Banner

Banner

FOLLOW US FACEBOOK

propertyfinder.co.tz

Wednesday, June 18, 2014

WATANZANIA TUSISUBIRI WAGENI KUSAIDIA WATOTO WALIO KWENYE MAZINGIRA MAGUMU

WATANZANIA wameshauriwa kuwasaidia watoto walio kwenye mazingira magumu walio kwenye maeneo wanayoishi, badala ya kuwatelekeza ama jukumu hilo kuwaachia watu walioko mbali, wakiwemo wafadhili kutoka nje ya nchi ya Tanzania.

Mkurugenzi wa shirika la Compassion International Tanzania, katika kijiji cha Msoga, kata ya Lugoba, Gombo Kahabi, amesema shirika hilo kwa kushirikiana na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania, (KKKT), walibaini mazingira magumu yaliyokuwa yakiwakabili watoto wengi wa eneo hilo, na kuamua kuwasaidia kwa kuwapatia wafadhili toka nje ya Tanzania.

Amesema hadi sasa waliweza kuwapata watoto 270 walio katika mazingira magumu ya kijiji hicho ambao wanapatiwa ufadhili katika masuala ya elimu, afya na hata malazi na kutoa wito kwa jamii kuwasaidia katika ukamilishaji wa miundo mbinu ya majengo ya kituo hicho ili wazazi na walezi wa watoto wanaohudumiwa, waweze kujifunza ufundi na kumudu kusaidia familia hata pale wahisani wanapokosekana, kutokana na watoto hao kuishi majumbani.
Gombo amesema pamoja na msaada huo, wameendelea kuibua vipaji vya watoto hao ikiwemo katika suala la uimbaji, na wamekusudia hadi mwakani, kurekodi na kutoa albamu ya watoto hao wadogo, ambao wanaamini itakuwa ni mwanzo mzuri wa kusaidia watoto hao.
Naye Muinjilisti wa KKKT mtaa wa Msoga, Sifu Dunia, amesema maeneo mengi ya mkoa wa Pwani hususani vijijini, bado kuna changamoto ya wazazi na walezi kukosa mwamko wa kuwapeleka watoto wa kike shuleni, na kwamba mpango huo wa compasion na KKKT, ulisaidia kundi kubwa la watoto ambao huenda kama wangekosa msaada huo, wangekuwa katika mazingira mengine.

Amewahimiza wazazi na walezi kutambua umuhimu wa Elimu kwa watoto wote bila kubagua, kwani hiyo ni haki yao ya msingi, na kwamba elimu ni njia muafaka ya kuwafanya watoto kujisaidia wenyewe hata wanapokuwa wakubwa.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Msoga, Herman Semindu, amesema kijiji hicho kimeendelea kukabiliana na changamoto ya ukatili na unyanyasaji wa watoto, na kama serikali wameendelea kutoa elimu kwa wananchi kusaidiana wenyewe kwa wenyewe, hasa kwa wale walio katika mazingira magumu.

Semindu ameipongeza KKKT kwa kushirikiana na shirika la Compasion kusaidia idadi kubwa ya watoto kwa kuwapatia wafadhili watakaowasomesha na kusaidia watoto kwa kuwakatia bima ya afya iwasaidie kwenye matibabu.

No comments:

Post a Comment