NIMEKUWA nikifuatilia kwa karibu sana matukio yanayotokea katika Jumuia ya
Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi CCM (WAZAZI) tangu Uongozi mpya ulipoingia
madarakani mwaka 2012.
Ni ukweli ulio dhahiri kuwa mwaka 2012 ulikuwa ni mwaka wa
chaguzi ndani ya CCM na jumuia zake yaani UVCCM, UWT(CCM) na WAZAZI.
Ndani ya Jumuia ya Wazazi CCM uchaguzi wa 2012 ulishuhudia kuchaguliwa kwa viongozi wapya akiwemo Mwenyekiti wa Taifa Bw. Abdallah
Bulembo.
Siyo yeye pekee yake uchaguzi huu pia ulishuhudia sura mpya
nyingi zikichaguliwa kama Wenyeviti wa mikoa na wilaya na kama
mfano tuu mkoani Kilimanjaro Bw. Festus Kilawe alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa
Mkoa akichukua nafasi ya Mwenyekiti wa zamani Bw. Thomas Ngawaia.
Baada ya kuchaguliwa Bw. Bulembo yeye peke yake na
kwingineko akishirikiana na Katibu Mkuu wake Taifa Bw. Seif Shaaban Mohamed
walianza kupanga safu mpya ya uongozi na utendaji katika chama hiki katika
mikoa, wilaya na taasisi zilizoko chini ya jumuia hii ya WAZAZI sehemu mbali
mbali nchini.
Bila kutarajiwa wengi wa viongozi na watendaji walioteuliwa
na Bw Bulembo ili kushika nyadhifa mbali mbali katika mikoa, wilaya na taasisi
husika wamekuwa ni watu wasiokuwa na sifa.
Aghalabu wengi wa watendaji walioteuliwa wamekuwa ni wale
waliompigia debe Bw, Bulembo katika uchaguzi wa 2012.
Ukweli ni kuwa teuzi hizi hazikufuata kabisa vigezo, uzoefu
wala uwezo wa mtu bali kuwa karibu na Bw. Bulembo.
Kiama kimekuja kwa wale wote watendaji na viongozi katika
jumuia hii ambao hawakuwa wapiga debe wa Bw. Bulembo.
Bw. Bulembo sasa sio kiongozi wa kisiasa tena bali mtendaji
mkuu wa jumuia hii ya wazazi hali inayojidhihirisha kupitia maamuzi
aliyoyafanya tangu aingie madarakani.
Kama mfano kati ya mifano
mingi ni maamuzi au maagizo yaliyotolewa na Bw. Mkubwa huyu katika shule za
sekondari zinazomilikiwa na wazazi mkoani Kilimanjaro.
Upo ushahidi wa kimaandishi ambapo Bw. Bulembo aliwaagiza
wakuu wote wa shule hizo kupeleka makao makuu ya Wazazi Jijini Dar es salaam
shilingi Elfu Thelathini (30,000/-) kutoka katika kila sehemu ya ada anayolipa
mwanafunzi katika shule husika yaani kwa kila kichwa cha mwanafunzi.
Shule husika mkoani Kilimanjaro ni Kibo, Namfua, Mango, Minja,
Hedaru, Wari na Kahe ambapo kwa mwaka 2013 lazima shilingi 30,000/= kwa kila
mwanafunzi ziende makao makuu ya wazazi huku katika mwaka 2014 kila kichwa cha
mwanafunzi kitalipa shilingi laki moja (100,000/-) pesa ambazo zitakatwa katika
kila ada ya wanafunzi husika.
Inasemekana na kuaminika kuwa kama
ilivyo katika maagizo ya Bw. Bulembo mwanafunzi atakayeshindwa kulipa ada katika
shule husika na afukuzwe mara moja.
Baya zaidi upo ushahidi wa kutosha kuwa katika shule ya
sekondari ya Kibo iliyoko maeneo ya Shanty Town mjini Moshi kuwa Bw.
Bulembo ametishia kuivunja bodi ya shule hiyo kutokana na kumpinga au kupinga
maamuzi yake.
Ipo barua ya tarehe 7/8/2013 iliyoandikwa na Mwenyekiti wa
Bodi ya Shule husika Bw. Athumani Ally Hassan ambayo pamoja na mambo mengine
ilihoji uhalalai wa Bw. Bulembo kuchukua bila maandishi au makabidhiano hati ya
ardhi ya shule ya sekondari ya Kibo (Certificate of Occupancy).
Inadaiwa katika barua hii kuwa Bw. Bulembo alitaka kuuza
sehemu ya ardhi ya shule hiyo.
“Bodi inategemea hati ya ardhi ya shule (certificate of
occupancy) uliochukua bila makubaliano na pasipo kuwekwa kumbukumbu yoyote ya
kimaandishi yanayoonyesha hati hiyo inahitajika wapi.
Tunaamini kuwa hati hiyo haitatumika katika kuuza sehemu yoyote
ya ardhi ya shule” inasomeka sehemu ya barua husika iliyopelekea Bw. Bulembo
kutaka kuivunja Bodi ya shule husika.
Mtu anaweza kuhoji je shule hizi za WAZAZI ambazo awali
zilikuwa kimbilio la wanyonge sasa kwa nini zimegeuka kama
jehanamu ya wanyonge.
Ufaulu katika shule hizi ni wa chini sana
kwani shule hizi hazina vitabu, maktaba, maabara na pia mishahara ya waalimu
katika shule hizi ni kidunchu sana.
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Mfuko wa Hifadhi ya
Jamii (NSSF) kwa pamoja zinadai shule husika mkoani Kilimanjaro mamilioni ya
shilingi.
Baya zaidi ni ukweli kuwa wakati haya yakitokea bado shule
husika zinazomilikiwa na WAZAZI nchini zililazimika kugharamia ziara za Bw.
Bulembo mikoani.
Vyanzo vya habari ambavyo havikutaka kunukuliwa vimebaini
kuwa shule husika katika mikoa ya Kilimanjaro, Tanga na Mbeya zimekamuliwa
mamilioni ya shilingi ili kugharamia ziara za Bw. Bulembo na msafara wake
katika mikoa husika.
“Shule za sekondari mkoani Kilimanjaro ziligharamia shilingi
milioni 12.9 katika ziara ya Bw. Bulembo iliyofanyika mkoani Kilimanjaro tarehe
15-22 June, 2013.
Shule za Tanga zilitoa shilingi milioni 14 wakati zile za
Mbeya zilichangia jumla ya shilingi milioni 10 ili kugharamia ziara za Bw
Mkubwa huyu” vimebaini vyanzo hivi vya habari.
Upo mkutano uliofanyika mwezi Juni 2013 katika Ukumbi wa
Ilala Boma jijini Dar es salaam
ambapo wakuu wa shule za sekondari nchini zinazomilikiwa na WAZAZI walikabidhi
WAZAZI Makao Makuu jumla ya shilingi milioni 231.
Tunaweza kuhoji je michango hii ya mamilioni ya shilingi
kutoka shule husika kwenda Makao Makuu ya WAZAZI ni kwa manufaa ya nani haswa?
Mbona hali kama hii haikuwepo kabla ya Bw.
Bulembo kuingia madarakani?
Ni dhahiri kuwa kama hali hii ikiachwa bila kukemewa au
kuchukuliwa hatua na mamlaka husika kama CCM na Mwenyekiti wake wa Taifa Bw.
Kikwete huenda shule husika zikafungwa kwa kushindwa kujiendesha.
Tutarajie nini katika shule hizi kama
sio hali kuendelea kuwa mbaya zaidi kwani vitabu havitanunuliwa, maktaba
hazitawekwa, maabara tusahau huku mishahara ya waalimu ambao sasa wanakaa miezi
3-6 bila kupewa sasa wataikosa kabisa.
Nani basi atamfunga paka kengele na kuliokoa Jahazi hili
linalokwenda mrama katika Jumuia hii ya WAZAZI?
Mungu ibariki Tanzania na Mungu na azinusuru
shule hizi za WAZAZI kutoka mikononi mwa Nahodha wa Jahazi hili ambalo sasa
linakwenda mrama.
No comments:
Post a Comment