Huu ni mtambo wa kutengenezea pombe haramu ya gongo.
KILIMANJARO Mkuu wa Wilayani Hai, Mkoani Kilimanjaro, Bwana Antony Mtaka alisema kuwa wazazi na walezi wengi wamesahau kuwalea watoto wao katika maadili mema na kuwafanya hali inayowafanya vijana wengi kutokuwa na heshima pia kujiingiza kwenye vitendo viovu, ikiwa ni pamoja na uvutaji bangi na unywaji pombe haramu ya gongo.
Hayo yalisemwa hivi karibuni na Mkuu huyo wa Wilaya na Hai, katika uzinduzi wa Katiba ya chama cha wazee wilaya ya Hai, sambamba na harambee ya kuwachangia wazee hao uliofanyika katika ukumbi wa Papaa Bomang'ombe Wilayani humo, ambapo mkuu huyo alichangia shilingi laki tano, Mjumbe wa Nec, Fuya kimbita alichangia shilingi laki mbili.
Mtaka alisema ni jukumu la wazazi na walezi kuhakikisha watoto wanalelewa kwenye maadili yanayostahili ili tuwe na kizazi kinachofaa siku za usoni, siku hizi mtoto anaanza kusoma darasa la kwanza hadi anamaliza chuo hajawai kukaa na mzazi akamfundisha maadili mema, huyo mtoto anaiga maadili ya mtaani mwisho wa siku wazazi wanaanza kulalamika kuwa watoto hawana heshima kumbe sisi wenyewe hatujakaa nao na kuwafundisha hayo maadili tunayotaka.
''Watoto hawafuati maadili kama zamani na sisi Wazazi tupo tunaangalia tuu, Wazazi Wenzangu ifike mahala tubadilike na tuwalee Watoto wetu katika maadili yanayokubalika na jamii." Alisema Mkata
Alitaja maadili yasiyokubalika kuwa ni pamoja na mavazi yanayovaliwa na watoto wa kike ya nusu uchi na wakiume kuvaa suruali chini ya makalio, Watoto wa kike kurudi nyumbani muda wanaotaka wao tofauti na zamani ambapo watoto wa kike ilikuwa mwisho saa 12 jioni kufika nyumbani.
Wazazi wa siku hizi tumekuwa wakimya mno, mtoto wa kike anafika nyumbani saa mbili za usiku hata kumuhuliza alikuwa wapi hakuna na akija na kitu ambacho haujamnunulia wewe wala haumuulizi hata kama unajua hana kipato chochote cha kufanya anunue kitu hicho, jamani tunawapeleka wapi watoto wetu, alisema matendo haya yamekuwa yakisababisha ongezeko la mimba za utotoni ambazo zimekuwa ni chamngamoto kwa watoto wakike.
Pia ametaka Wananchi wa Wilaya hiyo kuacha kunywa pombe za aina mbalimbali kama gongo, viroba, alisema Vijana wengi wa Wilaya hiyo wamekuwa wakitumia kilevi hicho kwa wingi na kushindwa kutekeleza majukumu yao mbalimbali, ikiwamo shughuli za uzalishaji mali kurudi nyuma jambo ambalo ni hatari kwa Taifa letu
Kutokana na hali hiyo amewataka Wazazi na Walezi kuwalea Watoto wao katika maadili mema kama ilivyokuwa zamani ili Taifa liwe zuri na pia kupata Viongozi Bora watakao tuongoza baadae.
Katibu msaidizi wa kikundi hicho Hashimu Swai alisema kuwa Wazee wa Wilaya hiyo wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwamo ya matibabu na chakula, alisema wamekuwa wakinyanyaswa pindi wanapofika katika vituo mbalimbali vya Afya ikiwamo hospitali ya wilaya kwa ajili ya kupatiwa matibabu utaambiwa dawa hakuna, ambapo mkuu huyo alisema atashughulikia changomoto hizo.
No comments:
Post a Comment