chama sura ya KUMI ibara ya (VII) hadi (XII) na hivyo kupelekea ukomo wa
yeye kuwa Mwenyekiti wa wilaya kuanzia tarehe 29 Novemba 2013. Baraza
la mkoa likiwa mamlaka ya nidhamu kwa mujibu wa katiba ibara ya 6.3.6
(a) (iv) limemjulisha tuhuma zake na hatua hii stahiki iliyochukuliwa.
Kwa vile Mchungaji Amani Silanga alikiri kosa hili mbele ya kamati
tendaji ya wilaya bila kulijutia au kuomba msamaha, baraza la mkoa
limechukua hatua hii stahiki kwa maslahi ya chama na kuwa uchunguzi
zaidi utafanyika ili kufikia maamuzi makubwa zaidi ya tuhuma nyingi kwa
mujibu wa kanuni za hatua za kinidhamu.
Baraza la uongozi la
mkoa wa Arusha, linatoa onyo kwa wote ambao wapo katika mtandao huu
mchafu, ama watoke wenyewe mapema maana hawatavumiliwa kamwe. Baraza la
uongozi wa mkoa liliona kuwa Mchungaji Silanga amepotoka na hivyo yeyé
kuendelea kuwepo ndani ya chama wakati wa uchunguzi wa tuhuma hizi nzito
dhidi yake ni hatari zaidi kwa ustawi wa chama na hivyo baraza
likaridhia kwa kuzingatia tafsiri ya katiba ya chama ibara ya 6.3.4 (c)
wa yeyé kukoma uongozi na hivyo akae nje kwa muda na waliopotoka
wenzake.
Amani Golugwa
Katibu wa CHADEMA – Mkoa wa Arusha.
(Kwa niaba ya Baraza la Uongozi la Mkoa wa Arusha)
Tarehe 30 Novemba 2013
No comments:
Post a Comment